D Voice, Zuchu wapo mbio sana

D Voice, Zuchu wapo mbio sana

Ni wazi kuwa waimbaji wa Bongofleva kutokea WCB Wasafi, D Voice na Zuchu wapo mbio sana kuwapa burudani mashabiki wao ukilinganisha na wenzao katika rekodi lebo hiyo iliyoanza kusaini wasanii miaka 10 iliyopita.

Utakumbuka wawili hao ndio wasanii wa mwisho kutambulishwa na WCB Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platnumz, mshindi wa tuzo tatu za MTV Europe Music Awards (EMAs) na akiwa kinara barani Afrika.

Zuchu aliyeshindwa kufua davu katika shindano la Tecno Own The Stage 2015, yeye alitambulishwa kupitia EP yake, I Am Zuchu (2020), huku D Voice aliyetoka na kibao chake, Kuachana Singapi (2021), akitambulishwa na albamu yake, Swahili Kid (2023).

Kwa kipindi cha takribani miaka miwili, D Voice na Zuchu tayari wameshirikiana katika nyimbo nne wakiwa ndio wasanii waliofanya kolabo nyingi kwa muda mfupi ndani ya WCB Wasafi inayowasimamia wasanii watano kwa sasa.

Ndani ya albamu ya D Voice, Swahili Kid (2023) alimshirikisha Zuchu katika nyimbo mbili, Nimezama (2023) na BamBam (2023) ambao video yake imetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 16 ikiwa video pekee ya D Voice kufikia namba hizo.

Baada ya kuona kolabo na Zuchu zinalipa, D Voice akampa tena nafasi binti huyo wa Khadija Kopa katika wimbo wake, Nani (2024) uliopata mapokezi mazuri huku video yake ikiwa ya pili kwa msaniii huyo kutazamwa zaidi YouTube.

Ikumbukwe D Voice ni msanii wa nane kusainiwa na WCB Wasafi baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Mbosso (2018) na Zuchu (2020).

Hata hivyo, wasanii watatu wameshaachana na lebo hiyo na kwenda kufungua zao, nao ni Rich Mavoko - Billionea Kid, Harmonize - Konde Music Worldwide na Rayvanny - Next Level Music (NLM).

Naye Zuchu akagundua kufanya kazi ni D Voice ni biashara inayotoka kwa haraka, ndipo akampa shavu katika albamu yake ya kwanza, Peace and Money (2024) inayofanya vizuri kwa sasa ikiwa na nyimbo 13 huku ikishirikisha wasanii saba.

Katika albamu hiyo, D Voice amesikika katika wimbo mmoja, Hujanizidi (2024) ambao video yake imetoka wiki iliyopita ikionyesha maisha ya uswahilini na vitimbi vyake kama maudhui ya wimbo huo unavyojieleza.

Na kwa matokeo hayo D Voice aliyefahamika kupitia muziki wa Singeli, anakuwa msanii wa pili Bongo aliyeshirikiana mara nyingi zaidi na Zuchu baada ya Diamond huku Mbosso na Rayvanny wakifuatia.

Utakumbuka albamu hiyo ya Zuchu imejumuisha wimbo wake, Wale Wale (2024) akiwa na Diamond ambao uliotangulia kutoka, na huo ni wimbo wa tano kushirikiana baada ya Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022) na Raha (2024).

Hivyo ni wazi D Voice anaifukuzia rekodi ya Diamond kwa Zuchu ambaye pia ndiye msanii pekee wa kike Bongo aliyeshirikiana mara nyingi na Diamond aliyetoka kimuziki na kibao chake, Kamwambie (2009) kilichobeba jina la albamu yake ya kwanza.

Ikumbukwe Diamond aliyeshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2010, wasanii wengi aliowasaini WCB Wasafi wamekuwa na mafanikio makubwa kimuziki, mathalani Zuchu tayari ameshinda tuzo saba za TMA ndani ya muda mfupi tu.

Ni Zuchu anayeshikilia rekodi kama msani wa kike Afrika Mashariki aliyetazamwa zaidi YouTube kwa muda wote, huku pia akiwa namba moja Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kujizoelea wafuasi wengi katika mtandao huo akifuatiwa na Yemi Alade wa Nigeria

Na Peter Akaro






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags