Mwanamuziki wa Hip-hop nchini Bando Mc ameweka wazi kuwa wapo mastaa wakubwa ambao waliwahi kumtumia kabla hajajipata katika muziki.
Akizungumza na Mwananchi Scoop amesema alipokuwa akijitafuta alikuwa akifanya challenge nyingi za mastaa wakubwa kwa kigezo cha kumsaidia kimuziki.
“Mastaa ambao walikuwa wakinitumia wapo wengi sana kwa kipindi ambacho nilikuwa najitafuta. Siwezi kuwataja maana ni wengi nishafanya challenge za mastaa wengi, mimi nimetoka kuwa underground kama hawa wa sasa ambao wanafanya challenge, lakini hazikuwahi kunipeleka sehemu yoyote ila ngoma zangu mwenyewe ndio zilinitoa.
"Kwa hiyo najivunia kupitia kazi za mikono yangu nilivyojitambua na kuanza kufanya kazi zangu mwenyewe ndio zimenifikisha hapa nilipo leo, nimekuwa msanii mkubwa naweza nikafanya vitu na Watanzania wakakipokea. Nawaonea huruma sana wasanii ambao bado wako mtaani,"amesema Bando.
Aidha Bando amewataka wasanii chipukizi kutotumika na wasanii wakubwa na badala yake wawekeze nguvu katika kutengeneza kazi zao.
“Nawashauri chipukizi wote wawekeze nguvu zao katika kutengeneza kazi zao hizi maswala ya challenge, sijui nitakuweka kwenye remix halafu mwisho wa siku wasanii wakubwa wanakuja kushirikisha mastaa wenzao.
"Wasanii wakubwa wanapotoa ahadi kwa watu watimize ahadi kwanza ni dhambi kutotimiza ahadi, kama vitu vipo nje ya uwezo wetu tusiwadanganye watu tusiwaambie wafanye bali tuwaombe wao wafanye kwa mapenzi yao,” ameeleza Bando.
Aidha amesema wasanii chipukizi ndiyo wanamuumiza kichwa kwa sasa kwenye gemu.
“Kitu ambacho mimi nakiogopa kwenye tasnia kwa sasa, sio watu waliopo kwa sababu nimeshawasikia kila kitu chao, mbinu wanazotumia katika uandishi na uimbaji wao, chipukizi ambao wako mtaani ndio nawaogopa. Muda mwingi nawasikiliza sana kwa sababu unapokuwa mwandishi mzuri na bora unatakiwa uwe shabiki wa kazi za watu wengine ili uwe noma zaidi.
"Sasa mimi ni shabiki wa wasanii chipukizi lakini kipengele kinakuja wasanii hawa hawapewi thamani thabiti ambayo wanatakiwa wapewe ili kufanikisha ndoto zao,”amemalizia Bando.
Kwa sasa msanii huyo anatamba na wimbo wa ‘Forever’ aliowashirikisha mastaa Roma Mkatoliki na Maua Sama wimbo uliotoka Februari mwaka huu.

Leave a Reply