Dalili kwamba mwanaume uliye naye si wako pekee yako

Dalili kwamba mwanaume uliye naye si wako pekee yako

Wakati mwingine ni vigumu kuamini, lakini jambo hili huwatokea wanawake wengi kwamba wanaume wanaotoka nao kuna uwezekano mkubwa wakawa wanatoka na wanawake wengine kwa nyakati tofauti na hufanya hivyo kwa siri sana. Inaweza ikawa ni mitoko ya kawaida lakini miongoni mwa hao wanaotoka nao wapo ambao watakuwa wanashiriki tendo na wakawa wameahidiwa kuolewa.


Hapa chini nitaeleza dalili zinazoweza kuwafanya wanawake kujua kwamba mwanaume anayetoka naye sio wakwake peke yake bali kuna wengine wanadanganywa huko waliko kama yeye.

1. Mnakuwa na ratiba ya kukutana siku maalum:
Baada ya kujuana unagundua kwamba bwana uliye naye anakuwa na kawaida ya kukutana na wewe kwa siku maalum tena anazopanga yeye, mwanaume anakuwa hana nafasi ya kushtukizwa miadi na akipanga ratiba yake hawezi kuibadilisha kirahisi. Anaweza kukupangia muwe mnakutana mara mbili kwa wiki na siku nyingine anasema yuko bize. Hapa inabidi ujiulize mara mbili.

2. Ugumu katika kukubali miadi:
Kama inatokea unamuomba mkutane kwa ajili ya mtoko siku fulani ni vigumu kukubali ombi hilo mara moja, sana sana ataishia kusema, "Inawezekana lakini sina uhakika" au "nitaangalia kama nitakuwa na nafasi." Pamoja na kutotoa jibu la kukubali moja kwa moja, lakini hatakuwa na sababu yoyote ya msingi ya kutokubali mualiko huo moja kwa moja. Mara nyingi wanajiumauma tu. Ukiona hivi akili kichwani mwako.

3. Usiri na kutokuwa wazi:

Kama mwanaume anatokea kumpenda mwanamke na ana matarajio ya kufika mbali na yeye, kwa maana kwamba huenda akafunga naye ndoa, atakuwa muwazi kwake hususan kuhusu maisha yake binafsi na shughuli zake. Lakini kama mwanaume akionekana kutokuwa muwazi na mtu anayeficha ficha kuhusu maisha yake na mambo yake, basi jua kwamba atakuwa na mwanamke mwingine anayetoka naye hivyo anaogopa kuweka mambo yake wazi ili asije akaharibu upande wa pili. Hapa mwanamke inabidi awe na akili kumkichwa.

4. Msururu wa marafiki wa kike:
Kwa kawaida wanaume wasiotulia wanakuwa na msururu wa marafiki wa jinsia ya kike, na huwa wanadai kwamba hao ni marafiki zake tu na hakuna jambo lolote zaidi ya urafiki wa kawaida, lakini kumbe ni urafiki unaomnufaisha kingono (friends with some benefits). Wanaume wenye kupenda kuzungukwa na wanawake wanakuwa katika nafasi nzuri ya kutoka nao kimapenzi hivyo huo mtego hauwezi kuwakosa na kama inavyojulikana kwamba wapo baadhi ya wanawake hupenda kutoka na wanaume wasiotulia, unadhani ataepuka mtego wao. Hivyo ukiona mwanaume ana msururu wa marafiki wa kike iwe ni wale anaokutana nao au wale wa kwenye mtandao, jua hauko peke yako.

5. Uzuri wa kubembeleza na lugha tamu:
Wanaume wasiotulia wanajua sana kubembeleza na wanakuwa na lugha tamu ambayo huwavutia wanawake, ni wazuri sana katika mazungumzo na ni rahisi kuteka hisia za mwanamke yeyote amtakaye. Mara nyingi ni rahisi kuwanasa wanawake wapendavyo kwa sababu wanajua sana kubembeleza na kujali hisia za wanawake. Lakini hata hivyo siyo wanaume wote wenye haiba hiyo kwamba hawajatulia, bali baadhi hutumia haiba hiyo kuwanasa wanawake kiurahisi. Hapa nashauri tu mwanamke achunguze kwa makini kabla ya kutuhumu eti kwa sababu Mtambuzi kasema. 

6. Kushtukiza mitoko:
Wanaume wasiotulia mara nyingi wanakuwa ni mabingwa wa kushtukiza mitoko (dates) pale ambapo mwanamke hatarajii kutoka, hushtukizwa kwa simu au ujumbe mfupi wa simu kwamba ajiandae kwa mtoko na akiuliza mbona imekuwa ghafla hivyo, jibu lake litakuwa ni rahisi tu, "It is a Suprise" Nilikuwa nataka kukushangaza tu. Na kwa kuwa wanakuwa na lugha tamu, ni rahisi kubembeleza na kukubaliwa huo mtoko.

7. Tatizo la kutunza kumbukumbu:
Siyo kila mtu anaweza kuwa na kumbukumbu nzuri, lakini kwa kawaida kama unamjua mtu fulani, ni lazima kuna kumbukumbu zitakujia kuhusu tabia zake na vitu vinavyomhusu mtu huyo. Lakini kama inatokea kila unapokuwa na mwanaume unayetoka naye anakusimulia stori hiyo hiyo kila mnapokutana na kukuliza maswali yale yale anayokuuliza kila mnapokutana pamoja na kwamba umekuwa ukimjibu mara kwa mara na anakuwa na na matatizo ya kuweka kumbukumbu, jua kwamba hauko pekee yako, kuna wanawake wengine anatoka nao hivyo hakumbuki stori ipi alimsimulia nani au aliwahi kukuuliza swali hili au la.

8. Kukuchukulia kama rafiki tu:
Hii ni dalili mojawapo ambayo haina mjadala, pale ambapo mwanaume unayetoka naye anakuchukulia kama rafiki na siyo mpenzi wako, hususan pale anapokuwa na marafiki zake au kama mwanaume unayetoka naye hakuiti mpenzi, au hakutambulishi kwa marafiki zake kama wewe ni mpenzi wake, basi jua kwamba anao msururu wa wanawake anaotoka nao hivyo anaogopa kuwachanganya marafiki zake na kuonekana kama hajatulia. Inama chini ufikiri.

9. Ni vigumu kutimiza ahadi:

Kwa kawaida wanaume wana kawaida ya kusema jambo lolote ambalo wanajua litamvutia mwanamke, Wengi wao hupenda kuahidi mambo makubwa, lakini tatizo ni utekelezaji wa ahadi hiyo. Anaweza kumuahidi mwanamke kumpa zawadi aliyokuwa akiitamani au kumpeleka visiwani kwenye hoteli za kitalii kwa ajili ya kujipumzisha na kuponda raha, lakini ahadi hizo zitaendelea kuwa hadithi za Alinacha. Wanaume wasiotulia wanakuwa ni mahiri sana wa kutumia lugha laini kuwalainisha wanawake, hilo tu na si vinginevyo.

10. Mapenzi kwa mgao:
Huwezi kujua kama tendo litafanyika au halitafanyika, hata kama mkiwa mmejifunika shuka moja kitandani. Kuna wakati tendo hufanyika kwa umahiri mkubwa mpaka unajisikia raha, lakini kuna siku ambayo kutokana na mazingira unaweza kujua kwamba gwaride litachezwa, lakini ukaambulia kapa, basi hapo jua kwamba, kuna mwanamke mwingine mahali fulani ana miadi ya kukutana naye hivyo anakwepa ili kukusanya nguvu za kutumika kwingine.

Kaa Chonjo!







Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags