Msanii wa vichekesho na mtayarishaji, AbdulMohamed 'Selengo' licha ya kuwachekesha wengine ni mtu ambaye uso wake unatawaliwa na machozi pindi anapozungumzia kitu kinachougusa moyo wake.
Katika mahojiano yake na Mwananchi, Selengo kuna wakati machozi yalikuwa yanambubujika alipokuwa akisimulia tukio lililogusa moyo wake, ingawa kuna muda alikuwa anacheka na kuchekesha.
Kati ya vitu ambavyo anavizungumzia ni neno kioo, linalotumika kwa watu maarufu kufanyika mfano wa kuigwa katika jamii inayowazunguka namna linavyoweza kuwanyima haki kama binadamu wanaoweza kukosea kama wengine.
"Jamii ya aina yoyote unapojulikana inakuwa imekutengenezea picha ya maisha fulani, inapotokea ukafanya tukio la kushangaza hawakuchukulii kama binadamu unayeweza kukosea, badala yake unaonekana ni mtu wa ajabu na heshima inaweza ikashuka kabisa, hivyo neno kioo cha jamii linatufanya kuishi maisha kwa uangalifu mkubwa," anasema Selengo anayekiri tamthilia ya Huba kumwongezea mashabiki na ushindani wa kazi.
Komedi kwa sasa
Anasema wasanii wa komedi wa sasa wana ubunifu na wanafanya kazi nzuri, kulingana na nyakati za sayansi na teknolojia zinazowasaidia wepesi wa kufikisha ujumbe wao kwa jamii.
"Pamoja na hilo bado hawajafikiwa kiwango cha ubora, kilichofanywa na wakongwe ambao kazi zao zinaishi hadi sasa kama marehemu mzee Majuto, kitu ninachoweza kuwashauri wafanye komedi za muda mfupi na ambazo zitaishi," anasema na kuongeza;
"Jambo lingine wapofanya komedi maudhui ya kazi zao yasiwe ya matusi, kwa sababu zinaangaliwa na watu wazima, vijana na watoto wadogo ambao hawawezi kuchambua baya na zuri, hivyo lazima tulilinde taifa kwa kuandaa viongozi walio na misingi ya nidhamu."
Teknolojia
Anazungumzia teknolojia namna ilivyowarahisishia kufanya kazi zao, tofauti na zamani ambapo hadi jamii ielewe kontenti waliyokuwa wanaifanya, ulitumika ubunifu mkubwa na ushawishi wa kutosha.
"Kwa sasa mtu anaweza akatumia simu kurekodi vichekesho na akaviachia na jamii inapokea vizuri, hivyo teknolojia imepanua wigo wa kila mtu kukionyesha kipaji chake," anasema na kuongeza;
"Mfano sisi tulipitia Kaole Sanaa Group Tanzania, ambako tulifundishwa na hadi itokee umepata nafasi ya kufanya kazi, ujue umeiva kweli kweli ila kwa sasa mtu anaweza akawaza kitu akakirekodi na kukituma mitandaoni na jamii ikakipokea na kukipenda."
Kanumba
Anasimulia jinsi kifo cha aliyekuwa msanii na mtunzi wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba kilivyomwachia kovu na upweke, wakati mwingine anatamani kuachana na sanaa kabisa.
"Kanumba kaniachia unyonge na hali ya kutokutamani kuendelea na fani, nakumbuka namna ambavyo alikuwa na ushirikiano mkubwa, upendo wa kutamani wengine wafanikiwe, jambo ambalo silipati kwa sasa, pamoja na hayo yote napambana na kujipa moyo na mimi niwasaidie chipukizi," anasema na kuongeza;
"Pia kifo cha Kanumba kimenipa somo kubwa la kuishi na watu vizuri, nikijua uhai ni mali ya Mungu anaweza akauchukua muda anaoutaka."
Mtego wa Umaarufu
Anakiri watu maarufu ni ngumu kupata upendo sahihi kwa watu wanaomzunguka asilimia kubwa wengi wao wapo kwa ajili ya mafanikio yanapoondoka wanapotea.
"Ngumu kupata upendo wa dhati ukitaka kuamini hilo wakipata walichokifuata kwako wanaondoka, niliwahi kuumizwa kimapenzi kwa kumpenda mdada niliyemfanyia kila kitu kinachotakiwa katika mahusiano mwisho wa siku akaniacha bila sababu za msingi," anasema na kuongeza;
"Nilichojifunza katika maisha ya mahusiano siyo kuangalia vitu vya kimwonekano bali ni kutafuta amani ya kweli ya kufurahia maisha mafupi ya hapa duniani."
Mbali na hilo anawazungumzia wasanii Muhogo Mchungu ambaye katika tamthilia ya Huba anajulikana kama Kashaulo, Ben Kinyaiya, Nicole kwamba nyuma ya pazia ni watu wacheshi waliyo na upendo na nidhamu dhidi ya wengine.
"Uhusika wa mtu katika kazi haumaanishi ndiyo uhalisia wao wa maisha, mfano mzuri hao wasanii unapokaa nao lazima utacheka, washauri wazuri na wenye upendo na kila mtu, hivyo anavyoigiza Ben ni mkorofi jamaa hayupo hivyo kabisa," anasema.
Maisha ya kazini (Location)
Anasema wanapokuwa kazini wanakutana watu wenye tabia tofauti.
"Kuna changamoto ambazo ni kudhibiti tabia ili wote muwe sawa asiwepo anayejiona staa dhidi ya mwingine, uzuri wake ni kubadilishana mawazo na kuingiza vitu vipya kichwani, kupata koneksheni ya kufanya vitu vingine nje na sanaa,"anasema.

Leave a Reply