Bodi ya filamu yashauri waigizaji kutengeneza maudhui ya kuelimisha

Bodi ya filamu yashauri waigizaji kutengeneza maudhui ya kuelimisha

Sute Kamwelwe

Dar es Salaam. Waigizaji na makampuni ya kuzalisha filamu yametakiwa kutengeneza maudhui kama afya, historia, elimu, utamaduni huku wakishauriwa kutojikita zaidi kwenye maudhui ya mapenzi.

Hata hivyo wameshauriwa wasiache maudhui ya mapenzi lakini waangalie na mawazo mengine, wapunguze eneo moja na waongeze nguvu katika maeneo mengine yenye fursa zaidi.

Rai hiyo imetolewa na Ofisa Maendeleo ya Filamu kutoka Bodi ya Filamu Tanzania, Clarence Venance wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 6, 2024 jijini Dar es Salaam.

Rai hiyo inakwenda sambamba na pongezi kwa kampuni ya Allan Cultural Group kwa kuja na mpango wa kutoa elimu kupitia njia ya filamu ya ‘Pigo’ yenye maudhui ya elimu ya saratani ya shingo ya kizazi.

“Kama Serikali tunatoa wito kwa kampuni na watu wengine kuja na mawazo kama haya ya kutoa elimu kwa njia ya filamu kufikisha ujumbe kwa jamii kwani changamoto ziko nyingi ambapo filamu inaweza kutumika kuelimisha,” amesema.

“Watu na kampuni nyingine zisijikite kwenye filamu za maudhui ya aina moja kama mapenzi tunajua watu wanapenda lakini waangalie kwenye afya au uchumi na mambo mengine,” amesisitiza.

Aidha katika hatua nyingine amesema bodi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo ya maandalizi ya filamu ili kufanya vizuri sokoni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Allan Cultural Group, Mwahija Mungi amesema filamu hiyo ya Pigo inahusiana na masuala ya saratani ya shingo ya kizazi.

“Filamu hiyo inatoa elimu kwenye jamii yetu kwani imekuwa pigo hivyo tunajitahidi kutoa elimu kwakuwa tumeguswa kuweza kuisaidia jamii,” amesema Mungi.

Amesema uzidunduzi utafanyika Desemba 5 hadi 7 mwaka huu na Waziri wa Afya. Ameongeza kwamba filamu itainesha athari za ugonjwa huo kiafya, kijamii na kiuchumi.

“Tatizo la Saratani limepoteza baadhi ya wapendwa wangu ndani familia. Watu wakipata huu ugonjwa wengine wanakimbilia kwa waganga. Niklatamani kujua unasababishwa nanini, baada ya kufahamu ndipo nikawiwa kuielimisha na jamii nzima kupitia filamu hii,” amebainisha.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags