Je, wajua mapenzi yao yalianzia wapi

Je, wajua mapenzi yao yalianzia wapi

Mbali na sanaa, kitu kingine msanii anachouza kwa hadhira yake ni mtindo wake wa maisha, na hapa ndipo mashabiki wengi hupenda kuliko hata zile kazi za msanii husika kitu ambacho hupelekea baadhi kudanganya kuhusu uhalisia wa maisha yao.

Ni wazi wasanii kwa wasanii kuwa na uhusiano ni jambo lenye mshawasha kwa mashabiki, waliofanya hivyo mara nyingi wanakuwa na nguvu ya ushawishi katika soko ulinganisha na wale wanaofanya siri maisha yao ya mapenzi.

Hapa Bongo wapo wasanii wa muziki na filamu ambao mahusiano yao yaliteka mazungumzo au bado yanafanya hivyo kwa mashabiki wao. Lakini wajua ni wapi walipokutana kwa mara ya kwanza na kuianza safari hiyo? karibu tukujuze.

Aunty Ezekiel & Kusah - Instagram

Mwimbaji wa Bongo Fleva, Kusah alipokea ujumbe (DM) Instagram kutoka kwa muigizaji Aunty Ezekiel aliyekuwa anampongeza kwa muziki wake mzuri, basi wakaendelea kuwasiliana katika mtandao huo hadi walipojikuta wapo katika uhusiano na tayari wana mtoto.

Wawili hao wamekuwa wakishirikiana katika kazi zao za sanaa, mfano Aunty Ezekiel ndiye amecheza kama mke katika video ya Kusah, I Wish (2021) ambayo imetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 18 YouTube ukiwa ni wimbo wake kwanza kufikia rekodi hiyo.

Navy Kenzo - India
Ni miaka 16 sasa Nahreel na Aika wanaounda kundi la Navy Kenzo wapo pamoja, walikutana mwaka 2008 wakiwa masomoni nchini India, kitendo cha Watanzania wawili kukutana Ughaibuni kwa kiasi kilichochea mapenzi yao na sasa wana watoto wawili wa kiume.

Ujauzito wa mtoto wao wa kwanza, Gold aliyezaliwa Desemba 2017 ulipatikana walipoenda kufanya show nchini Israel na ndipo waliposhutia video ya wimbo wao ‘Morning’ kutoka katika albamu yao ya kwanza, AIM (Above Inna Minute) (2016).

Diamond & Wema - Facebook
Kwa mara ya kwanza Wema alimuona Diamond Bilicanas na hawakusalimiana, wakati huo Diamond alikuwa anavuma na nyimbo zake ‘Kamwambie’ na ‘Mbagala’, baada ya muda Wema aliyekuwa anatoka na Chalz Baba, akaenda Marekani kwa dada yake.

Alipofika Marekani dada yake akamuuliza kama ana namba ya Diamond maana nyimbo zake zinafanya vizuri huko, akawa hana ila akamtafuta Facebook na kumueleza hilo, basi wakaendelea kuchati hadi kupendana na aliporudia Bongo wakaanza kuishi pamoja.

Vanessa Mdee & Rotimi - Marekani
Wawili hawa waliochumbiana Desemba 2020, kwa mara ya kwanza walikutana Julai 2019 kwenye tamasha la Essance Marekani, siku hiyo Vanessa alikuwa na mdogo wake Mimi Mars, alipobadishana namba za simu na Rotimi ndio ukawa mwanzo wa uhusiano wao.

Kwa mujibu wa Vanessa, ilimchukua siku mbili pekee kutambua kuwa Rotimi ni mwanaume atakayekuwa naye milele, hiyo ni baada ya kwenda mapumziko pamoja ambapo walizima simu kwa kipindi chote na kujadili mipango yao na sasa wana watoto wawili.

Nandy & Billnass - Fiesta
Walikuwa wanasoma pamoja CBE ila hawakuwa na ukaribu, sasa wote walipokuja kufanya vizuri kimuziki, mwaka 2016 wakaitwa katika tamasha la Fiesta, wakaenda kutumbuiza Sumbawaga ila wakaenda kulala Mbeya na huko ndipo mambo yalipoanzia.

Hata hivyo, uhusiano wao waliendelea kuufanya siri mbele ya mitandao na vyombo vya habari hadi mwaka 2020 walipochumbiana na kuja kufunga ndoa Julai 2022, na sasa wana mtoto mmoja huku wakishirikiana katika nyimbo tano zilitoka kati ya 2019 hadi 2024.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags