Je wajua bibi harusi anatakiwa kujiandaa siku 30 kabla

Je Wajua Bibi Harusi Anatakiwa Kujiandaa Siku 30 Kabla

Bibi harusi ndiye kinara katika siku muhimu ya sherehe yake ya harusi, hivyo anapaswa kupendeza kwani macho ya watu wengi watakaohudhuria katika sherehe hiyo yatakuwa kwake.

Yeye ndiye malkia wa siku hiyo adhimu katika maisha hivyo anatakiwa kuhakikisha hafanyi makosa katika suala zima la muonekano wake kuanzia nywele, make-up, ngozi, kucha na hata mavazi.

Na muonekano huo wa kuvutia hauji kwa bahati mbaya, unahitaji maandalizi ya siku kadhaa kabla ya kufikia siku hiyo ya harusi pamoja na kupata ushauri wa nini cha kufanya ili kuweza kupata muonekano mzuri ambao utawafanya watu wakuendelea kukusifia hata baada ya shughuli kuisha.


Kauli hiyo inaungwa mkono na Precious Simba, mtaalamu wa masuala ya urembo wa wanawake na mmiliki wa saluni ya Goddess Glam Beauty iliyopo Kinondoni Biafra, mtaa wa Pazi, inayojihusisha na masuala  ya urembo ikiwemo make-up, huduma mbalimbali za nywele na kucha, singo pamoja na maandalizi muhimu kwa bibi harusi.

Precious alisema kuwa kwanza siku 30 kabla ya sherehe, bibi harusi anapaswa kuwa amekwishafanya maamuzi ya ni saluni gani atakayopambwa na ni vyema iwe na wataalamu wa masuala ya urembo ili aweze kupata ushauri ni kwa namna gani atatunza ngozi, uso, nywele pamoja na kucha ili inapofika siku yake hiyo muhimu aweze kupata muonekano mzuri na kuvutia ambao utawaacha watu kinywa wazi.

“Bibi harusi anapaswa kulichukuliwa kwa umakini na uzito mkubwa swala la muonekano kwani ndiye mtu ambaye kila mtu anayefika katika shughuli anatamani kuona namna alivyotokelezea na muonekano huo unapatikana kwa kufanya maandalizi mbalimbali siku 30 kabla ya harusi, “alisema.

Anasema kwa upande wa ngozi haswa ya uso kwa siku hizo 30 kabla ya harusi anatakiwa kuwa na mazoea ya kufanya singo kwa mara tatu hadi nne ndani ya siku hizo 30 zinazoshauriwa kitaalamu.


Anaongeza kuwa singo ya kutumia inaweza kuwa ya asili au ya viwandani cha msingi ni kuhakikisha anapata ushauri wa kitaalamu kwanza ili aweze kutumia ile inayoendana na aina ya ngozi yake.

“Hii husaidia kupunguza mafuta katika ngozi, kuondoa chunusi na uchafu uliopo katika ngozi, kufanya iwe ya kuvutia na ang’avu pamoja na ngozi iliyoharibika kuondoka kwani ngozi ya mwanadamu hubadili ngozi yake kila baada ya siku 21,” alisema.

Pia aliwashauri mabibi harusi wanaotumia vipodozi vya kuchubua ngozi siku chache kabla ya kuingia kwenye harusi kuacha kufanya hivyo kwani kunaweza kufanya ngozi zao kuharibika.

“Baadhi ya mabibi harusi hujichubua ili waonekane weupe jambo linaloweza kuathiri Ngozi, ni vyema katika kipindi hicho kuitunza ngozi yako ni vizuri ili iwe nzuri, laini yenye afya na kuvutia mbele ya macho ya watu. Si vizuri kuingia katika ukumbi wa harusi halafu wageni waalikwa waanze kunyoosheana vidole kwamba si alikua mweusi huyu mbona kawa mweupe ghafla,”alisema.

Katika upande wa nywele, Precious alisema ni vyema bibi harusi kufanya maamuzi mapema juu ya ni nywele aina gani mfano nywele halisia au utumiaji wa mawigi.

Kwa wanaopendelea kutumia mawigi Precious anashauri wahakikishe wanatumia mawigi ambayo ni ‘original’ ili waweze kupata muonekano wa kuvutia kwani huwa yanapasika vizuri hivyo kuwa rahisi kumtengeneza bibi harusi mitindo mbalimbali.

Kwa wanaopendelea kutumia nywele halisia anashauri wahakikishe wanazitunza nywele zake vizuri kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kutumia bidhaa zinazoendana na nywele zako ikiwemo mafuta, shampoo na steaming, kuziosha pamoja na kuziacha zipumzike na mambo yanayoweza kupelekea nywele hizo kuharibika ili ikifika nywele zako ziwe na afya nzuri.

Kwa upande wa kucha anashauri kuwa ni muhimu kuzitunza kucha zake vizuri na inapofika siku ya harusi kwa wale wanaopendelea kupaka rangi wanashauriwa kupaka rangi zisizowaka sana kwani bibi harusi hatakiwi kuwa na mambo mengi haswa linapokuja suala la kucha.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post