Haya Ndio Mafanikio Album Ya Dizasta Ndani Ya Mwaka Mmoja

Haya Ndio Mafanikio Album Ya Dizasta Ndani Ya Mwaka Mmoja

Albamu ya A Father Figure kutoka kwa mkali wa Hip Hop, Dizasta Vina iliyotoka Januari 6, 2024 ikiwa imeshiba ngoma kama Theluji, Nobody is safe 5, Hatia VI, Not A Hero, Chupa Moja Ya Ziada, Karibu Duniani, Wachezaji Wa Tmu, Top Shelf, Fanani, Mbuzi, Achia Jala na zingine nyingi, imetimiza mwaka mmoja tangu kutoka kwake.

Muundo wa mashairi aliyotumia kwenye albamu hiyo unajumuisha usimulizi wa matukio mbalimbali kupitia ngoma kama Achia Jala, Not A Hero na Wachezaji Wa timu. Hadithi za maisha halisi ya jamii anayotokea yapo katika ngoma kama Theluji. Pia tungo zake zinasifika kwa kuelimisha na kugusa masuala ya kijamii ikiwemo malezi, usimuliaji wake upo katika ngoma kama Karibu Duniani. Hajayasahau maisha ya siasa, umasikini kwani ameyasimulia kwenye ngoma kama Get Better.
Masuala ya dini yapatikana katika ngoma kama Hatia VI na masuala mengine yaliyopo ndani ya ulimwengu mzima kwa ujumla.

Albamu hiyo imeandaliwa chini ya watayarishaji Jacob Mahuwi, Ringlebeat, Slimsal, na wengineo wakishirikiana kuziandaa ngoma 21.

Mwanachi imefanya mahojiano na Jacob Mahuwi ambaye alikuwa mtayarishaji mkuu wa albamu hiyo na amezungumzia kwa upande wake hii ni miongoni mwa albamu kubwa kuwahi kutokea kwenye kiwanda cha muziki wa Hip Hop kwa sababu ya maudhui yanayopatikana ndani yake.

"Mimi ninaipa asilimia 90 kwa sababu ukiangalia maudhui ambayo yapo kwenye hiyo albamu jamaa kafanya kazi kubwa sana," amesema Jacob.

Jacob ameongeza kuwa mara nyingi nyimbo ambazo Dizasta amekuwa akizitayarisha zimekuwa zikimpa ukakasi kutokana na maudhui yanayopatikana humo, ametolea mfano wimbo wa Hatia VI uliyopo kwenye albamu hiyo ya A Father Figure.

"Mara nyingi jamaa mawazo yake inabidi ukae ufikirie sana maana 'idea' anazoandika anapenda mtu afikirie zaidi aje na majibu ameelewa nini, hapendi akutafsirie moja kwa moja ndio maana ana wasikilizaji wake wanakuja na maoni tofauti tofauti kwa kile walichokielewa," amesema Jacob.

Hata hivyo, kwa upande wake mtayarishaji Ringlebeat ameelezea sababu ya albamu hiyo kutoachiwa kwenye majukwaa ya kuuzia muziki (Digital Platform) na badala yake kuuzwa kwa njia ya E-mail na WhatsApp akielezea walipima na kuona njia wanayotakiwa kutumia ni ya kuuza kupitia mfumo huo kutokana na soko la muziki wa Hip Hop lilivyo.

"Kila mtu ana namna yake tofauti ya kufanya vitu, sasa ukiangalia kwenye muziki wa Hip Hop mfano anaofanya Dizasta ukiwa kwenye mfumo wa Media ni ngumu kupata mashabiki wa kweli, lakini pia sisi tunafanya hii kitu ili tuendeshe maisha, kwa hiyo tukagundua kuna upande watu wengi wameusahau ambao hutengeneza mashabiki waaminifu sana," amesema Ringlebeat.

Mashabiki wa Hip Hop wanaitaja A Father Figure kuwa miongoni mwa albamu bora, sio tu kwa mwaka 2024 bali mashabiki wanaihusudu mpaka kuitaja kuwa albamu bora ya Hip Hop kwa muda wote Bongo, japo haijasambaa sana kwa sababu hakuamua kuiweka kwenye Digital Platform na badala yake anaiuza kupitia WhatsApp na E-mail shilingi 10,000 kwa kila nakala moja.

Jambo hilo limepelekea Mwananchi imtafute Dizasta Vinna kutaka kujua kwanini mfumo wa uuzaji na usambaji wa Albamu ya A Father Figure ni wa tofauti.

"Kuna mahusiano makubwa sana kati ya aina ya mashabiki wa msanii na mifumo ya usambazaji wa kazi zake. Mfumo huu licha ya kuwa na matobo machache ila ni fanisi sana kwa aina ya mashabiki niliokuwa nao inalingana na elimu yao ya tehama na teknolojia, utamaduni wao wa namna ya kupata huduma za burudani kama muziki na filamu na uchumi wao," amesema Dizasta Vinna.

Dizasta ameongeza kwa kusema albamu hiyo imekuwa na ufanisi kwenye namna ya kuitangaza, mauzo ya hii kazi ni taswira ya ufanisi huo.

A Father Figure ni albamu ya tatu kutoka kwa Dizasta Vinna ikitanguliwa na A Verteller na Jesusta. Mbali na hapo anatajwa kuwa ndiye msanii pekee Tanzania mwenye Squels zaidi ya moja ambazo ni Hatia, Comfession na Nobody Is Safe yote hayo ameyafanya kabla ya kufikisha miaka 30 bila kuwa na usimamizi, msaada na hata mkataba kwenye studio ya kurekodia.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags