Kwa ukware wangu nikapigwa ndoa ya mkeka Ununio

Kwa ukware wangu nikapigwa ndoa ya mkeka Ununio

Nilimuona yule binti akipita na dada yake mke wa yule mzee mwenyeji wetu. Yule dada yake aliniangalia sana kisha akawa anatabasamu, sikuelewe ni kitu gani kinaendelea. 

Niliendelea kupigisha mziki na ilipofika mida ya saa sita usiku kakaja kabinti kamoja na kuniambia kwamba naitwa nimfuate.

Nilikafuata hadi upenuni mwa ile nyumba ya shughuli, nilipofika pale nilimkuta yule binti na aliniambie tuondoke. 

Nilikwenda kuwaaga wenzangu na kuondoka na yule binti, tulipofika akanipeleka chumbani kwake ambapo aliniandalia chakula nikala kisha akavua nguo na kutupia khanga.

Pamoja mwanga hafifu wa kandili iliyowashwa mle chumbani haikuninyima fursa ya kuona mwili mbichi ulionona wa yule binti ulionakshiwa na kalio lililopachikwa likamkaa vizuri kiasi cha kuendana na mwili wake...

Kiunoni alikuwa amejaza shanga zenye rangi karibu zote zikiwa zimemkaa kiunoni barabara.

Aliniacha nimekaa pale kitandani akaenda uwani kujiswafi.

Kitendo kile cha kunionyesha mwili wake na zile shanga kiliniacha nikiwa nimeshapandisha mizuka na Mapigo ya moyo yalikuwa yanaenda kasi na kusukuma damu kwa wingi kwenye kichwa cha chini nikajua Leo hakuna mswalie Mtume.

Aliporudi alijifukiza udi kisha akajikabidhi kwangu.

Nikiwa kama simba mwenye njaa nilimpulusa mpaka alfajiri swalaaa swalaaa ndiyo tukalala.

Asubuhi kulipopambazuka nilishtuliwa na mlango ukigongwa kwa nguvu. 

Nilishtuka sana na nilimuona yule binti akiwa hana wasiwasi. 

Alijizoazoa pale kitandani na kutupia khanga na kwenda kufungua mlango na kutoka nje na kufunga mlango kwa nje. 

Nilisikia watu wakiongea huko nje na mmoja wa watu hao alikuwa ni yule mzee mwenyeji wetu.

Baada ya muda yule binti alirudi akiwa amejitanda kanga kisha akaniambai nivae kuna wageni wanataka kuingia kunisalimia. 

Nilishtuka sana na nilivaa haraka haraka.

Baaada ya kuvaa yule binti alifungua mlango na mara nikamuona mwenyeji wetu akiingia na wazee wanne wenye Kanzu kuonyesha ni Maustaadhi kina mama watatu na mkeka na chetezo cha ubani.

Kwa akili yangu ya Wanzuki mie nikajua labda wanataka tu kusoma dua kwa ajili ya ile shughuli hivyo nikanyanyuka ili nitoke.

Nilizuiwa pale mlangoni na kuambiwa kuna kikao kidogo. Nilikaa na sikuwa na wasiwasi.

Yule mzee alianza kuwambia wale wazee wenzake aliofuatana nao……

“Wazee wenzangu mniwie radhi kwa kuwashtukiza kuja kukamilisha jambo hili la muunganiko wa watu wawili kati ya mtu mume na mtu mke, kama Kur'ani tukufu ilivyotuusia kwamba tusiikurubie zinaa, na hivyo basi huyu bwana hapa nimemfuma akizini na shemeji yangu na kwa mujibu wa dini yetu ya kiislamu mimi kama mlezi siwezi kuingia katika dhambi hivyo nimeona nihalalishe kabisa niwafungishe ndoa……”

Muda wote wakati yule mzee anazungumza mimi nilikuwa kama ninaota na nilikuwa siamini kile kinachotaka kunitokea. 

Nilianza kubabaika na kuwaza, nitampeleka wapi mimi huyu binti wakati mie kula kulala na bado ninasoma.

Mwili ulipigwa ganzi ghafla....

“Samani wazee mimi sijazini wala nini, nililetwa hapa na huyu mzee kwenye shughli ya kuwatoa mabinti zake na baada ya uchovu nilikuja kujipumzisha hapa kama nilivyoelekezwa na mke wa huyu mzee……….”

Nilijikakamua na kujitetea…

Yule mzee alinikata kalma na kuwaambia wale mashekhe kwamba ni kweli alinipangia nilale pale lakini chumba alichoniandalia ni cha nje na si cha ndani. 

Hicho chumba nilicholala ni cha shemeji yake ambaye ndiye niliyefumaniwa naye.

Wale masheikhe wakasema wasipotezewe muda na niliamriwa nikae kwenye mkeka nifungishwe ndoa niondoke na mke wangu.

“Wazee wangu naomba mnisamehe kwani mie bado mwanafunzi na nikakaa kwa kaka yangu na sina hata uwezo wa kujitegemea…..”

Nilijitetea ili kujinusuru na ndoa ile ya fedheha.

Yule dada yake na binti niliyefumaniwa naye akadakia……

“Si wewe ulomwaambia mdogo wangu kwamba una nyumba mbili Dar na daladala tatu, sasa habari ya kusoma na kwamba huna uwezo wa kuishi na mke inatoka wapi? Tena ulimuahidi utamuoa, sasa tatizo liko wapi, wewe ondoka naye utatuletea mahari yetu hata mwakani.” 

Kusikia hivyo, nikajua Nkondo Igwa. Jasho lilinitoka. 

Nilimsikia Mzee mmoja nje akisema kama sitaki kukaa kwenye mkeka kwa hiyari nikalishwe kwa bakora nikajua huyu anazungumzia Tokomile.

Kwa msiojua Tokomile ni ngoma ya Wazaramo ya kutandikana bakora Kwelikweli.  Kusikia habari ya bakora nilikaa kitako kwenye mkeka kwa hiyari yangu bila shurti...

Wakati wote wa kadhia hiyo nje kulijaa umati wa watu waliokesha kwenye ngoma na wale wenzangu niliokuja nao walikuwa hapo nje wananisubiri ili tuondoke.

Nikiwa bado nimeduwaa, ubani ulichomwa na ndoa ikafungwa, lakini muda wote mwili wangu ulikuwa umekufa ganzi na sikuelewa kinachoendelea kabisa kwani chaneli zikikata.

Baada ya dua nilisikia huko nje mdundiko ukipigwa na watu wakicheza kwa  furaha na nyimbo za vijembe zikitawala za kuozeshwa mke. Mwanaume lilinishuka shuu………

Nilitolewa nje nikiwa nimefunikwa kwa kanga na mke wangu huku nikisindikizwa na vigelegele. 

Yule mwenyeji wetu aliagiza pick up yetu isogezwe ili maharusi tupande na safari ya kurudi Dar ianze. 

Niliposikia hivyo nilipata fahamu, nilichomoka hapo mbio hata wale waliojaribu kunikimbiza waliambulia vumbi.

Hata sikumbuki nilifikaje barabarani maana kijiji chenyewe kipo mbali kidogo na barabara. 

Nilipofika barabarani nilibahatika kupata lori la mkaa nikapanda na kurudi Dar. 

Kufika nyumbani wala sikuelezea masaibu niliyokutana nayo huko Uzaramoni nilikusanya nguo zangu na kukimbilia Mbagala Kibondemaji kwa mjomba wangu. 

Pale nilikaa siku tatu baada ya kupata nauli nilirudi kijijini kujipanga upya….






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post

Latest Tags