Diddy Azidi Kuelemewa Na Mashitaka

Diddy Azidi Kuelemewa Na Mashitaka

Machi 6, 2025, waendesha mashtaka wa shirikisho walifungua hati mpya ya mashtaka dhidi ya Sean "Diddy" Combs, wakimtuhumu kwa kulazimisha wafanyakazi wake kufanya kazi kwa muda mrefu na kuwatishia adhabu ikiwa wasingemsaidia katika mpango wake wa usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya biashara ya ngono iliyodumu kwa miaka ishirini.

Katika hati hiyo mpya iliyowasilishwa mahakamani inadai Combs na washiriki wake ambao hawajawekwa wazi walitumia nguvu za kimwili, vitisho vya fedha na matendo mengine ya kuharibu saikolojia kudhibiti wafanyakazi hao.

Wafanyakazi hawa walilazimishwa kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupata usingizi, wakihofia kupoteza ajira zao kwa ajili ya kutii matakwa ya Diddy huku mmoja wa wafanyakazi hao akilazimishwa kushiriki katika vitendo vya ngono na Combs.

Mbali na hayo, mmoja wa mfanyakazi wa zamani wa Diddy aitwaye Phillip Pines, Desemba 2024 alifungua kesi akidai alilazimishwa kuandaa na kusafisha mazingira yaliokuwa yakifanyika sherehe za kingono zilizojulikana kama ‘Wild King Nights’ akidai kuwa aliandaa vyumba vya hoteli kwa taa nyekundu, pombe, dawa za kulevya, na vifaa vingine vya ngono, na baadaye kusafisha ushahidi wote wa shughuli hizo. Pia alidai kulazimishwa kushiriki katika vitendo vya ngono.

Combs, mwenye umri wa miaka 55, alikamatwa Septemba 16, 2024, jijini Manhattan, na kushtakiwa kwa makosa ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono, njama ya kihalifu, na kusafirisha watu kwa madhumuni ya ukahaba.

Aidha rapa Combs amekana vikali mashtaka yote dhidi yake huku mawakili wake wakiweka wazi kwamba hajawahi kumlazimisha mtu yeyote kushiriki katika vitendo vya ngono bila ridhaa yao. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani tena Machi 14 kwa ajili ya mashtaka mapya, na kesi yake imepangwa kuanza kusikilizwa Mei 5, 2025.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags