Je Unaichunguza familia kabla ya kuchagua mwenza

Je Unaichunguza familia kabla ya kuchagua mwenza

Mila na desturi zetu zilikuwa zinahimiza kwamba, kabla ya vijana hawajaamua kuwa pamoja, ilikuwa ni lazima wazazi kujua kuhusu familia ya mwingine. Hata kama haina maana kuwa mmoja akijua mwenzake familia yake ina laana ya kupiga, aachane naye, hapana. Kwa kujua, anaweza kuwa kwenye nafasi ya kujua namna anavyoweza kumsaidia mwenzake kuchana na tabia hiyo au kujisaidia kuepuka vipigo kwa maana ya kuchukua tahadhari.

Wazazi wetu zamani hawakuwa wajinga walipokuwa wanachunguza familia ya mahali binti yao anapotaka kuolewa au kijana wao anapotaka kuoa. Walikuwa hawajui somo linaloitwa saikolojia, lakini walikuwa wakijua kwamba, tabia mbaya au nzuri zinaweza kuwa zinatembea katika familia.

Wataalamu wamethibitiaha hivi sasa kwamba, familia ambazo wazazi ni walevi kwa mfano, au ni wavuta bangi, ni rahisi sana kwao kuwarithisha watoto wao kuliko watu wanavyofikiria. Jambo ambalo halipendezi katika matokeo ya tafiti nyingi kuhusu hali hii ni ule ukweli kwamba, baadhi ya tabia mbaya hujitokeza wakati watoto wa familia yenye ‘laana’ fulani wakiwa barubaru, (miaka 13 hadi 19) au huweza kujitokeza ukubwani. Kwa nini nimesema halipendezi? Subiri nitakwambia.

Tabia huwa inaambukiza na inaambukiza kwa njia ambayo ni sawa na mtu kupita mahali ambapo pana rangi mbichi ambayo humuingia kwenye mwili au nguo,halafu tayari anakuwa na rangi hiyo bila hiyari yake. Hakutaka kujipaka rangi, lakini rangi iko pale na ameigusa, hawezi kuepuka kujipaka. Kwa hiyo mzazi au wazazi wanapokuwa na tabia mbaya, watoto hudaka tabia hizo kwa njia hiyo.

Katika jarida la Abnormal Child Psychology la hivi karibuni limebainisha kwamba, ni mara chache kukuta mtoto hajaathiriwa na tabia za wazazi wake ambazo hujitokeza sana katika familia. Kwa mfano kati a watoto watano wa wazazi walevi, anaweza kupona mtoto mmoja tu. Labda tu kama mzazi mmoja anapinga ulevi na ndiye mwenye nguvu kwa watoto. Awali wanaweza kuzichukia, lakini baadaye ukubwani wakazitumia kwa sababu ndizo njia pekee wanazozijua katika kukabiliana na matatizo  ya kimaisha.

Kwa nini nilisema pale awali kwamba, yale ni matokeo yasiyopendeza? Nadhani unakumbuka. Basi nilikuwa na maana hii:
Mwanamke: Hebu fikiria kwamba, umepata mchumba, handsome boy, ana fedha zake na amesoma madarasa ya kutosha. Anataka kuwa na uhusiano nawe, tena pengine uhusiano wa kudumu yaani kuoana. Je utaangalia tu uzuri, elimu na fedha zake au utakwenda mbali zaidi?

Mwanaume: hebu chukulia kwamba, umekutana na msichana, jicho-jicho, guu-guu, kalio-kalio na anajua mahaba, halafu amekubali kuwa rafiki yako, nawe umebabaika nanataka haraka sana mitwe mke na mume. Je najitendea haki kuishia kwenye guu-guu tu au unapaswa kwenda mbali zaidi?

Familia anayotoka mtu ina mchango mkubwa sana kuhusiana na tabia za mtu huyo. Anaweza asioneshe tabia hizo wazi na hata akizionesha kwa kiasi fulani tunaweza kushindwa kujua kwamba, ni tabia ambazo hawezi kujiepusha nazo, kwani ni za familia kwa sababu hatujui familia yake.

Kwa hiyo badala ya kuishia kwenye guu-guu au jicho-jicho na kuishia kwenye u-handsome, elimu au fedha, inabidi twende mbali zaidi. Kama kweli tunataka kuwa na familia bora na imara, inabidi twende mbali zaidi tunaposema tumempenda fulani.

Usipoenda mbali utampata handsome ambaye amerithi kupiga mke, amerithi ulevi, amerithi ghubu na mengine yanayofanana na hayo. Kwa  kuwa umempenda utakaa kwenye ndoa ya mateso na vipigo, ambapo watoto wenu nao watakuwa ni wa kupiga wake au kupigwa na waume zao na kuwavumilia. Hapo mtakuwa mnaendeleza familia ya laana.

Ni jambo la kusikitisha kukuta binti anajua vizuri familia ya mpenzi wake kwamba, baba wa mpenzi wake huwa anampiga sana mkewe, mbaya zaidi, inawezekanameshaanza kuona dalili za mkono mwepesi wa kupiga kwa huyu mpenzi wake. Lakini bado anang’ang’ania kuingia kwenye ndoa na mpenzi huyu mkorofi. Huu ni ujinga….

Ukweli ni kwamba ukienda kuoa kwa wapewa na watoa talaka, jiandae kwa kutoa au kupewa talaka. Huna haja ya kujidanganya kwama, utaweza kubadili tabia hii kirahisi kama unayeoana naye anayo kutoka katika familia yake…






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags