Fahamu zaidi kuhusu ugonjwa wa saratani ya koo (part 2)

Fahamu zaidi kuhusu ugonjwa wa saratani ya koo (part 2)

Na Elizabeth Malaba

Ooooiiih! Niaje niaje watu wangu wa nguvu, kama kawaida afya ndo jambo la muhimu katika maisha haya, sasa tunaendelea pale tulipo ishia katika suala zima la saratani ya koo (canser ya koo).

Wiki iliyopita tulizungumzia jambo hili hili na tuliishia katika vipimo ambavyo anatakiwa kuvifanya mgonjwa ambae saratani yake imesambaa sana, na leo tunaendelea hapa ungana nasi mwanzo mpaka mwisho…

Hatua (staging) za ugonjwa wa saratani ya koo

Wakati mwingine madaktari hulazimika kufanya upasuaji ili kuweza kufanya staging kwa uhakika zaidi.Kwa mujibu wa staging, kuna hatua tano za saratani ya koo:

Hatua ya 0:

Hatua hii huitwa carcinoma in situ ambapo seli za saratani hupatikana tu kwenye utando wa juu wa koo.

Hatua ya I: Saratani husambaa kutoka utando wa juu mpaka kwenye tando nyingine za koo.

Hatua ya II: ina tabia mojawapo kati ya hizi zifuatazo:Saratani husambaa kutoka kwenye utando wa juu wa ukuta wa koo mpaka kwenye utando wa chini yake yaani submucosa na kisha kuenea kwenye tezi za karibu, AU Saratani husambaa na kushambulia utando wa misuli wa koo (muscle layer) na baadhi ya seli nyingine za saratani hufika kwenye tezi za jirani, AU Saratani husambaa kutoka katika utando wa ndani mpaka kufikia utando wa nje kabisa (outer layer) wa koo.

Hatua ya III: ina tabia mojawapo kati ya hizi:Saratani husambaa kufikia kwenye utando wa nje kabisa wa koo na kisha kusambaa hadi kwenye tezi za jirani, AU Saratani husambaa na kushambulia viungo vya karibu na koo kama vile njia ya hewa. Aidha seli za saratani huwa zimesambaa mpaka kwenye tezi za jirani.

Hatua ya IV: Seli za saratani husambaa na kuathiri viungo vingine vilivyo mbali na koo kama vile mapafu, ini na mifupa.Matibabu ya Saratani ya Koo

Matibabu ya saratani ya koo

Uchaguzi wa aina gani ya tiba itumike hutegemea sana eneo lililoathiriwa na saratani, iwapo saratani imeshambulia viungo vilivyo karibu na koo, iwapo saratani imesambaa mpaka kufikia kwenye tezi au viungo vingine vya mwili, na hali ya mgonjwa kwa ujumla.

Kutokana na hayo, saratani ya koo yaweza kutibiwa kwa kufanya upasuaji, kutumia mionzi, kutumia kemikali maalum, au mchanganyiko wa yote matatu.

  • Upasuaji

Kuna aina kadhaa za upasuaji kwa ajili ya kutibu saratani ya koo. Kila aina inategemea sehemu saratani ilipo. Daktari wa upasuaji anaweza kuondoa sehemu iliyoathiriwa au kuondoa koo lote. Hata hivyo kabla upasuaji haujafanyika, daktari hujadiliana na mgonjwa wake kumueleza ni aina gani ya upasuaji utakaofanyika, faida na hasara zake, na nini cha kutarajia kutokana na upasuaji huo.

  • Tiba ya Mionzi

Hii ni aina ya tiba inayotumia mionzi yenye nishati kubwa kuua seli zilizoathiriwa na saratani. Kwa kawaida tiba ya mionzi huathiri seli zilizo katika eneo linalotibiwa tu.

Aidha tiba ya mionzi inaweza pia kutumika kuua seli za saratani zilizobakia mara baada ya kufanyika kwa upasuaji au hata kabla ya upasuaji kufanyika.

Mara nyingi tiba ya mionzi hutolewa pamoja na tiba ya kemikali (chemotherapy). Tiba ya mionzi inaweza kutolewa kwa kutumia mashine ya mionzi iliyo nje ya mwili (external radiation therapy) au kwa kuingiza mashine ya mionzi ndani ya koo na kuua seli zenye saratani (internal radiation therapy au brachytherapy).

Tiba ya mionzi inaweza kusababisha, mbali na kuua seli zenye saratani, madhara kama vile maumivu kwenye koo

  • maumivu kama kiungulia au maumivu kwenye tumbo au utumbo.
  • Aidha wagonjwa wengine wanaweza kuharisha, kujihisi kichefuchefu, kuwa na ngozi kavu, ya moto na nyekundu, na kunyonyoka nywele sehemu iliyopigwa mionzi.

Tiba ya kemikali (Chemotherapy)

Aina hii ya tiba hutumia kemikali kuua seli zenye saratani. Kwa kawaida dawa hizi hutolewa kwa njia ya sindano kupitia kwenye mshipa wa damu wa vein. Aidha matibabu kwa njia hii hutolewa kwa awamu (cycles) huku kila awamu ikifuatiwa na kipindi cha mapumziko bila dawa. Madhara yanayoweza kusababishwa na njia hii ya matibabu hutegemea sana aina ya dawa husika. Baadhi ya madhara hayo ni:

  • Kupungua kwa kiwango cha chembe za damu hali ambayo inaweza kusababisha mgonjwa kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya vijidudu kwa urahisi,
  • kupata mikwaruzo na michubuko kirahisi, au kujihisi mchovu kila wakati.
  • Baadhi ya nywele za mwili hunyonyoka.
  • Kuathirika kwa seli zinazounda mfumo wa chakula na hivyo kusababisha mgonjwa kukosa hamu ya kula, kujihisi kichefuchefu, kutapika, kuharisha, na kutoka vidonda mdomoni.
  • Madhara mengine ni kama vile maumivu ya viungo, kuvimba miguu na vidole, kupata ganzi mikononi na vidoleni na matatizo ya kusikia.

Lishe na saratani ya koo

Lishe ni jambo la muhimu sana kwa mgonjwa wa saratani ya koo. Chanzo kikuu cha vifo kwa wagonjwa wa saratani ya koo ni utapiamlo pamoja na upungufu wa kiwango cha sukari mwilini yaani hypoglycemia unaosababishwa na mgonjwa kushindwa kumeza chakula. Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha mgonjwa anapata lishe kamili kwa ajili ya mwili.

Iwapo mgonjwa anashindwa kabisa kula, daktari anaweza kutumia njia kadhaa za kuhakikisha mgonjwa anapata chakula. Mojawapo ni ya kutumia mpira wa maalum wa  kupitishia chakula (feeding tube) katika koo ambalo husaidia kupitisha chakula mpaka kwenye tumbo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags