Tasnia ya uchekeshaji imeendelea kuwa miongoni mwa zinazofanya vizuri kwenye kiwanda cha burudani Bongo kutokana na kubeba majina ya vijana wengi wanaojihusisha na kazi hiyo ili kujitafutia ugali wao wa kila siku. Ukweli ni kwamba wamekuwa wakipata mafanikio.
Kwa mwaka 2024 wapo wachekeshaji wengi ambao wamefanya vizuri kwenye kazi zao lakini huwezi acha kutaja jina la Jol Master kama mmoja wa vijana wanaofanya kazi hiyo kwa viwango na kwa malengo makubwa.
Jol Master amefanikiwa kujiwekea viwango vyake madhubuti kwenye kazi na mtindo wake wa maisha kwa ujumla, kwa lugha nyepesi ametengeneza Brand yake kwa kujitofautisha thamani yake na Comedian wengine.
Mfano mwaka jana alitangaza hafanyi shoo chini ya shilingi milioni 10 kitu ambacho kiliibua vioja midomoni kwa watu wengi lakini pia alipunguza kuonekana sana hadharani kitu ambacho Mwananchi Scoop iliamua kubonga naye ili kufahamu yaliyo nyuma ya pazia.
"Unajua kila mtu ana maisha yake ambayo amejipangia, mimi tu nimechagua maisha fulani ya kutokuwepo kila mahali na hiyo nilifundishwa na kaka yangu Joti kuwa hutakiwi kuwepo kila mahali, ukifanya hivyo inakuongezea thamani" amesema Jol Master.
Hata hivyo, Jol Master ameongeza kuwa hali hiyo imempa nafasi ya kujitathmini zaidi yeye binafsi na kupitia baadhi ya kazi zake kuangalia nini aongeze na nini apunguze ili awe bora zaidi.
"Imenitengenezea mazingira ya kujitathimini na kujua nakosea wapi, unajua ukiwa na ratiba nyingi labda za kutoka na washikaji unakosa muda wa kufahamu mambo yako binafsi yanayokuhusu lakini imenipa thamani zaidi," amesema Jol Master.
Machi 27, 2024, Jol Master alifanya shoo yake ya kwanza ya Zeguy aliyoiandaa mwenyewe ikifanyika Mlimani City, Dar Es Salaam na ameeleza kuwa hii ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu kufanya hivyo siku moja na amefanikiwa kuitimiza mwaka huo.
"Ilikuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu sana kufanya shoo yangu ya kwanza Mlimani City na ilinitia moyo sana, nilisema kama nimeweza kujaza hapa basi hakuna kinachoshindikana, ninaweza kufanya chochote na kikawezekana, ni suala la muda tu kwa sababu wazo nilipata tangu 2022 lakini nimekuja kufanikisha 2024 maana yake ni kwamba kipindi chote hicho nilikuwa najisuka vizuri na nikakubali muda uongee, mwisho wa siku ukaongea," amesema Jol Master.
Watu wengi walimfahamu Jol Master kupitia jukwaa la Cheka Tu ambalo limebeba majina ya wachekashaji wakubwa Tanzania, lakini baadaye Jol Master alijiengua na kuanza kujitegemea akianzisha shoo yake ya Zeguy mwaka 2024, ambayo imekuwa ni miongoni mwa shoo kubwa za uchekeshaji.
Jol Master amenyoosha maelezo kuwa wazo la Zeguy alilipata mwaka 2022 wakati anafanya Cheka Tu lakini alishindwa kuifanya kwa kuhofia kuingiliana kwa maudhui na shoo ya Cheka Tu.
"Wazo nilikuwa nalo toka nipo Cheka Tu lakini sikuweza kufanya pale japo sikukatazwa na mtu lakini niliwaza nikaona jukwaa la Cheka Tu limetengenezwa kwa ajili ya Stand Up Comedy na sio michezo ya jukwaani kama ninayofanya kwenye Zeguy.
"Niliona Cheka Tu sio sehemu sahihi nikasema inabidi nianzishe Zeguy ili mtu akija anapata kitu tofauti," amesema Jol Master.
Hata hivyo, Jol Master ameelezea mapokezi ya Zeguy baada ya kuanzishwa akisema kwa upande wake hapendelei mapokezi makubwa sana wakati kitu kikiwa kinaanza ila anapendelea mapokezi ambayo yanaweza kumjenga kwa namna moja au nyingine.
"Huwa sipendelei mapokezi makubwa sana, nikiwa naanza kufanya kitu napenda watu wanipe ushauri ili mawazo yao yanijenge kwa ajili ya kutengeneza kitu bora zaidi," amesema Jol Master.
Lakini pia Jol Master anajivunia kwa shoo hiyo kuruka Clouds Tv ikiwa ni mojawapo ya shoo kubwa inayoonekana kwenye runinga kila Jumatano kwani imekuwa ikimpa hamasa ya kuendelea kufanya zaidi.
"Kuwa na kipindi cha Tv ambacho ni cha kwangu hayo ni mafanikio makubwa sana nimeyapata kwa mwaka huu kwa sababu ni kitu ambacho nimekiwaza kwa muda mrefu, sasa kukubaliwa tu kwenye Tv najivunia sana," amesema Jol Master.
Jol Master amemaliza kwa kusema wachekeshaji wengi wanashindwa kuanzisha shoo zao kutokana na uwoga wa kujitegemea kwa sababu shoo yako mwenyewe lazima uwajibike kuisimamisha ili iwe juu zaidi.
"Wengi tunaogopa kufanya maamuzi ya kukua, mtu ukiwaza kuanzisha kitu chako mwenyewe unaona kabisa kila kitu kitakutegemea wewe lakini pia ukianzisha shoo watu wasipokuja utakabiliana nalo vipi hilo, kwa hiyo kikubwa ni uthubutu tu, basi," amemaliza Jol Master.
Leave a Reply