Julius: Vicheko vya wanawake vilifanya niape kutooa

Julius: Vicheko vya wanawake vilifanya niape kutooa

Mwigizaji Julias Charles anayefanya vizuri kwenye tamthilia ya Huba, amesema kutokana na urefu alionao anakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kwenye vyombo vya usafiri.

Julius ameiambia Mwananchi kuwa usafiri kwake ni ishu, kwani gari linalotosha urefu wake linauzwa kuanzia Sh400 hadi 500 milioni ambapo uwezo huo kwa sasa hana.

“Sijapata gari la saizi yangu hapa nchini ambalo naweza nikakaa kwa uhuru kama wengine, kupanda daladala ni ngumu, kiti kinachoweza kunitosha ni kiti cha kati kwenye siti za mwisho nakuwa naweza kunyosha miguu yangu.

“Zamani nilikuwa nikikuta gari limejaa nilikuwa sipandi,mimi ni mrefu hivyo siwezi kusimama wala kumnyanyua mtu aliyekaa ili nikae mimi, ila usafiri wa ndege una huduma tofauti kuna siti za watu wa aina yangu.”

Anasema kwa sasa huwa anakodisha gari binafsi ama anachukua bodaboda kwenda sehemu anapotakiwa kufanya majukumu yake, lakini nako hakai kwa kujiachia.

“Nikitaka kuingia ndani lazima nitainama mlangoni, kwa sababu bado sijajipata kujenga nyumba ambayo itakuwa ya ndoto zangu, kitanda ninacholalia ni futi 8 kwa sita natengeneza kwa oda maalumu. Viatu naagiza kutoka nje navaa namba 18 sawa namba 55 za viatu vya kawaida, ninachoshukuru nina marafiki nje ambao wananiletea, ila kwa mara ya mwisho kununua kwa pesa yangu ilikuwa Sh.200,000.

“Natumiwa viatu kutoka China, Canada, Marekani na marafiki zangu, Mungu anapokuumba tofauti anakupa na njia ya kufanya maisha yako yaende, nakumbuka zamani nilikuwa natembea bila viatu na sikumbuki kwa mara ya mwisho lini nilivaa kandambili zaidi ya sandozi ambazo pia naagiza kutoka China,"anasema

Ana miaka mitatu katika mapenzi

Anakumbuka akiwa na miaka 16 alikutana na wanawake watatu waliomzidi umri, baada ya kumuona wakaanza kucheka mmoja wao, akasema hata dunia iishe yote abakie Julias hawezi kukubali kuwa naye, maneno hayo yalimuumiza sana moyo wake.

“Kauli ile ilinifanya nijiulize maswali mengi sana, moyo wangu uliniuma kupita kiasi, nikajiapiza kwamba sitakaa nioe katika maisha yangu,ndio maana nimechelewa sana kuingia katika mahusiano.

"Tangu nimechekwa nikiwa na miaka 16 sikuwahi kuwa na mahusiano na nilianza nikiwa na miaka 27 na sasa nina miaka 30, mwanamke wa kwanza aliyenitoa uvulana wangu tulikuwa marafiki sana na alikuwa na watoto, kuna siku aliniambia ana hisia na mimi ikachukua siku mbili kumaliza kila kitu,"anasema

Anasema baada ya hapo alipata safari ya kwenda Marekani ambako alikaa zaidi miezi sita, ndipo mwanamke yule akaingia kwenye mahusiano mapya. Huku kwa upande wa Julius naye akaingia kwenye mahusiano mengine.

“Zamani niliwahi kujifungia ndani miezi mitatu, mimi ni mkimya vile jamii ilivyokuwa inaniona kama siyo mtu wa kawaida nilikuwa naumia moyoni, ila mama alikuwa ananiambia tembea mtaani lazima watu watakuzoea, nikaja kupata ujasiri baada ya kuanza kidato cha kwanza shule ya bweni, tulikuwa wanafunzi zaidi ya 1000 nilipendwa na kila mtu.

“Nikawa nacheza mpira wa kikapu, hilo pia likachangia kupata mashabiki ambao wananipenda na kunipa moyo, lakini bado haikuondoa kuwachukia wanawake, katika familia yetu mimi ni mtoto wa pili kati ya saba, mrefu nipo pekee yangu wenzangu wote wa kawaida hata baba na mama wapo kawaida tu,”






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags