Sauti za Busara 2025 ilivyotumika kupigania amani ya dunia

Sauti za Busara 2025 ilivyotumika kupigania amani ya dunia

Tamasha la Muziki la Sauti za Busara la 22, lililoanza Februari 14,2025, hatimaye limetamatika leo Februari 16, 2025 kwa burudani ya kusisimua kutoka kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi kama vile Zenji Boy, Blinky Bill, Thandiswa na wengineo.

Tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu lililenga kupaza sauti kwa ajili ya kuleta amani duniani kupitia muziki limefanikiwa kuzileta pamoja sauti za wasanii kutoka mataifa mbalimbali.

Ujumbe huo unakuja wakati dunia na Afrika ikishuhudia machafuko katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo ambako waasi wa M23 wanaendeleza mapigano huku wakitwaa baadhi ya miji ya nchi hiyo.

Kaulimbiu hiyo ya tamasha hilo la kimataifa ilitolewa Februari 14,2025 na Mtendaji Mkuu wa tamasha hilo, Journey Ramadhan akifanya ufunguzi wake.

"Nina ujumbe mdogo kuhusu kwanini tuliamua kuchagua kauli mbiu hii kwa mwaka huu. Katika dunia ambayo migogoro inatisha. Kila mmoja wetu ana nguvu ya kuwa sauti ya amani.

"Tumeshuhudia migogoro mingi Afrika, kama ninavyosema. Tuache muziki uzungumze kwa sababu sauti za amani zinanza leo hadi tarehe 16 Februari,"alisema Journey wakati akifungua tamasha.

Naye Zakia Lulu ambaye ni Meneja Masoko wa Sauti za Busara amesema furaha yake kubwa katika tamasha la 2025 ni kuona watu wote wameungana wakitaka amani

"Kila bendi jukwaani inatumbuiza, na kila wakati wanaposema 'Voices for Peace' au wanapozungumzia jambo lolote linalohusiana na amani. Ninyi nyote mnaungana. Yaani, naona tuko pamoja kwenye kutaka amani. Furaha yangu tumeungana na kukubali kupaza sauti kwa ajili ya amani,"alisema Zakia

Katika mandhari ya kuvutia ya Zanzibar, baadhi ya wasanii kama Frida Amani, Ukhoikhoi walitumbuiza siku ya kwanza ya tamasha hilo.

Aidha siku ya pili ya tamasha lilifunguliwa na Mwenyekiti wa Board ya Sauti za Busara, Simai Mohammed Said, kwa wimbo wa uitwao Afrika ulioimbwa na Salif Keita (Mali). Ukiwa umebeba maudhui ya upendo, umoja, na kujivunia urithi wa bara la Afrika.

Haikuishia hapo baadhi ya wasanii waliopanda jukwaani kwa siku hiyo ni Baba Khas (Tanzania), Ukhoikhoi (Afrika Kusini), Mumba Yachi (Congo). Ambapo naye Christian Bella aliifunga siku hiyo kwa kuwapa vibe mashabiki kwa kutumbuiza ngoma zake kama vile 'Nani kama Mama', Subira na nyinginezo.

Mbali na siku hizo zote mbili ambazo mashabiki walijaza uwanja na kucheza kwa furaha. Tamasha hilo lilitamatishwa leo Februari 16, 2025 kwa sauti za wakali kutoka mataifa mbalimbali kama Zenji Boy, Blinky Bill (Kenya) na kufungwa na msanii wa Afrika Kusini Thandiswa

Hivyo basi jukwaa la Sauti za Busara lilipambwa na wakali kama vile Thandiswa (Afrika Kusini), Blinky Bill (Kenya), Christian Bella & Malaika Band (Tanzania). Bokani Dyer (Afrika Kusini), The Zawose Queens (TZ/UK).

Kasiva Mutua (Kenya), Zanzibar Taarab Heritage Ensemble (Zanzibar), Leo Mkanyia & Swahili Blues (Tanzania), Boukouru (Rwanda), Tryphon Evarist (Zanzibar), Charles Obina (Uganda), Baba Kash (Tanzania).

Frida Amani (Tanzania), Assa Matusse (Msumbiji), Mumba Yachi (Congo), Nidhal Yahyaoui (Tunisia), Étinsel Maloya (Reunion), WD Abo (Sudan), B.Junior (Mayotte), uKhoiKhoi (Afrika Kusini), na Joyce Babatunde (Kamerun)

Walichosema wasanii

Akizungumza na Mwananchi, mwanamuziki wa singeli Baba Kash alisema ni mara yake ya kwanza kupanda kwenye jukwaa hilo. Lakini mapokeo ya mashabiki yalikuwa makubwa tofauti na alivyotegemea.

"Mimi mwanzoni nilikuwa naimba na Dj, lakini nikaona hapana. Nikaanza kutengeneza ladha ya Singeli, Mchiriku na Mnanda kwa pamoja nikiwa napiga bendi. Nimefanikiwa katika hilo ndiyo maana nimepata nafasi ya kutumbuiza Sauti za Busara 2025, hii ni mara ya kwanza lakini imekuwa poa sana,"anasema.

Naye msanii wa Congo Christian Bella alisema ni zaidi ya mara mbili anashiriki jukwaa hilo. Lakini mapokezi na jukwaa la mwaka huu lipo tofautii

"Jukwaa lipo vizuri sana, mashabiki wana nguvu ya kutosha lakini kikubwa ni dhima ya mwaka huu kupaza sauti kwa ajili ya amani. Wasanii tunaweza kutumia nyimbo zetu kufikisha ujumbe na kupinga machafuko,"anasema

Aidha msanii wa Kenya Blinky Bill alisema katika uzoefu wake wa miaka miwili ya tamasha hilo, mwaka huu umekuwa wa tofauti kwani amekutana na hadhira yenye vibe zaidi.

"Mimi siyo mara ya kwaza lakini hakuna kitu kizuri kama kutumbuiza na mashabiki ukaona wanaitikia hata kama hawaelewi kinachoimbwa. Hicho ndicho kitu ninachotaka, naona Sauti za Busara inaendelea kukuza muziki wa Afrika,"anasema

Aidha Frida Amani ambaye ameingia katika historia ya kuwa msanii wa kwanza wa kike wa Tanzania kutumbuiza kwenye tamasha hilo amesema, muziki ni kitu muhimu kinachoweza kuwaunganisha watu pamoja.

"Wasanii tutumie nyimbo zetu kuhamasisha amani duniani kote, lakini hii ni mara yangu ya kwanza Sauti za Busara. Mwitikio wa mashabiki ulikuwa mzuri sana,"anasema

Wanachosema Wadau wa muziki

Akizungumza na Mwananchi Said Salim kutoka Dar es Salaam amesema tamasha la mwaka huu limekuwa tofauti na miaka mingine ambayo amekuwa akihudhuria

"Nimekuwa nikihudhuria mara kwa mara na hili ni kama la sita wangu, niseme ukweli sijajutia pesa yangu ya kiingilio. Yaani naona nimeitoa kihalali, kila kitu kilikuwa poa kuanzia orodha ya wasanii hadi muziki ulivyokuwa unasikika,"anasema Said

Naye Pili Sande wa Michenzani kisiwani hapo anasema kwake siyo tu tamasha bali ni njia ya kukutana na watu wapya.

Najifunza vitu vingi Kupitia tamasha la sauti za busara, lakini pia nakutana na watu wapya ambao wao wananipa uzoefu ambao sikuwa nao. Walichokilenga mwaka huu ni amani mimi ushauri wangu duniani tudumishe amani.

Akimalizia Michel Tyson wa Italy anasema Sauti za Busara imemfanya asikie midundo mbalimbali ya muziki ambayo hakuwahi kuisikia.

“Kuna miziki sikuwahi kuisikia nikiwa nyumbani kwetu, lakini Tanzania Kupitia Sauti za Busara nimesikia. Hii ni mara yangu ya kwanza nimekuja kutazamwa tamasha hili, matarajio yangu nitaendelea kuja kila mwaka,” anamalizia






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags