Love; Nitapungua kama kuna ajira

Love; Nitapungua kama kuna ajira

Charity James

Habari ya mjini kwa sasa kwa baadhi ya wanawake hasa maarufu ni namna wanavyopambana kutengeneza miili yao kwa upasuaji ili kuwa na mionekano ya tofauti.


Hilo lilikuwa likifanyika mataifa makubwa kama China na Uturuki lakini sasa mambo yamebadilika kwani wameletewa karibu zaidi hapa nchini.

Hii ni baada ya huduma hiyo kupatikana Tanzania katika Hospitali ya Taifa ya Mloganzila, kali ni kwamba wakati wengi wakifanya hivyo staa anayefanya vizuri kwenye tamthilia ya Juakali, Love Pande maarufu kama Love wa Juakali yeye amekiri kuupenda mwili wake na hajawahi kufikiria kuubadilisha.

Mwananchi limefanya mahojiano na mkali huyo wa kuigiza akifunguka mambo mengi ya kushangaza ikiwa ni pamoja na kuzungumzia kupunguza mwili wake kama kutakuwa na ajira sawa lakini kuoga kwake siyo ishu.





Kula, Kulala

Kula ni lazima, kuoga hiyari ni kauli ambayo imekuwa ikizungumzwa sana mitaani hii ni kutokana na wengi kupenda kula kuliko kuoga, lakini kwa upande wa Love humwambii kitu kuhusu chakula.

"Napenda kula, lakini kuna muda naweza kula mara moja kwa siku kutokana na kutingwa na kazi na nikiwa nyumbani sina kazi ya kufanya basi nakula zaidi ya mara tatu.

"Siyo kula tu mimi hata kwenye suala la kulala nipo vizuri ndiyo starehe yangu ya pili, baada ya kula ukitaka kunikwaza nisumbue wakati wa kulala sipendi usumbufu kabisa linapofika suala hilo," anasema.

Muigizaji huyu anasema pia anakerwa na suala la kupelekeshwa kwenye jambo lolote kwani anajitambua kuwa ni mtu mzima, nini anatakiwa kufanya na nini hapaswi kufanya, anapenda zaidi kuelekezwa na siyo kitu kingine.





Ni mali safi, single

Inaaminika kuoa au kuolewa ni suna, lakini siyo kila mwanadamu anapitia katika hatua hiyo kwani wapo ambao wanazeeka hadi kufa bila ya kuoa au kuolewa, Love amethibitisha hilo baada ya kuweka wazi kuwa yupo single na ni mali safi.

"Mimi ni mali safi, nipo single sina mtoto wala familia, nafurahia maisha yangu na kuhusiana na kuolewa hiyo ni mipango ya Mungu ikitokea itakuwa hivyo." anasema Love ambaye amezaliwa peke yake kwenye familia yao.

Chapati mchezo wa ngano

Kupika siyo kila mwanamke au mwanaume anaweza kuna wengine suala la kuingia jikoni ni changamoto, wao wanasubiri kuambiwa chakula kimeiva wakae na kula tu, hilo ni tofauti kwa upande wa Love wa Juakali ambaye amekiri kuwa licha ya kupenda kula hata jikoni yupo vizuri.

"Napenda kula kwa sababu hata kupika nipo vizuri, sisubiri kuandaliwa na mtu naingia mwenyewe jikoni, chakula ninachopenda kupika zaidi ni pilau.

"Lakini pia kila chakula naweza kupika isipokuwa chapati ambazo licha ya kufahamu kuzipika lakini ni mchezo ambao siupendi kwa sababu maandalizi yake ni magumu hakuna kazi ngumu kama kuchezea ngano."

Love anasema chapati za maji anapenda kuzipika kwa sababu hazina mchakato mkubwa kuziandaa ila za kusukuma hata akipata mgeni anapenda kuandaliwa chakula hicho atafanya lakini kwa manung'uniko.

Kununa unazeeka

Kila mwanadamu anakitu ambacho anakipenda na kimekuwa kikimpa furaha kuna ambao wanapenda kula, kulala kama ambavyo Love wa Juakali amekiri kuwa yeye anapenda kufurahi muda mwingi.

"Muda mwingi napenda kucheka sipendi kununa kwa sababu sitaki kuzeeka haraka ukinuna unajizeesha na mimi huko sitaki kufika kwa sasa." anasema.

2023 mwaka mbaya

Tumeuanza mwaka 2024 ndiyo kwanza tunaingia mwezi wa pili muigizaji huyu wa Jua Kali amesema mwaka ulioisha haukuwa mzuri kwake kwani alimpoteza mtu muhimu.

"2023 haukuwa mwaka mzuri kwangu nimepitia nyakati ngumu kwani nilimpoteza rafiki na mama yangu mzazi, siwezi kusema ulikuwa mbaya zaidi kuna kipindi nilipitia mambo mazuri lakini kitendo cha kuondokewa na mama ndiyo kiliharibu mwaka wote.

"Licha ya kumpoteza mama na kupunguza nguvu kazi yangu, namshukuru Mungu nimeanzisha safari nyingine ya maisha kwani nimemudu kuishi mwenyewe siyo tegemezi tena kama nilivyokuwa chini ya mama yangu." anasema.

Instagram imempa ajira

Mtandao wa kijamii Instagram umekuwa na faida na hasara kwa kila mtumiaji kwani kuna ambao unawaingizia kipato kutokana na kunufaika na matangazo kutokana na kuwa na wafuasi wengi, kwa upande wa Love yeye amekiri kupata ajira kupitia mtandao huo.

"Nafahamika zaidi kupitia tamthilia ya Juakali lakini huwezi kuamini nimeipata nafasi hiyo baada ya Lamata kunitafuta kupitia DM yangu ya Instagram na kunipa nafasi.

"Sijakutana naye kwenye gari au ofisini alinitafuta DM na kuniambia naweza kufanya kazi ya kuigiza huku akinihakikishia kuwa nitafanya vizuri na mimi sikutaka kuipoteza nafasi hiyo ambayo licha ya kuniingizia kipato nimetengeneza familia mpya." anasema.

Umaarufu free passport

Pamoja na mastaa wengi kuumizwa na umaarufu wao kutokana na kazi zao za kuigiza au kuimba kwa upande wa Love wa Juakali, imekuwa tofauti kwani anasema unampa njia rahisi ya kutatua shida zake.

"Umaarufu kwangu siyo shida bali ni njia ambayo inanirahisishia mambo mengi na najitengenezea ndugu wengi kupitia kazi zangu japo siyo wote watanipenda.

"Nakumbuka kuna kipindi nilipita Muhimbili kwa mambo yangu binafsi nikakutana na mashabiki ambao wanafuatilia Tamthilia ya Juakali wakawa wananifurahia lakini sikuwa kwenye mood nzuri wakanichukia bila sababu,

"Hivyo kuna changamoto zake na faida yake pia halafu mimi sitaki kuteseka na umaarufu bado naishi maisha yangu ya kawaida napanda daladala kama kawaida nafurahia kucheka na mashabiki wangu na kuishi maisha ya kawaida." anasema Love.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags