Mahusiano:Kupenda kupita kiasi ni tatizo la homoni

Mahusiano:Kupenda kupita kiasi ni tatizo la homoni

 

Tunajiuliza siku zote ni kwa nini penzi linapoingia mahali huweza kuharibu kila kitu? Tumekuwa na misemo yetu ya siku nyingi kama siyo ya asili, kama vile ule wa ‘penzi ni ulevi’ au ‘penzi ni upofu’ na mingine yenye kuonyesha kwamba penzi lisipoangaliwa kwa makini linaweza kuleta athari mbaya na kubwa kwa binadamu.

Ni nani ameshawahi kujiuliza ni kwa nini hali hiyo hutokea? Kuna yeyote ambaye hata mara moja ameshawahi kujiuliza ni kwa nini penzi halina shujaa au mnyonge pale linapoingia wote huwa kama waliopagawa? Bila shaka sio wengi, kama wapo ambao wameshawahi kujiuliza swali hili. Kila mmoja anadhani ndivyo ilivyo na hakuna awezaye kujua ni kwa nini.

Ukweli ni kwamba penzi halina tofauti na ulevi sugu kama ule wa pombe au madawa ya kulevya. Penzi linaelezwa kwamba ni sawa na ubobeaji wa mcheza kamari. Ile starehe na pumbazo la akili ambalo mtumiaji wa madawa ya kulevya au mlevi sugu analihisi, ndilo hilo hilo ambalo mtu aliye katika mapenzi anahisi.

Penzi (Kwa maana ya mtu kumpenda mwingine wa jinsia tofauti kwa penzi la kawaida au hadi kwa kufanya mapenzi) na usugu wa madawa au pombe, vyote huwa vinauchochea mwili wa anayehusika kutoa homoni inayofahamika kama dopamine. Homoni hii ambayo ni kemikali katika ubongo huwa inaujaza mwili raha na ni kemikali hii hii ndiyo ambayo inahusika katika kuupa mwili tabia ya usugu katika mambo fulani kama ulevi.

Ni kitu gani kikubwa katika hili?

Ni kwamba kama ni hivyo, ina maana kuwa mtu kuwa kwenye kiwango kikubwa au cha juu cha kupenda, yaani kama tulivyozea kusema ‘kuwa hoi kwa penzi’, ni sawa na wakati ule mlevi sugu wa madawa akiwa ameshavuta au kunywa.

Mbaya zaidi ni pale penzi linapofikia hatua ya kuwa penzi la kukutana kimwili. Ni mbaya kwa sababu katika hatua hii homoni ya depomine inayotolewa inaweza kuizinga akili milele.

Kinachotokea ni kwamba kama homoni hiyo itajizinga kwenye akili, mhusika anakuwa sawa kabisa na mlevi sugu wa pombe au madawa ya kulevya, inakuwa ni vigumu sana kumtoa mtu kama huyo kwenye penzi na huyo fulani wake.

Bila shaka umeshawahi kuona au kusikia juu ya watu ambao wanaishi kwenye uhusiano mgumu sana na wapenzi wao, lakini bado wakawa wagumu wa kuondoka kwenye uhusiano huo. Kwa mawazo yetu wengi huwa tunadhani kung’ang’ania huku kunatokana na hali kama utegemezi, hasa kwa wanawake.

Baadhi yetu huwa tunaamini kwamba hali hiyo inaweza kuwa inasababishwa na dawa za asili au uchawi maarufu kama Limbwata, hasa pale mwanaume anapokuwa ameshikwa kwenye mapenzi na mpenzi wake au mkewe. Hii sio kweli.

Kuna wakati unakuta kwamba mwanamke ana uwezo wa kuendesha maisha yake na pengine yeye ndiye anayemsaidia mwanaume katika maisha, lakini pamoja na kuteswa au kuburuzwa na mwanaume huyo, bado atang’ang’ania kuishi naye. Kuna wakati tunaona kabisa kwamba, mwanaume anajua kwamba mwanamke anamfurusha kwenye uhusiano wao na anakiri, lakini bado anang’ang’ania kwenye uhusano huo na mwanamke huyo.

Itaendelea wiki ijayo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post