Jukwaa la pamoja la Wakurugenzi wanawake wa asasi za kiraia lazinduliwa

Jukwaa la pamoja la Wakurugenzi wanawake wa asasi za kiraia lazinduliwa

Katika kusherekea siku ya wanawake duniani,Wakurugenzi mbalimbali wanawake wameungana nchini kuzindua Jukwaa la pamoja la Wakurugenzi wanawake wa Asasi za Kiraia  ikiwa na lengo la kuwa na sauti za pamoja katika kusimamia haki za wanawake , haki binadamu na Kijamii.

Pia Wanawake hao wameweza kuzindua kitabu maalum cha Wanawake 15  wenye historia kubwa nchini ambapo kati ya  wanawake hao wapo waliokuwa wakurugenzi katika taasisi mbalimbali walioleta mapinduzi ya wanawake katika nyanja mbalimbali za kijinsia, kisheria na kijamii katika kuwakomboa wanawake.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa Uzinduzi wa Kitabu hicho na Jukwaa hilo la wanawake, Mkurugenzi  wa Shirika la Wanawake  katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Anna Kulaya amesema katika kusherekea siku ya wanawake duniani wameona vema kuwakumbuka wanawake wa nguvu ambao ni Malkia na wamefanya mambo mazuri  nchini.

Amewataja miongoni mwa wanawake hao ni pamoja na  Maria Shaba,Dkt.Helen Kijo Bisimba,Dkt.Judith Odunga,Mama Nakazael Tenga,Dkt.Annanilea Nkya,Mary Rusimbi, Dkt.Marjurie Mbilinyi,Gemma Akilimari,Dkt.Gertude Mongela,Edda Sanga na Justa Mwaituka.

Wengine ni Leila Sheikh,Dkt.Monica Mhoga,Christina Ruhinda na Gelina Fuko kitabu hicho kimeweza kuwatambua na kuandika historia zao katika harakati za kumkomboa mwanamke. 

Kulaya amesema wameona wawaheshimu na kuwaenzi kwa kuandika taarifa zao katika kitabu ambacho kitabaki kuwa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo kwa namna walivyofanya  harakati za kuwakomboa  wanawake.

“Kitabu hiki kitakuwa Chachu kwa wasichana wetu wa kike ambao watakuwa viongozi  kuja kusoma njia ambazo wanawake hao wameweza kupitia,Changamoto walizopitia nchini Tanzania,Afrika na Duniani,”amesema

Aidha Akizungumzia uzinduzi wa Jukwaa hilo la wanawake Wakurugenzi,Kulaya amesema malengo makubwa ya kuanzisha jukwaa hilo ni pamoja na kupashana habarj,kujifunza kwa viongozi waliopo,kuwa na sauti ya pamoja wanaposimamia haki za wanawake  na binadamu.

Amesema pia Jukwaa hilo linatathimini nguvu kubwa na mchango mkubwa inayofanywa na wanawake viongozi wa asasi za kiraia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo Cha Haki za Binadamu LHRDC.Anna Henga amesema kitabu hicho kilichoandikwa ni cha muhimu  kwa nchi za Afrika  kwa kuandika mambo mazuri yaliyofanywa na yanayofanywa na waafrika.

“Kuandika kitabu hiki ni jambo la msingi sana kwa kuwatia moyo  wasichana wadogo wanaokuja kuwa viongozi baadae kuona nao wanaweza katika mapambano hayo ya kumkomboa mtoto wa kike,”amesema na kuongeza

“Jambo hili linatutia moyo na sisi viongozi tuliopo katika taasisi mbalimbali kuona kazi zinazofanyika zinaonekana na kutambuliwa katika Jamii,”amesema






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags