Peter Akaro
Mkali wa Afrobeats kutokea Nigeria, Davido amefunguka kuhusu nguvu kubwa ya ushawishi aliyonayo mkewe Chioma katika maisha yake binafsi na kazi yake ya muziki na kusema mambo huwa hayaendi sawa pindi wanapotofautiana.
Davido aliyevuma na wimbo wake, Unavailable (2023) uliowania Grammy, amesema Chioma ni nguzo muhimu katika safari ya mafanikio yake kabla hata hawajafungua ndoa iliyogeua gumzo Afrika Juni mwaka uliopita.
Utakumbuka Davido alianza muziki katika kundi la KB International nchini Marekani, alipata umaarufu alipoachia wimbo wake, Dami Duro (2011) ambao ulijumuishwa katika albamu yake ya kwanza, Omo Baba Olowo (2012) chini ya HKN Music.
Katika mahojiano na The Breakfast Club hivi karibuni, Bosi huyo wa DMW (Davido Music Worldwide) alisema mke wake kwa nyakati zote amekuwa akimuunga mkono tangu walipokuwa vijana wadogo na hilo limetengeneza jambo la kipekee kwake.
"Kwa kila mara ninapogombana au kutofuatiana naye, basi kuna kitu kibaya kitatokea katika biashara yangu ya muziki. Huwa anasema 'unapigana na mimi wakati una mpango wa kutoa albamu?, acha tuone!'. Hivyo ana hiyo neema juu yangu," alisema Davido.
Akikumbushia kuhusu uhusiano wao wa muda mrefu, Davido alifichua kwamba walikutana wakiwa shule, wakati huo wakiwa na umri wa kati ya miaka 18 na 17, na wamekuwa pamoja kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.
Ukaribu wao ulibadilika kutoka urafiki hadi kuwa uhusiano wa kimapenzi na sasa ndoa huku akigusia jinsi ambavyo Chioma amekuwa akiishi na watoto wake aliyowapata katika uhusiano mwingine.
"Watoto wangu wanampenda sana Chioma, hasa binti yangu Hailey. Kuna nyakati niliogopa kuwaleta watoto wangu wakae karibu naye, lakini amekuwa akiishi nao vizuri tu," alisema Davido aliyetikisa zaidi na wimbo wake, Fall (2017).
Katika hatua nyingine, Davido alizungumzia kwa hisia tukio la kufiwa na binti yake wa kwanza, Ifeanyi ambaye aliaga dunia hapo Oktoba 2022 baada ya kuzama katika bwawa la kuogelea nyumbani kwake.
Alisema tukio hilo ni moja ya nyakati ngumu zaidi kuwahi kupitia maishani mwake na kuishukuru familia yake kwa kumsaidia kuweza kusonga mbele, na sasa anafurahi kuwa baba wa watoto pacha waliozaliwa na Chioma mnamo Oktoba 2023.
"Kwa sasa tuna watoto pacha, huyo wa kiume amefafana kabisa na binti yangu [Ifeanyi] aliyefariki. Matendo yao yanafana, kila kitu alichokuwa akifanya, naye anafanya," Davido alieleza.
Alipoulizwa iwapo kama ana michepuko nje ya ndoa yake, Davido alisema hataki matatizo kwani ameamua kutomsaliti mke wake tena na hana mpango wa kuoa mke mwingine kama ulivyo utamaduni wa wanaume wengi Nigeria hasa wale wanaojiweza kiuchumi.

Leave a Reply