Headpiece kwa bi harusi inaongeza urembo kiasi gani

Headpiece kwa bi harusi inaongeza urembo kiasi gani

 Halooo!!! Moja kati ya siku ambazo ni special sana kwa mwanamke ni ile siku ambayo anapata nafasi au bahati ya kufunga ndoa kwenye maisha yake na hua ni siku kubwa sana kwake ambayo mara nyingi hubaki kwenye kumbukumbu za maisha yake.

Je umeshawahi kufikiria siku hiyo unatamani utoke na muonekano gani? Bila shaka hili li[ po kwenye vichwa vya wadada wengi ambao ikifika siku ya kufikia hatua hii basi lazima kila mmoja apambane ajue siku hiyo anatokaje.

Nikwambie tu kuwa   Kila bibi harusi ndiye kinara wa harusi yake hivyo katika siku hiyo muhimu kwake anapaswa kuhakikisha anapendeza kwani macho ya watu wengi watakaohudhuria katika sherehe hiyo yatakuwa kwake.

Nikukumbushe tu kuwa ili  muonekano wa bi harusi uwe ni wenye kuvutia pamoja na kuzingatia gauni bila kusahau  viatu  ni muhimu kuwa makini katika mtindo wa nywele pamoja na mapambo yake kwani navyo vina nafasi kubwa katika kupendeza kwake.

Mapambo ya nywele kwa bi harusi huwa yanabadilika kadri siku zinavyozidi kwenda, hivyo wataalamu wa masuala ya urembo wa maharusi wanashauri kabla ya kupata ya kuchagua urembo ni vyema kuchunguza ni aina ipi inabamba kwa wakati huo ili aweze kuonekana wa kisasa.

Baada ya urembo wa nywele aina ya ‘Crown’ kutamba kwa muda mrefu, miaka ya hivi karibuni kumeingia aina mpya ambayo kwa jina maarufu unajulikana kama ‘headpiece’ na kwa sasa ndio habari ya mjini kwa mabibi harusi, Ukitaka kuthibitisha hilo angalia urembo unaovaliwa sana na mabibi harusi wa miaka ya hivi karibuni.

Kutokana na umaarufu wake kwa sasa, Mwananchi Scoop  ilidodosa taarifa kutoka kwa wataalamu wa masuala ya urembo wa nywele kwa mabibi harusi ili kujua mengi kuhusiana na urembo huo.

 Mtaalamu wa masuala ya urembo huo kutoka Crystal Wedding Accessories, Irene Shamge alisema ‘headpiece’ asili yake ni kutoka nchi za Ugiriki pamoja na Italia haswa katika mji wa Roman ambazo zilikuwa zikivaliwa na watawala kama ishara ya utukufu na uongozi.

“Aina hiyo ya urembo wa nywele haukuibuka tu siku za hivi karibuni, una historia yake kama nilivyobainisha watawala wenye historia kubwa kama Cleopatra waliwahi kuvaa, lakini kadri siku zinavyoenda wabunifu wamekuwa wakiboresha kwa kuweka ubunifu wa aina mbalimbali,” alisema.

Irene alisema zipo aina mbalimbali za urembo huo hivyo uchaguzi wake unategemea na mtindo wa nywele ambao ataubana bibi harusi katika siku yake hiyo adhimu.

“Headpiece zipo ndefu sana, fupi, zilizotengenezwa kwa ajili ya mbele, pembeni au nyuma ya kichwa cha bibi harusi kwa rangi tofauti tofauti uchaguzi hutokana na aina ya mtindo anaoubana bibi harusi na rangi hutegemea aina ya nguo,”alisema.

Aliongeza;” Mabibi harusi walionyoa nywele hawajaachwa nyuma nao zipo zilizotengenezwa kwa ajili yao ambazo wanaweza kuvaa na kupendeza kama wengine”.

Alisema pamoja na kuvaliwa sana katika harusi lakini pia inaweza kuvaliwa katika shughuli mbalimbali ikiwemo Kitchen Party, Sendoff, Bridal Shower, Baby Shower na nyinginezo lakini kwa yule mlengwa wa kike wa shughuli husika.

Pia alisema kuwa bibi harusi anapovaa urembo huo kwanza unaongeza muonekano wake kuwa ni wa kuvutia zaidi na kumfanya aonekane wa kisasa.

“Ni muhimu kwa bi harusi kuzingatia vitu atakavyovivaa katika shughuli yake kuanzia gauni, viatu nywele na urembo wake vinakuwa vinaendana na wakati huo, kwani mambo ya mitindo hubadilika kila kukicha,”alisema.

Alisema pia aina hii ya urembo ipo ya kila aina kulingana na size na hepu ya kichwa cha muhusika hivyo inampa uhuru mkubwa bi harusi ya kuchagua na kupendeza.

Nae Mwanaisha Mtawa kutoka   Isha Beauty Saloon anatueleza kuwa si lazima uvae wigi ndio uweze kutumia vibanio hivyo unaweza kutumia nywele zako za asili na ukapendeza.

“Cha msingi ni kuhakikisha miezi kadhaa kabla ya siku ya harusi uanze kufuata ratiba ya utunzaji wa nywele zako vizuri kwa uanze kuzijali nywele zako, kula vizuri, kuziosha, kumia mafuta mazuri ya nywele na kuzipumzisha kwa muda na vitu vinavyoweza kupelekea kuharibika  ili siku ya harusi ikifika nywele zako ziwe na afya nzuri,”alisema.

Ebwanaa eeeh!! Mengi yamewekwa bayana hapo mtu wangu Urembo na umaridadi unanafsai kubwa sana kwenye siku ya special hakikisha unatoka ile mbayaaa! Tukutane wiki ijayoo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post

Latest Tags