Mudi Msomali aliyekuwa akimsimamia marehemu mchekeshaji Frank Patrick 'Molingo' katika sanaa yake, amesema kijana huyo alikuwa na tatizo la kuishiwa damu baada ya kutokwa damu kwa saa tano mfululizo.
Mchekeshaji huyo maarufu alifariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya kuugua kwa muda.
"Alikuwa na tatizo la kuishiwa damu kwa muda wa miezi miwili. Mwezi wa tisa akawa ametoka kwenda kutafuta kazi, Oktoba 4,2024 akarudi akaniambia anaumwa malaria nikampatia dawa, alikuwa amevimba uso akatumia dawa uso ukawa umerudi vizuri.
"Siku mbili zikapita akaanza kutokwa na damu nyingi sana puani nikamkimbiza zahanati ya hapa jirani ikashindikana. Damu zikagoma kukata tukampeleka hospitali ya mkoa wakamshughulikia kuanzia saa sita damu zilikuja kukata saa kumi na moja," amesema.
Akizungumza na Mwananchi anasema baada ya hapo alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Geita ndipo akaruhusiwa Desemba 2,2024, akaenda nyumbani kwa baba yake mzazi huku akitokea nyumbani kwenda kuongezewa damu.
"Juzi akatoka kwa baba yake akaenda nyumbani kwa mama yake mzazi Chato, ambapo ndipo umauti ukamkuta huko.Tunategemea kumpumzisha leo Desemba 10,2024 katika kijiji cha Katoro,"amesema Mudi.
Akizungumzia namna alivyokutana na Molingo hadi kuanza kufanya naye kazi anasema kwa mara ya kwanza walikutana mnadani.
"Molingo nilikutana naye kwenye minada ya Ng'ombe alikuwa anafanya kazi za kupaka rangi Ng'ombe. Nilivyofika Geita nilimuona Molingo anazurura kwenye machinjio ya Geita nikamwambia twende tukaishi nyumbani. Akasema amekuja kufanya kazi nikampeleka kwa kaka yangu akawa anafanya kazi kama miaka miwili au mitatu ya kusimamia ndama.
"Alivyoacha kazi nilimwambia akae nyumbani yeye ni kama mdogo wangu nikawa nakaa naye nikamwambia asiishi kama mfanyakazi," amesema.
Leave a Reply