Mwaka fulani aliibuka msanii wa Bongofleva anayeitwa Harmorapa. Jamaa aliiteka mitandao ya kijamii akaondoka na kijiji. Na sio kwamba alikuwa mbadi kwenye muziki, hapana. Alikuwa wa kawaida sana au chini ya kawaida kama nataka kuwa sahihi zaidi.
Gia aliyoingilia katika gemu ni kwamba yeye anafanana na msanii Harmonize. Kipindi hicho Harmonize yupo Wasafi. Na ndiyo maana hata jina alikuwa anajiita Harmorapa akimaanisha yeye ni kama Harmonize, lakini anayerapu kwa sababu alikuwa anafanya hip hop.
Harmorapa aliitwa katika kila chombo cha habari kikubwa kipindi kile. Hata mimi mwenyewe nilimuita na kumfanyia mahojiano.
Baadaye alikuwa mkubwa zaidi hadi P Funk Majani prodyuza muasisi wa Bongofleva alimchukua na kumfanya msanii wake.
Watu walimponda P Funk wakamuona kama amechanganyikiwa. Watu walijiuliza P Funk ameona nini kwa huyu dogo asiyejua kuimba? Ina maana P Funk ameshindwa kutofautisha kati ya kutrendi na kuwa na kipaji?
Jibu la P Funk lilikuwa ni “hata nilipomchukua Juma Nature watu walisema hivyo hivyo.” Hii ni sawa na kusema P Funk alikuwa anajiona anakwenda kutengeneza Sir Nature mwingine. Lakini, safari hii P Funk na ukongwe wake wote hakuwa sahihi.
Harmorapa alipotea na hakuwahi kugusa hata punje ya heshima anayotembea nayo Juma Nature Kiroboto.
Sasa hivi ameibuka msanii mwingine. Anaitwa Dogo Rema. Ni msanii ambaye mitandaoni tunafahamu yuko chini ya ‘influesa’ mmoja hivi. Dogo bwana dah!. Lakini, jinsi anavyojitokeza mbele ya watu, mbele ya kamera lazima utamkubali. Ana mbwembe.
Ana machejo kinoma. Anavyojionyesha ni kama msanii haswa. Anajiita Dogo Rema kwa sababu naamini anaamini anafanana na Rema. Narudia tena nilichosema hapo juu.
Dogo Rema kuimba mmmh! Lakini, mbwembwe za kuonekana kwenye mitandao anazo. Na mara nyingi mtu akitrendi bila kuwa na utaalamu anaishia kuja na kuondoka.
Hadumu. Mfikirie Piere Konki Likwidi. Alitrendi kwa sababu aliingia na staili yake ambayo wengi tunaijua. Hakuwa msanii. Hakuwa muigizaji.
Mwisho wake akaondoka akatuacha na mitandao yetu. Unamkumbuka hayati Mia Tisa Itapendeza? Alitrendi bila kuwa muigizaji, mcheza mpira au mwimbaji. Akaondoka akatuacha na mitandao.
Kataa au ukubali ukitrendi bila utaalamu au kipaji kilichozoeleka kudumu kwenye gemu ni kazi ngumu. Utakuja utaondoka na mitandao itamtrendisha mtu mpya na wewe utasahaulika.
Kama Dogo Rema na menejimenti yake watakuwa na hekima wasihangaike sana kumsukuma kuwa kama Mbosso au Aslay kwani kipaji hicho kuwa nacho ni kazi ngumu.
Na wanachopaswa kufanya ni kumsukuma katika kupata matangazo, madili ya hapa na pale apige pesa zake kipindi hiki ambacho bado wa moto kisha akazitumie kufanya mambo mengine. Piga pesa uende zako Dogo Rema.

Leave a Reply