Harmonize na rekodi zake mbili kubwa

Harmonize na rekodi zake mbili kubwa

Staa wa Bongofleva, Harmonize anaenda kuzindua albamu yake ya tano tangu ametoka kimuziki miaka tisa iliyopita, huku rekodi mbili kubwa zikiwa upande wake katika mradi huo alioutaja kuwa wa mwisho.

Mei 25 katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam ndipo albamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa, eneo ambalo pia albamu yake ya kwanza ilizinduliwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete mnamo Machi 2020.

Harmonize aliyetoka kimuziki na wimbo wake, Aiyola (2015) baada ya kusainiwa WCB Wasafi, tayari ametoa albamu nne ambazo ni Afro East (2020), High School (2021), Made For Us (2022) na Visit Bongo (2023).

Albamu ya tano inakuja akiwa pia ametoa na Extended Playlist (EP) moja, Afro Bongo (2019) yenye nyimbo nne alizoshirikiana na Diamond Platnumz, Yemi Alade, Mr. Eazi na Burna Boy.

Je, ni kwa namna gani albamu hii ya tano inaenda kuweka rekodi kwa Harmonize na tasnia nzima ya muziki nchini?, hizi ni rekodi mbili kubwa zinazoenda kuwekwa na albamu hiyo itakayotoka chini ya Konde Music Worldwide.

Mosi; Harmonize atakuwa msanii wa pili wa Bongo Fleva kutoa albamu kila mwaka kwa miaka mitano mfululizo akiwa amefanya hivyo kuanzia 2020 hadi 2024, huku albamu zake nne pekee zikiwa na jumla ya nyimbo 70.

Tangu Bongo Fleva inaanza kushika kasi miaka ya 1990 chini ya kina Saleh Jabir hadi ujio na mapinduzi ya Hard Blasters Crew (HBC) chini ya Professor Ludigo, ni wasanii wawili tu waliofanya hivyo, Sugu na Harmonize.

Rekodi zinaonyesha Sugu alitoa albamu kwa miaka mitano mfululizo kuanzia 1998 hadi 2002, albamu hizo ni Niite Mr II (1998), Nje ya Bongo (1999), Millennium (2000), Muziki na Maisha (2001) na Itikadi (2002).

Ikumbukwe Rayvanny amejaribu kufanya kitu kama hicho ila kwa upande wa EP ambapo kwa miaka mitatu mfululizo aliachia EP nne ambazo ni; Flowers (2020), New Chui (2021), Flowers II (2022) na Unplugged Session (2022).

Kwa Afrika mwanamuziki ambaye ametoa albamu mfululizo miaka ya hivi karibuni ni Burna Boy wa Nigeria, akiwa ametoa albamu saba, zilizofuata ni Outside (2018), African Giant (2019), Twice As Tal (2020), Love Damini (2022) na I Told Them... (2023).

Pili; Harmonize anapanda hadi tano bora ya wasanii wa Bongofleva waliotoa albamu nyingi kwa muda wote akiungana na Sugu (10), Lady Jaydee (8), Nikki Mbishi (6), Soggy Doggy (5), Juma Nature (5) na Professor Jay (4).

Ukitazama orodha ya wasanii hao wa Bongo Fleva wenye albamu nyingi, wengi wameanza muziki katikati mwa miaka 1990 hadi mwanzoni mwa 2000, isipokuwa kwa Harmonize na Nikki Mbishi ambaye tangu mwaka 2011 ametoa albamu sita.

Hadi sasa Nikki Mbishi ametoa albamu kama; Sauti ya Jogoo (2011), Malcom XI (2013), Ufunuo wa Unju Bin Unuq (2015), Sam Magoli (2018), Welcome to Gamboshi (2022) na Katiba Mpya (2023), huku akitoa Mixtape moja, K.I.G.U (Kisirani Ghubu cha Unju).

Utakumbuka Lady Jaydee ndiye msanii wa kike mwenye albamu nyingi kutoka kwenye Bongo Fleva akiwa ametoa nane zake binafsi na moja ya ushirikiano, Love Sentence (2023) akiwa na Rama Dee aliyeshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2013 kama Msanii Bora wa RnB.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags