Enzi za uhai wake hakuchoka kuitumikia Tasnia ya filamu

Enzi za uhai wake hakuchoka kuitumikia Tasnia ya filamu

Mwigizaji wa Marekani, James Earl Jones ambaye alipata umaarufu kupitia filamu kama ‘Coming to America’ amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 93.

Taarifa ya kifo chake imetolewa na wakala wake, Barry McPherson kwa kueleza kuwa James amefikwa na umauti siku ya jana Jumatatu asubuhi akiwa nyumbani kwake Hudson Valley huko New York akiwa amezungukwa na familia yake. Mpaka kufikia sasa sababu ya kifo chake bado haijawekwa wazi.

Aidha baadhi ya mastaa wenzake wameonesha kuumizwa na taarifa hiyo akiwemo LeVar Burton, ambaye aliigiza na mkali huyo kwenye filamu ya “Guyana Tragedy: The Story of Jim Jones,” kwa kuandika kupitia ukurasa wake wa X: “Hakutakuwepo mwingine aliye na mchanganyiko wa neema kama yeye."

Jones aliyekuwa mwasisi wa kupinga ubaguzi wa rangi, mwaka 1965 alikuwa mmoja wa waigizaji wa kwanza wa Kimarekani mwenye asili ya Kiafrika kuonekana kwenye tamthilia iliyokuwa ikiruka mchana iitwayo ‘As the World Turns’.

Katika moja ya mahojiano yake ya kukumbukwa ya mwaka 2014, James alifunguka sababu ya kuendelea kuonekana kwenye filamu kadhaa kubwa licha ya umri kumtupa mkono akiweka wazi kuwa siri ni kutoisahau nafasi yake ya uigizaji.

“Siri ni kutokusahau kamwe kuwa wewe ni mwigizaji ambaye safari yako itaendelea muda wote, na hakuna kitu kinachokuwa cha mwisho kwako, hakuna kitu kinachokuwa bora zaidi, hakuna kitu kinachokuwa kibaya zaidi, kwangu mimi bado najiona ni mwanafunzi kwenye tasnia hii,” alisema James.

Enzi za uhai wake alishinda tuzo mbalimbali zikiwemo za Tony, Emmy, Grammy pamoja na Tuzo ya Heshima ya Oscar Mwaka 2011.

James Earl Jones alizaliwa Januari 17, 1931 Arkabutla, Mississippi na ameonekana kwenye filamu kama Field of Dreams, Coming To America, Conan the Barbarian, The Lion, Return of the Jedi na nyinginezo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags