Ikiwa siku kadhaa zimepita tangu mwanamuziki wa Nigeria Ayra Starr, kudaiwa kusainiwa chini ya lebo ya Jay Z Roc Nation. Hatimaye kitengo cha michezo kwenye kampuni hiyo Roc Nation Sports International (RNSI), kimesaini wachezaji wanane chipukizi wa soka kutoka nchi sita Afrika.
Hawa si wachezaji wa kwanza kutoka Afrika kusainiwa na wakala Emile Witbooi, kutoka kwenye kampuni hiyo kwani winga wa Cape Town City mwenye umri wa miaka 17, alifanikiwa kusainiwa mapema mwaka huu.
Usajili huu wa karibuni unaonyesha kuwa kampuni hiyo ya kimataifa imekusudia kuwekeza barani Afrika.
“Tunaamini Afrika ni hazina ya vipaji vya soka ambavyo bado havijagunduliwa, na upanuzi wetu hapa ni hatua katika kutimiza dira yetu ya kimataifa,” alisema Nathan Campbell, Mkuu wa Usajili wa Kimataifa wa Kandanda kutoka RNSI, kupitia taarifa rasmi iliyotolewa.
“Mkakati wetu umejengwa juu ya ushirikiano wa kina na wadau wa ndani, jambo ambalo linatuwezesha kuelewa na kukidhi mahitaji ya kipekee ya wachezaji wa Kiafrika, na kuwahakikishia msaada bora zaidi ili kufikia uwezo wao wa juu kabisa.”
Hatua ya Roc Nation kuingia katika soka la Afrika haikuwa ya kushangaza. Kwani 2021 kampuni hiyo iliingia kwenye makubaliano na klabu ya Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns ushirikiano ambao bado unaendelea hadi leo.
Nchi sita za Kiafrika zinawakilishwa kati ya hao wachezaji wanane waliosainiwa ni mshambuliaji wa Kaizer Chiefs Neo Bohloko (Afrika Kusini) na kiungo wa Benab FC, Joseph Narbi (Ghana), hadi mshambuliaji wa Al Nasr Mamadou Diallo (Guinea) na winga wa Sibonor United Francis Gomez (Gambia).
Wengine ni Ifeoluwa Olowoporoku (Nigeria), Tadiwa Chakuchichi (Zimbabwe), Siyabonga Mabena (Afrika Kusini), na Ali Umar (Ghana). Wachezaji wote, isipokuwa wawili wa mwisho (wenye umri wa miaka 18), wana umri kati ya miaka 16 na 17.
Mbali na sekta hiyo ya michezo wasanii wa muziki walio chini ya Roc Nation ni pamoja na Rihanna, Alicia Keys, na J Balvin.

Leave a Reply