Chanzo, wasanii wengi wa hip-hop kufariki kwa kupigwa  risasi

Chanzo, wasanii wengi wa hip-hop kufariki kwa kupigwa risasi

Matukio ya wasanii kupigana risasi yamekuwa yakisikika kila kukicha katika baadhi ya mataifa, kama ilivyotokea Februari 10, 2023 kwa msanii AKA kutoka nchini Afrika Kusini , kutokana na hayo wapenzi wa muziki wamekuwa  wakiendelea kuumizwa hisia zao kutokana na vifo vya wasanii wanaowapenda. 

Tukiachana na wasanii wa Afrika ambao wengi wao wamekuwa wakipoteza maisha kwa sababu za magonjwa ajali na sababu nyingine tofauti na kupigwa risasi kwenye kama ilivyokuwa kwa AKA. Nchi nyingi za Ulaya wasanii wengi hasa wa muziki wa hip-hop wamekuwa wakipoteza maisha kwa kupigwa risasi, tofauti na idadi ya wale wanafariki kwa matatizo ya kiafya.

Jambo hilo limekuwa na mifano hai kutoka kwa baadhi ya nguli wa muziki waliopendwa na watu wengi, huku ngoma zao zikiendelea kuishi kwenye mioyo ya mashabiki hadi leo kutokana na rekodi walizoacha.

Siku chache zilizopita kesi dhidi ya kifo cha aliyekuwa mwanamuziki wa hip-hop Tupac Shakur imefufuka upya huku wengi wakiwa na hamu ya kutaka kumfahamu muhusika wa kifo cha mkali wa ‘Dear Mama’ ambacho kwa miaka 27 saa kimekosa majibu, huku ya kifo chake bado tunabaki palepale kwenye mchezo mchafu wa risasi. 

Ukiachana na Tupac, wasanii wengi kutoka Ulaya imekuwa ni nadra sana kukuta wamefariki kwa magonjwa bali wengi wao vifo vyao husababishwa na matatizo mengine hasa kupigwa risasi. 

Matukio hayo hayakuanza kwa Tupac tu bali yalikuwepo toka enzi na enzi na hadi saa bado yanaonekana kuendelea, kwani vifo vya baadhi ya wasanii vimeendelea kutokea kwa mfumo huo huo. 

Baadhi ya wasanii waliouawa kwa kupigwa risasi

 Kirsnick Khari wengi walimfahamu kwa jina Takeoff  rapper huyo kutoka nchini Marekani aliwaburudisha wapenzi wa muziki wa kufoka akiwa wenye kundi la Migos, lililokuwa na watu watatu akiwemo Offset na Quavo.

Mshumaa ulizima na majozi yaliwapata mashabiki wa kundi hilo Novemba mosi 2022, baada ya rapper huyo kupoteza maisha kwa kupigwa risasi  akiwa na umri wa miaka 28, katika eneo la Houston, Texas, US huku mtuhumiwa wa kifo chake akiwa Patrick Xavier Clark ambaye hadi sasa bado yupo mikononi mwa sheria. 

Bashar Jackson maarufu kama Pop Smoke, alikuwa  msanii wa muziki wa hip-hop kutoka nchini Marekani naye ni miongoni mwa wasanii waliofariki kwa kupigwa risasi huku kwa upande wake Februari 19, 2020 akiwa na umri wa miaka 20 tu alikatishwa uhai wake kwa kupigwa risasi akiwa Los Angeles, California, huku kifo chake kikihusishwa na watu wawili akiwemo Corey Walker na Keandre Rodgers.

 

Licha ya ukali wake kwenye kufoka lakini pia alikuwa mbaya kwenye upande wa uandishi wa mistari ya ngoma. Pop enzi za uhai wake alisumbua na ngoma kama vile ‘Element’.

 

Ermias Asghedom maarufu kama Nipsey Hussle, ni rapper kutoka nchini Marekani ambaye alifanya vizuri na ngoma kama vile ‘Racks In The Middle’ lakini Machi 31, 2019 akiwa na umri wa miaka 33 mambo yaligeuka baada ya msanii huyo kupoteza maisha kwa kupigwa risasi akiwa Los Angeles, California, US kama ilivyokuwa kwa Pop Smoke.

 

Kutokana na kifo cha msanii huyo alidakwa  Eric Ronald Holder Jr akiwa ni mtuhumiwa namba moja wa mauaji hayo. 

Mkali wa muziki wa hip-hop Travon Smart maarufu kama Jimmy Wopo uwepo wake ulitoweka machoni mwa mashabiki wake kutokana na kifo chake kilichotokea Juni 18, 2018 akiwa na miaka 21 kwa kupigwa risasi  akiwa Pittsburgh, Pennsylvania, US huku mtuhumiwa wa kifo chake hadi leo bado hajafahamika, kati ya ngoma alizotamba nazo ni ‘Gangsta’.

Maumivu yalikuwa makali sana kwa wapenzi wa muziki wa hip-hop kwani Juni 18, 2018 siku ambayo aliuawa Jimmy Wopo, ndiyo siku aliyouawa pia XXXTentacion mwanamuziki ambaye alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na ngoma alizoachia na aina ya maisha aliyokuwa akiishi. Kifo chake kilitokea akiwa Deerfield Beach, Florida, US ambapo  kilihusishwa moja kwa moja na  wanaume wanne ambao walidaiwa kumpiga risasi msanii huyo aliyekuwa na umri wa miaka 20 tu. 

Kifo cha Tupac Shakur nacho ni kati ya vifo ambavyo vimekuwa vikiumiza vichwa vya watu wengi kwa kutaka kufahamu muhusika halisi wa tukio hilo ni yupi.

Septemba 13,1996 akiwa Las Vegas, Nevada, US, ilibaki ‘stori’  kwenye Tasnia ya Muziki wa Hip-hop kuwa aliwahi kutokea mkali ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa na umri wa miaka 25 huku mwanzo Orlando Anderson akiwa mtuhumiwa wa tukio hilo ambalo siku za hivi karibuni limegeuka na kushikiliwa mtuhumiwa mwingine wa mauaji hayo aitwaye  Duane Keith Davis. 

Kati ya wasanii wengi waliopoteza maisha yao kwa kupigwa risasi Christina Grimmie ni miongoni mwa wasanii wa kike waliofariki katika matukio ya aina hiyo, huku mtuhumiwa wa mauaji yake akiwa Kevin James Loibl, ambaye alidaiwa kumpiga risasi msanii huyo wa pop katika maeneo ya Orlando, Florida, US June 10, 2016. 

Kutokana na baadhi ya majina ya wasanii waliofariki kwa kupigwa risasi swali kubwa lililopo kwa watu wengi ni kwa nini wasanii wengi wahapotezi maisha kwa kuugua kama ilivyozoeleka katika nchi za Afrika?

Ukweli ni kwamba matukio hayo wala hayatokei kwa bahati mbaya kwani kuna sababu kadhaa ambazo husababisha wasanii kupigwa risasi na kupoteza maisha yao.

Ikiwemo matatizo binafsi, kama ilivyo kwa watu wasio na umaarufu wowote kugombana ndivyo hutokea pia kwa wasanii kuwa na ugomvi ambao mara nyingi huambulia kwenye kurushiana risasi, kwani wengi wao humiliki silaha za kujilinda.

 

 

Wakati mwingine hujikuta wakiingia katika ugomvi wa kimapenzi kama ilivyotokea kwa mwanamuziki wa hip-hop Tory Lanez ambaye hadi sasa bado anasota gerezani kwa kumpiga risasi mpenzi wake Megan Thee Stallion ambaye naye ni msanii.

 

Aidha wasanii wengi wamejikuta kwenye wimbi la kutumia dawa za kulevya ambazo zinaweza kusababisha utata na ugomvi kwa baadhi ya watu ambao huwapa wasanii dawa hizo, na matokeo yake huangukia kwenye kupigana risasi.

 

Uhasama wa kisiasa nao kwa baadhi ya wasanii umekuwa changamoto hasa pale wanapotaka kuwasilisha jumbe fulani zenye ukakasi wa kufichua maovu ya kisiasa yafanyikayo, hujikuta  wasanii wengi wakiingia kwenye uhasama wa kisiasa ambao huwa na matokeo ya vifo vya kupigwa risasi.

 

Pamoja na hayo wasanii wamekuwa wakiishi maisha ya kuonesha kila kitu wanachofanya hapo ndipo hudakwa, wengi hupendelea ku-share location waliyopo bila kujali kuwa wana maadui wengi na marafiki wengi pia , na katika hilo ndipo maadui hutumia nafasi hiyo kufika na kuwamaliza kirahisi.

Kutokana na kuonekana wasanii wengi wa muziki wa hip-hop ndiyo wahanga wakubwa wa kuuliwa kwa kupigwa risasi muandishi wa habari na mtangazaji mbobezi wa muziki wa Hip-hop Tanzania Jabir Saleh ametolea ufafanuzi kwa kueleza sababu zinazopelekea wasanii hao kuwa wahanga wakubwa wa matukio hayo.

“Hip-hop ni utamaduni ambao uliletwa kwa ajili ya kuifanya jamii ya watu weusi waweze kuongea mambo ambayo yanaikumba jamii yao lakini, baadaye iligeuka na mambo mengine ya kibiashara yakaingia kwenye hip-hop, kama vile biashara za madawa ya kulevya, ambayo yalifanya utokee mgawanyiko wa makundi kati yao. 

Walio kwenye makundi ya madawa waligeukana na kuanza kutofautiana, kwa hiyo makundi mengi yakawa yanaendelea kuzaliwa na hapo ndipo matatizo yalipoanzia.Kuna wasanii walizaliwa kutoka kwenye makundi hayo na ukiwa ‘staa’ umezaliwa kutoka kundi fulani wanakuwa wanakulinda na kawaida kutokana na kulindwa msanii anaanza kushirikiana nao kwa kuwasaidia. 

Hivyo basi makundi mengine huanza kumchulukia msanii kama adui kwani anasaidia kundi jingine ndipo hapo uadui na chuki kutoka kwa makundi mengine inapelekea wao kuuawa.

Ni wasanii wachache ambao wamepigwa risasi kwa bahati mbaya lakini wengi wanapigwa kwa makusudi kwani wanakua na ushirika mkundi hayo.”Anasema Jabir

 

MWISHO






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post