Diamond Mbana pua mwenye damu ya Hip Hop

Diamond Mbana pua mwenye damu ya Hip Hop

RAMADHAN ELIAS

KOLABO la Diamond Putnumz na Mr Blue ndio habari ya mjini kwa sasa. Wimbo ni 'Mapozi' humo ndani akiwemo pia Jay Melody. Inabamba kinoma huko kitaa.

Gemu ya Hip Hop ina asili yake, miiko yake na ladha yake. Ndio maana wasanii wengi wa RnB wanaihusudu.

Inaaminika chimbuko la aina nyingine za Muziki ni Hip Hop. Tangu mwanzoni mwa miaka ya 1970, miondoko hii ilipoanzishwa huko Bronx, New York, Marekani, imekuwa na mitazamo tofauti kwenye harakati za maisha kuanzia, siasa, maendeleo na uchumi. Ni muziki unaobeba maisha ya watu.

Kurap ni moja kati ya miiko minne ya Hip Hop, mingine ni DJ, grafiti (sanaa ya uchoraji kwa kutumia rangi maalumu) na kudansi kwa mtindo wa kuvunja viungo. Wanahip hop wanaelewa.

Hata hivyo, si kila mwanahiphop anaweza kurap, atafanya moja ya miiko hiyo, lakini kurap ndio imekuwa kama utambulisho mkubwa kwenye hip hop.

Aina hii ya muziki imekuwa ikibadilika kutokana na mazingira, tangu ulipoanza miaka ya 1970 hadi sasa staili ya kurap imebadilika, hata hivyo bado inasimama kwenye miiko yake.

Wengi wamefanikiwa kwenye muziki huu hasa huko Masrekani ulikoanzia, kwa hapa Tanzania wapo pia waliofanikiwa na wengine wakashindwa kabisa kuingia huko ingawa walijaribu kurap.

Diamond Plutnumz, ni mmoja wa wanamuziki wanaofanya vyema kwenye Bongo Fleva. Lakini wengi hawajui alikoanzia. Mwenyewe anasema alikuwa akichana 'kurap', kabla ya kuamua kuimba kawaida 'kubana pua'.

Inaweza ikawa hujawahi kusikia wimbo wake wa Hip Hop, lakini ni kweli. Mondi ni kipaji halisi. Ana uwezo wa kufanya aina yoyote ya muziki na akashirikiana na wasanii wa aina yoyote, sio wa nyimbo za kihindi, taarabu, singeli, rhumba, reggae na mingine.

Kwenye hip hop ndio usiseme, mbali na kuwahi kuchana na kuonyesha anaweza, amekuwa akiuhusudu muziki huu na kila mara amekuwa akishirikishwa na wasanii wakubwa ndani na nje ya Tanzania kwenye hit zao za Hip Hop.

Nyingi ya nyimbo hizi, ameimba mashairi na kiitikio.

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea baadhi ya ngoma za rap na Hip Hop ambazo Diamond amehusika nazo.

'I HATE YOU' -DIAMOND

Wengi watakuwa hawaijui hii ngoma. Ni mkwaju wa miaka ya nyuma kidogo ambao Mondi alimshirikisha Hemedy PHD.

Humu Diamond alionyesha mahaba yake kwenye kurap kwani alichana vesi mbili huku Hemedy akimbia kiitikio. nyimbo ina mahadhi ya mapenzi lakini akionyesha chuki kwa mlengwa. Yaani anamchukia aliyekuwa mpenzi wake.

'FRESH REMIX' - FID Q

Wimbo 'Fresh' wa Fid Q alioufanya peke yake ulipita masikioni mwa wapenzi wa Hip Hop. Ukahit sana na baadaye, ulimwengu wa Hip Hop ukashtuka kusikia mistari ya Mondi kwenye 'Fresh Remix' wakiwa pamoja na Rayvanny.

Wimbo huo ulifunika ule orijino na kutokana na mistari ya Mondi akirap, uliifanya hadhira itikise kichwa ikikubali anajua.

'KIPI SIJASIKIA' - PROFESA JAY

Mwaka 2014, mashabiki wa muziki nchini walijikuta wakiingia kwenye mfumo baada ya lijendi Profesa Jay kumvuta Diamond na kumweka kwenye ngoma ya Hip Hop iliyokwenda kwa jina la 'Kipi Sijasikia'.

Profesa humo alichana sana ikiwemo uhalisia wa maneno yaliyokuwa yakisemwa kuhusu yeye lakini Mondi aliingia na kulainisha akiimba kiitikio na ngoma kuwa habari ya mjini kwa wakati huo. Huo ni muendelezo wa Mondi kujichanganya kwenye Hip Hop.

'KOMANDO' - G NAKO

Novemba mwaka jana mitaa ilisimama baada ya Mkali G- Nako kumpa shavu Mondi kwenye ngoma yake iitwayo 'Komando' na wimbo huo kusambaa kila kona.

Usishangae ngoma hii kuwekwa kwenye kundi la Hip Hop. Lengo ni G-Nako mwenyewe. Huyu jamaa ni mwana Hip Hop kitambo akianzia gemu kwenye kundi la Nako 2 Nako waliokuwa wagumu ile kinoma.

 Hata hivyo G-Nako amebaki kuwa mwana Hip Hop akiwa na kundi lake la Weusi na amefanya ngoma zake kibao za Hip Hop na kushirikishwa huku akiwa miongoni mwa wakali wa Bongo ambao ni wanyama sana linapokuja suala la kupiga kiitikio kwenye ngoma.

Maisha na ubora wa G-Nako unamfanya kuimba ngoma za aina tofauti lakini asili yake ni Hip Hop na kwenye Komando amerap na kumwounyesha Mondi namna Hip Hop ilivyo damuni kwake.

'TUISHI NAO' - CHID BENZ

Nani asiyemjua Chid Benz? basi mkali huyo wa misimu yote kwenye Hip Hop aliingia Studio kwa Prodyuza S2Kizzy na kuweka vesi kwenye moja ya midundo aliyoikuta hapa.

Siku moja Mondi akiwa ameenda studio hapo kufanya kazi zake, akakutana na ngoma hiyo ya Chid. Mondi akaizimia kinoma na kumuomba S2Kizzy aweke kiitikio na ikawa kweli akamwaga korasi la maana humo.

 

Ilikuwa sapraizi kwa Chid alipoambiwa Mondi ameweka kiitikio kwenye ngoma yake na baadae wimbo huo ukawa moto. ukipata muda kauisikilize utakubaliana na mimi.

'ZIGO REMIX' - AY

Lijendi wa Hip Hop, AY baada ya kutoa ngoma ya Zigo na kufanya vizuri, Diamond alivutiwa nayo na kuomba kufanya Remix.

AY hakuwa na noma na kuafiki ombi la Mondi kisha wakaingia studio. Kilichotoka hapo ni balaa. Ngoma ilifanya vizuri na kuifunika ile ya mwanzo. Hiyo ilikuwa mwaka 2016 lakini wimbo huo ukiusikia hadi leo bado ni wa moto.

'MPAKA KUCHEE' - CHID BENZ

Hii ni ngoma nyingine ya Hip Hop ambayo Diamondi ametia sauti yake na kunata kisawa sawa na mdundo.

Humo ndani Mondi ameeimba kiitikio huku vesi zikisimamiwa na Malijendi wa Hip Hop Fid Q na AY ambao mistari yao imebebwa zaidi na viitikio ambavyo vimenyongwa na Diamond, usipime.

'MUZIKI GANI' - NEY WA MITEGO

Moja ya nyimbo zilizopendwa zaidi mwaka 2013 ni pamoja na 'Muziki gani' ambayo nyota wa Hip Hop Ney wa Mitego alimshirikisha Diamond.

Humo ndani ilikuwa ni vesi baada ya vesi, yaani Ney na Mondi walikuwa wakiimba kwa kupokezana na Ney alikuwa akiisifia Hip Hop huku Mondi akisimama na RnB. Licha ya kuchanana kinoma humo ndani, lakini Mondi alionyesha wazi anaiheshimu Hip Hop.

 

'PAMELA' - YOUNG KILLER

Wakati Diamond akiandaa Albamu yake 'A Boy from Tandale', aliona haiwezi kukamilika bila kuwemo kwa msanii wa Hip Hop.

Bila kuchelewa alimvutia waya mwanaHip Hop, Young Killer Msodoki na kufika studio kisha kuweka mistari yake kwenye ngoma iliyoitwa Pamela.

Baada ya albamu hiyo kutoka mwaka 2018, Pamela ilikuwa miongoni mwa ngoma zilizopendwa zaidi na hiyo ni kutokana na namna wawili hao walitisha kwa kuchanganya fleva.

'BBM' - NGWEAR

Nakurudisha nyuma tena kipindi mkali wa Hip Hop, Albert Mangwea 'Ngwear' akiwa hai. Mondi aliona isiwe tabu na kumwomba kolabo Ngwear aliyekuwa hashikiki wakati huo.

Ngwear akamkubalia Mondi na kumweka kwenye ngoma iitwayo BBM ambayo humo ndani yumo pia Mr Blue. Wengi watakuwa hawaifahamu hii ngoma lakini ipo na humo ndani Mondi kasimamia kiitikio.

'WAKA' - RICK ROSS

Diamond ni Hip Hop bwana. Baada ya kudondoka Marekani, aliwaacha wasanii wote wanaobana pua na kumfuata Mkali wa Hip Hop Rick Ross ili wafanye naye Kolabo na mwamba kufanya hivyo.

Wakaingia studio na kurekodi ngoma iliyokwenda kwa jina la 'Waka', na baada ya hapo ikawa habari ya mjini kuanzia Afrika hadi Ulaya ambako Rick Ross ana mashabiki kibao. Ngoma hiyo ni miongoni mwa kolabo kubwa za Diamond hadi sasa.

'MTOTO WA MAMA' - GODZILLA

Hayati Godzilla pia aliwaaminisha wadau wa muziki nchini Diamond ni msanii mwenye damu ya Hip Hop baada ya kumpa vesi kwenye ngoma yake ya 'Mtoto wa Mama' iliyofanyika studio za MJ Records.

 

Humo ndani Mondi hajabana pua bali amechana mistari na kwenda sambamba na Zilla ambaye alikuwa akiogopwa na marapa wengine kutokana na ubora wake wa kunata na biti.

'NASHINDWA' - CHANDE

Wakati Diamond akijitafuta kutafuta tobo la kutoka, aliingia studio na kufanya ngoma na rapa Chande na kuipa jina la Nashindwa.

Wimbo huo ulikuwa na mahadhi ya mapenzi na Chande alichana vesi za maana na Mondi akapiga kiitikio na ngoma hiyo kuwa kali na pendwa hadi kufikia kuifanyia video na ndani ya kichupa alionekana boss wa zamani wa Mondi, Bob Junior.

'MAKE ME SING' - AKA

Afrika Kusini mwaka 2016, Diamond alikomba mashabiki kibao baada ya kufanya ngoma na aliyekuwa mkali wa Hip Hop nchini humo AKA (kwa sasa marehemu).

Ngoma hiyo iliitwa Make Me Sing na kusindikizwa na bonge moja la video na kuifanya kushika namba moja kwenye chati mbalimbali Afrika.

Hizo ni baadhi ya ngoma ambazo zinamuidhinisha Diamond kuwa na damu ya Hip Hop, pia bado zipo nyingine nyingi ambazo hazijatoka.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags