“Kuvaa nguo ya ndani ambayo ni mbichi kunatengeneza fangasi ukeni, fangasi inaathari kubwa ikiwemo ya kula hadi mfumo wa uzazi, hivyo upo uwekezano mkubwa hasa kwa mwanamke kupata tatizo la uzazi,”
Hiyo ni kauli ya Dk. Elizabeth Lema kutoka hospitali ya Cornwell Tanzania ambaye amefunguka na kuweka wazi athari za uvaaji wa nguo mbichi za ndani hasa kwa upande wa wasichana.
Anasema uvaaji wa nguo za ndani ambazo ni mbichi si salama kiafya hasa kwa wanawake kwani utengeneza fangasi ukeni ambazo zikimpata mtu upata athari katika mfumo wake mzima wa kizazi.
“Fangasi ni ugonjwa mkubwa sana na umekuwa ukiwatesa wasichana wengi mno na hiyo ni kutokana tiba yake sio rahisi ndio maana basi tunawaambia watu kuacha kabisa tabia ya uvaaji wa nguo mbichi za ndani,” anasema
Dk. Lema anasema hata uvaaji wa nguo za mpira au plastiki sehemu za siri utengeneza pia fangasi kwani zimekuwa zikihifadhi unyevunyevu ambao ndio utengeneza hizo fangasi.
“Ndio maana ukipata shida ya kuwashwa sehemu za siri unashauriwa uvae nguo za kotoni ambazo uondoa yale majimaji yanayotoka na kumfanya mtu kuwa mkavu wakati wote,” amesema
Dalili za fangasi
Dk. Lema anafunguka na kusema dalili zinazoonesha kuwa unaugonjwa wa fangasi za ukeni zipo nyingi lakini moja wapo ni muwasho sehemu za siri, kutokwa na vipele vidogo vidogo ukeni.
Anasema dalili zingine ni kutokwa na uchafu mweupe au wa rangi ya kijivu ukeni wenye harufu mbaya, kutokwa vidonda au michubuko ukeni.
“Dalili zingine za mtu mwenye fangasi ni kutokwa na harufu mbaya ukeni, kupatwa na maumivu makali wakati wa tendo la ndoa, kuvimba na kuwa mwekundu katika mdomo wa nje wa uke pamoja na kuwaka moto ndani na nje ya uke,” anasema
Kinga ya fangasi za kike
Dk. Lema anasema moja ya kinga ya fangasi hizo ni kuacha kabisa kuvaa nguo za ndani ambazo ni mbichi kwani hiyo ni moja ya njia itakayokufanya usipate fangasi.
Anasema wasichana wanapaswa kuepuka kuosha uke kwa kutumia vitu vyenye kemikali kama sabuni pamoja na kuepuka kutumia marashi yenye kemikali ukeni na kuingiza vitu mbàlimbali ukeni kama vidole na asali.
“Wewe msichana epuka kutawadha kutokea nyuma kwenda mbele baada ya kujisaidia haja kubwa au ndogo, lakini pia mtibu mpenzi wako alie na Ugonjwa wa fangasi,” anasema
Anasema kuwa msichana unapaswa kusafisha uke na kujifuta kwa kitambaa safi ilikuuacha mkavu na kuongeza kuwa ni muhimu kuvaa nguo za ndani zinazotengenezwa na vitu halisi kama Pamba na hariri.
“Pia epuka ulaji mbaya wa chakula hasa kwa kupunguza kula vyakula vyenye sukari kwa wingi, tumia Pads zisizo na kemikali na zenye vitu vya kukulinda na maambukizi, kukufanya uwe mkavu na huru,” anasema.
Dk. Lema anasema kuwa katika kutibu fangasi ni muhimu pia kutumia dawa za asili za virutubisho na kuacha zenye kemikali wakati wa kutibu fangasi za ukeni.
Ushauri
Dk. Lema anasema anatambua kwa idadi kubwa ya wanafunzi wa kike hasa waliopo vyuoni wanaweza kuongoza kwa kuvaa nguo za ndani mbichi na hiyo ni kutokana na mazingira yaliyokuwa nayo.
Anasema anapenda kuwashauri kuacha tabia hiyo mara moja kwani ina athari kubwa kiafya hivyo anawataka kufua nguo zao na kuzianika nje sio ndani ili zikauke na jua.
“Tuache kufua taiti au chupi kisha kuzianika ndani na ukiamka asubuhi haijakauka unaivaa tu, hapana tuache kabisa mtindo huo, amka mapema asubuhi fua nguo yako na anika nje ikauke na jua kisha ndio uivae.
“Nasisitiza tu nguo za ndani zinazofaa kuvaliwa ni zile za kotoni, achene kabisa kuvaa hizi za mpira maana si salama kabisa kiafya,” anasema
Leave a Reply