Athari za kiafya zitokanazo na matumizi ya tumbaku (sigara)

Athari za kiafya zitokanazo na matumizi ya tumbaku (sigara)

Uvutaji wa tumbaku inayotumika kutengeneza sigara ni tabia hatarishi inayoweza kusababisha madhara makubwa kwa mvutaji na watu wa karibu yake wanaovuta moshi anaoutoa.

Licha ya elimu kubwa inayotolewa, bado idadi ya wanaovuta tumbaku na sigara inazidi kuongezeka kila kukicha.

Utafiti wa kitaalamu unaonesha kwamba moshi wa tumbaku una kemikali nyingi zenye sumu ambazo ni hatari kwa mwili wa binadamu na kwa taarifa yako, uvutaji huo huathiri karibu kila kiungo katika mwili wako, kuanzia mapafu, macho, koo, ini, figo, ubongo na vingine vingi.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kila mwaka watu milioni 6 watapoteza maisha kutokana na matumizi ya tumbaku, wakati karibu watu 900,000 wasiotumia watapoteza maisha kutokana na kuvuta hewa yenye moshi wa tumbaku.

Katika taarifa yake iliyotolewa Desemba 31, mwaka jana, WHO ilifafanua kuwa gharama za magonjwa yatokanayo na matumizi ya tumbaku kila mwaka ni dola trilioni 1.4 kote ulimwenguni.

Juni 4, mwaka juzi wakati akizindua Ripoti ya Utafiti wa matumizi ya Tumbaku nchini kwa watu wazima ya mwaka 2018, mjini Dodoma Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliweka wazi kwamba Tanzania kama ilivyo nchi nyingine za Afrika watumiaji wa tumbaku wapo hatarini kupata magonjwa yasiyoambukiza na hata kuyumba kuchumi.

Kutokana na takwimu hizo, Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) nao wanaweka wazi kuwa moshi wa tumbaku una madhara kwa watumiaji na watu waliokaribu na mvutaji kwani una kemikali zaidi ya 400 ambazo 250 zinajulikana kuwa ni hatari na kati ya hizo 50 husababisha ugonjwa wa saratani.

Akizungumza hivi karibuni, Meneja Mradi wa TANCDA, Happy Nchimbi alisema kwa ujumla moshi wa tumbaku unamadhara kwa watumiaji na hata watu waliokaribu na mvutaji ambao watafikiwa na moshi huo.

Alisema tumbaku inapatikana katika matumizi mbalimbali kama sigara, ugolo ambapo kadiri mtu anavyoitumia ndivyo anavyoendelea kuzoea na kutaka kuitumia kila wakati.

“Wakati wa kuanza uvutaji kunakuwa na changamoto nyingi ikiwemo kukohoa, kichwa kuuma, mapigo ya moyo kwenda kwa kasi na kujihisi kuumwa lakini mtu akishazoea inakuwa ngumu kuacha kutokana na kichocheo kilichopo kwenye tumbaku.

"Hapa nchini watu wanaotumia tumbaku huitumia kama sigara, msokoto, kiko, kunusa na kutafuna maarufu kama ugoro. Wanaotumia tumbaku na hata wanaofikiwa na moshi wa wavutaji wako hatarini kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kifua sugu, saratani ya mapafu, koo, kizazi, mifupa na ngozi," alisema na kuongeza

"Madhara mengine ni magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, vidonda vya tumbo, meno kuoza na kupungua nguvu za kiume, nusu ya watumiaji wa tumbaku kwa muda mrefu hufa kutokana na madhara yake, nusu ya vifo hivyo ikiwa ni chini ya miaka 70," alisema

 

Alisema matumizi ya tumbaku kwa mama mjamzito yanaweza kusababisha mimba kuhaharibika au mtoto kuzaliwa na uzito pungufu, kutokuwa vizuri, vifo vya ghafla pamoja na magonjwa ya mapafu na njia za hewa.

Aidha Nchimbi alisema kutokana na watumiaji wa tumbaku kufa mapema, huziacha familia, hasa watoto, katika hali mbaya kiuchumi hivyo kushindwa kumudu gharama nyingine za maisha kama vile afya, chakula, mavazi, malazi na elimu.

"Faida zitakanazo na kutotumia tumbaku ni pamoja na kupunguza uwezekano wa kupata athari za magonjwa yasiyoambukiza niliyoyataja hapo juu na pia kuboresha mzunguko wa damu na upatikanaji wa hewa safi ya oksijeni mwilini. Pia huboresha ufahamu wa ladha na harufu na huondoa hali ya uchovu," alisema

Hata hivyo Nchimbi alisema taarifa ya WHO iliyotolewa hivi karibuni inaonesha kuwa virusi vya corona ambavyo vinasababisha ugonjwa wa homa ya mapafu wa Uviko 19 vinawaathiri zaidi watu ambao wanatumia tumbaku.

Alisema WHO inasema wanaotumia tumbaku mapafu yao yanakuwa dhaifu hivyo wakipata ugonjwa wa Uviko 19 huathirika kwa kiwango kikubwa hivyo kuwa rahisi kuingia katika shida ya upumuaji.

"TANCDA inashauri watu wasiotumia tumbaku kutojaribu hata kidogo kwani ni vigumu kuacha wakishaionja. Hii inatokana na uraibu unaopatikana kutoka kwenye kemikali ya nikotini ambayo huufanya mwili kutojisikia vizuri bila kuupata," alisema na kuongeza.

 

"TANCDA inawashauri pia watumiaji kupata msaada wa kuacha kutoka kwa wataalamu wa afya na ni vizuri kulinda afya za wasiovuta sigara hasa watoto. Tunawashauri wanaovuta kutoitumia ndani ya nyumba, karibu na watu hasa watoto ambao mapafu yao bado yanakua kuepuka kuwaathiri," alisema.

mwishoo






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags