Burna Boy afanya kama Navy Kenzo

Burna Boy afanya kama Navy Kenzo

Mwanamuziki wa Nigeria Burna Boy, amefungua shule ya kufundisha soka nchini humo ikiwa na lengo la kukuza vipaji vya vijana wacheza soka kwenye taifa hilo.

Shule hiyo ya Burna Boy, inayowalenga wavulana wenye umri wa miaka 4-16, imeweka vituo vya mafunzo huko Lagos, Abuja, na Port Harcourt.

Mbali na hilo Burna amezindua kipindi cha televisheni kitachohusisha matukio ya ukweli 'reality show' kinachoitwa Burna Boy Football Show, kwa ajili ya wachezaji wenye umri wa miaka 18-21 kuonesha vipaji vyao kwa lengo la kupata fursa kwenye vilabu vikubwa vya Ulaya kama Manchester City na Tottenham Hotspur.

Hii si mara ya kwanza kwa wasanii wa muziki kuwekeza kwenye soka, hata nchini wasanii Nahreel na Aika ambao pia ni wapenzi wanashule ya soka iitwayo Navy Kenzo Academy inayolenga kukuza vipaji vya soka na kuviuza nje katika ligi za ushindani mkubwa.

Nahreel anayeunda kundi la Navy Kenzo na mwenzake Aika, kupitia Academy hiyo wanachukua vijana wadogo wenye vipaji vya kusakata soka na kuwapatia mafunzo ikiwa ni sehemu nyingine ya biashara yao ukiachana na muziki.

Akizungumza na Mwananchi, Nahreel amewahi kusema anaangazia zaidi vipaji vya vijana wadogo kwa sababu ni rahisi kuvikuza na umri wao unatoa fursa kuja kuwa wachezaji wakubwa ndani na kimataifa baadaye.

“Lengo ni kuandaa wachezaji kuja kuwa ‘professional players’ kucheza nje ya nchi na ndani, ndiyo maana unakuta tunachukua vijana hadi chini ya umri wa miaka 17 ili niweza kuwapelekea sehemu maana umri wa miaka 17, 16 wanauzika kirahisi,” alisema.

“Pia nipo na watoto wa miaka 13  hadi 17, muda mwingine nina vijana wawili watatu wa miaka 19 siyo mbaya, lakini  13  hadi 17 ndiyo ninao wengi,” alisema Nahreel.

Ikumbukwe mwaka juzi kupitia Academy hiyo walianzisha mashindano, Navy Kenzo Cup 2021 U15 ukiwa ni mwendelezo mara baada ya mwaka 2018 kupitia Navy Kenzo Foundation kuandaa mashindano mengine, Navy Kenzo Cup.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags