Kila mwaka, watu duniani kote wanasherehekea kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa njia mbalimbali. Mojawapo ya desturi maarufu ni kuwasha mishumaa kwenye keki na kisha baadaye kuizima kwa kupuliza.
Hii ni mila inayovutia na kufurahisha watu wengi, lakini je, unajua chanzo chake?. Mila hii imetokana na tamaduni za Wagiriki na Warumi wa kale.
Kwa Wagiriki, mishumaa ilikuwa na umuhimu mkubwa katika sherehe na ibada. Walikuwa wakimsherehekea mungu wa mwezi 'Artemis', ambaye alihusishwa na mwanga wa mwezi, uzuri, urembo, na uzima.
Ili kumheshimu Artemis, Wagiriki waliandaa keki ndogo za mviringo, kisha juu yake wanaweka mishumaa, ilikuwa ishara ya mwanga wa mwezi. Kisha baada ya hapo walitoa shukrani zao na maombi na ndipo walipuliza na kuizima wakiamini moshi unaotoka kwenye mishumaa unafikisha maombi kwa mungu wao.
Hata hivyo kwa upande mwingine, Warumi wa kale pia walikuwa na desturi ya kuwasha mishumaa kwenye sherehe za kuzaliwa, hasa katika familia za kifalme.
Warumi walikuwa wakitumia mishumaa kama sehemu ya ibada, na walikuwa na imani kwamba mwanga wa mishumaa ungeweza kutoa nguvu na ulinzi kwa mtawala au mfalme anayesherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Hivyo, mila hiyo ilijenga misingi ya kuwasha mishumaa kama ishara ya kumheshimu na kuombea mafanikio mfalme.
Katika jamii za kisasa, kuwasha mishumaa kwenye keki kunaendelea kuwa sehemu muhimu ya sherehe za kuzaliwa. Ingawa maadhimisho haya yamekuwa na mabadiliko kadhaa, kama vile aina za keki na mishumaa zinazotumika.
Lakini wengi hufanya hivyo kwa imani ya kuwa anapopuliza mishumaa, anapaswa kuwa na ombi, na kutarajia kwamba ombi lake litajibiwa.
Leave a Reply