Hii hapa historia ya Boxing Day duniani

Hii hapa historia ya Boxing Day duniani

Kila ifikapo Disemba 26, dunia husherehekea sikukuu ya ‘boxing day’ ambayo mara nyingi huenda sambamba na kutoa na kupokea zawadi.

Na huwa inafanyika siku ya pili baada ya kusherehekea sikukuu ya Krismasi, kwa mujibu wa mtandao wa ‘The Sydney Morning Gerlad’ wa nchini Australia umeripoti kuwa zaidi ya Sh22.7 trilioni zinatarajiwa kutumika kununulia zawadi duniani kwa mwaka 2023.

Matumizi hayo yatakuwa ni ongezeko la asilimia 1.6 ya matumizi yaliyofanyika katika kipindi kama hicho mwaka 2022. Utafiti huo unaonyesha katika bidhaa zitakazoongoza kununuliwa zaidi ni vifaa vya kazi, nguo, vyakula na mapambo.

 

Historia ya ‘boxing day’

Tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) inasema ‘Boxing Day’ ilianza kuitwa hivyo wakati Malkia Victoria wa Uingereza akiwa madarakani mwaka 1800, kutokana na utamaduni uliokuwapo wakati huo uliohusisha familia za kitajiri kutoa zawadi kwa familia za kimasikini.

“Kwa kuwa watumishi wa watu wa tabaka la juu walitakiwa kufanya kazi siku ya Krismasi, hivyo siku iliyofuata waajiri waliwapatia wafanyakazi masanduku yenye zawadi, fedha na mabaki ya Krismasi kama vile bonasi ya likizo,” imeandika tovuti hiyo katika moja ya makala yake iliyoelezea asili ya sikukuu ya boxing day.

Hata hivyo, tovuti ya www.history.com inaeleza nadharia nyingine kuhusu asili ya sikukuu hiyo ya kupeana zawadi, “Jina la ‘boxing day’ lilitokana na masanduku ya sadaka yaliyowekwa makanisani kwa ajili ya kukusanya michango kwa wale wanaohitaji, kisha Desemba 26 makasisi hutoa fedha hizo kwa masikini kwa heshima ya sikukuu ya Mtakatifu Stefano, shahidi Mkristo anayejulikana kwa matendo ya hisani,” imeeleza tovuti hiyo.

 

Wachumi waielezea

Mack Patrick, ambaye ni mchumi anasema sikukuu ya hiyo pamoja na nyingine za mwishoni mwa mwaka zinachochea ukuaji na ongezeko la biashara duniani na nchini pia.

“Katika kitu ambacho nchi za Ulaya kinanufaika nacho katika kujiimarisha kiuchumi ni sikukuu za mwishoni mwa mwaka, kwao huo ni muda wa manunuzi hasa na hii inasababisha mzunguko wa fedha kuongezeka,” amesema.

Alisema, “Kumbuka biashara zinapofanyika pia Serikali inapata kodi ambayo itatumika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.

Kuhusu boxing day, Patrick alisema bado Tanzania inashindwa kutumia vizuri sherehe hiyo katika upande wa biashara. “Bado hatuna tabia ya manunuzi katika kipindi hiki japokuwa ukienda baadhi ya maeneo kama vile Moshi, kule biashara inafanyika hasa na katika nyakati hizi watakuwa wanakusanya sana kodi,” amesema.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags