Mkurugenzi wa Kampuni ya Look inayoendesha mashindano ya kumsaka Miss Tanzania, Basila Mwanukuzi amesema Miss Tanzania 2023, Tracy Nabukeera hajajitoa kushiriki Miss World 2025 kwani sio yeye aliyekuwa amepangwa kwenda kushiriki.
Leo Aprili 14, 2025 Basila ameiambia Mwananchi kwamba mwaka 2024 Tracy aliwaandikia barua ya kudai anapitia changamoto binafsi.
“Trace haja ‘withdraw’ (hajajitoa) kwa sababu tayari organization (taasisi) ilipanga haitampeleka kushiriki Miss World kwa sababu mwaka jana alituandikia barua kuwa anapitia changamoto binafsi. Kwa hiyo tulikuwa tunamlinda hatukutaka kutangaza kuwaambia watu kuwa anapitia changamoto.
“Itoshe tu kusema hajajitoa kwa sababu alikuwa haendi kutokana na hizo changamoto alizosema anazipitia na alishukuru kwa sapoti na nafasi aliyopata kama Miss Tanzania. Sisi hatukutaka kumbebesha lawama, tulimpa muda kwa sababu alikuwa anapitia namna ya kutatua changamoto yake,” amesema Basila.
Basila ameongezea kwa upande wao hawakuwa na wasiwasi kwa sababu walikuwa wakijiandaa kupeleka mrembo mwaka ujao.
“Miss World ilikuwa inasuasua kutokana na wao wanajua wanayopitia huku wamekuwa wakiahirisha mashindano. Na kwa sababu Tracy hiyo 2023 mpaka 2024 alikuwa amemaliza majukumu yake hata kama Miss Tanzania ingefanyika 2024 ina maana Miss Wolrd siyo lazima kwenda yeye ilikuwa ni sisi organization kuamua nani aende,” amesema na kuongezea.
“Miezi miwili imepita tangu Miss World imetuandikia barua kuwa wanafanya mashindano Mei na sisi tupo kwenye mchakato wa kufanya fainali Agosti kwa hiyo mwaka huu kama taifa hatutashiriki.
“Yeye Tracy kuandika hivyo ni sehemu ya changamoto anayopitia, siyo ishu kubwa, hiyo kukosa ushirikiano siyo taarifa za kweli na zinadhihirisha hayo matatizo anayopitia,” amesema.
Utakumbuka hayo yote ni baada ya Miss Tanzania 2023, Tracy kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa hatoweza kushiriki Miss World 2025 kutokana na kukosa sapoti.
“Baada ya kufikiria na kutafakari kwa kina, nimefanya uamuzi wa kutoshiriki Miss World
2025. Hili halikuwa chaguo rahisi, lakini kutokana na kukosa usaidizi, mawasiliano sahihi, na maandalizi ya kutosha kutoka kwa shirika linalohusika. Sikujiona tena kuwa na uhusiano au uwezo wa kutosha kuiwakilisha Tanzania katika hatua hiyo ya kimataifa,” ameandika Tracy kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Hata hivyo baada ya Mwananchi kumtafuta Dk Kedmon Mapana ambaye ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa (Basata) alidai kuwa hana taarifa zozote za kinachoendelea.
“Hiyo taarifa mimi sina na wala sijasikia mahali popote. Mimi Instagram sijui na siwezi kwenda na vitu vya Instagram,” amesema Mapana.

Leave a Reply