Mama Kanumba ajitenga na filamu za mwanaye

Mama Kanumba ajitenga na filamu za mwanaye

Mama wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa amesema tangu mwanaye afariki dunia hajawahi kuangalia filamu yake hata moja kwasababu zinamuumiza licha ya kuwa anazikubali kazi hizo.

Mama Kanumba ameyasema hayo leo Septemba 7, 2024 katika Tamasha la Faraja ya Tasnia ambalo linafanyika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwaenzi mastaa mbalimbali waliotangulia mbele za haki.

“Kwanza tangu ameondoka duniani siangaliagi movie (filamu) yake hata moja. Kwa hiyo movies zote mimi nazipenda ila siangaliagi nimejitahidi sana lakini hilo limenishinda,” amesema Mama Kanumba

Kanumba alizaliwa Januari 8, 1984 mkoani Shinyanga na alifariki dunia Aprili 7,2012 akiwa na umri wa miaka 28.

Ni miongoni mwa wasanii wanaoenziwa leo katika viwanja vya Leaders Club kwenye tamasha la Faraja ya Tasnia litakalokuwa likifanyika kila mwaka mara moja.

Amewahi kutamba na filamu kama ‘Magic House’, ‘Big Daddy’, ‘This is it’, ‘Kijiji cha tambua haki’ na nyinginezo nyingi.

Mbali na hayo mama wa mwigizaji Othman Njaidi ‘Patrick Kanumba’ amesema Kanumba amejenga historia kubwa kwenye maisha ya kijana wake.

“Kanumba ana historia kubwa sana kwenye maisha ya Patrick kuliko hata kaka zake aliozaliwa nao, kwa sababu Kanumba ndiyo alikuwa amemshika mkono amemtoa kwenye fani hii na kila kukicha anamkumbuka, hajawahi kumsahau hata siku moja," amesema mama mzazi wa Patrick

Hata hivyo aliendelea kueleza kuwa kuna mipango ambayo mwanaye ameiandaa kwa ajili ya kumuenzi Kanumba pamoja na kusherehekea kutimiza miaka 15 katika tasnia ya uigizaji.

Utakumbuka kuwa Kanumba ndiye alivumbua kipaji cha Patrick alifanikiwa kuigiza naye filamu kama 'Uncle JJ', 'This is it' na nyinginezo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags