Julai 2020 Umoja wa Mataifa (UN) ilitoa ripoti mpya ambayo ilibaini kwamba ujasiriamali unaweza kuwa suluhu kubwa ya ajira kwa vijana na kusaidia jamii nyingi zisizojiweza.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa mjini New York na idara ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kiuchumi na kijamii (DESA), ilieleza kuondoa vikwazo ambavyo vinawazuia vijana kuwa wajariliamali wenye mafanikio kutachangia kwa kiasi kikubwa kusonesha mbele maendeleo endelevu na kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii.
Ripoti hiyo ya dunia ya vijana kwa mwaka 2020 iliyopewa jina “Ujasiriamali wa kijamii kwa vijana na ajenda 2030” ilitoa wito kwa serikali na wadau wengine wafanyamaamuzi “kuondoa vikwazo kwa ujasiriamali kwa vijana kama vile fursa ya kupata mitaji ya kuanzia ambayo kwa sasa ni adimu na inawazuia vijana wengine kujihusisha katika shughuli mbalimbali zinazoweza kuwaletea faida.”
Iliogeza kuwa mifumo mingi ya ufuatiliaji pia mara nyingi inakuwa kikwazo ama bila kujua inawakosesha vijana wengi kupata fursa za mikopo ya kifedha na huduma zinazohitajika kuanzisha shughuli za ujasiriliamali.
Na uhaba wa fursa za mafunzo, msaada wa kiufundi, mitandao na masoko vimeelezwa na ripoti hiyo kuwa ni sababu zingine zinazowakatisha tamaa vijana kuanzisha miradi.
Arafat Faraji, ni mwanafunzi wa shahada ya sheria Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro mwaka wa nne, ambaye na yeye ana amini ujasiriamali ni moja ya mbinu ya kupambana na tatizo la ajira na umasikini nchini.
Faraji ambaye anajishughulisha na utengezaji wa keki za shughuli mbalimbali pamoja na upishi wa pizza na vyakula vingine vingi anasema ujasiriamali hasa kwa wanafunzi ni muhimu kwani uwafanya kujitegemea na kusaidia wengine.
Anasema yeye ni miongoni mwa wanafunzi wanaofanya biashara hizo akiwa chuoni na aliona ni fursa nzuri kwake kuanza kujifunza ujasiliamali akiwa bado mwanafunzi kama mbinu moja wapo ya kujikomboa na tatizo la ajira na umasikini.
“Hivyo nilivyokua mwaka wa kwanza nilitumia pesa ya kujikimu au boom kufanya mtaji nikanunua baadhi ya mahitaji, pia niliwashirikisha walimu wangu mfano Dk. Salum alinisaidia jiko (oven) ambayo ilikuwa halitumii, nikaanza nayo na mpaka sasa napika cake na pizza.
“Niwaeleze vijana wenye ndoto kwamba sikujifunza kwa mtu nilipendelea sana kusoma mtandaoni hivyo nilijifunza vitu vingi kupitia Youtube, Instagram, Google, Pinterest na Tiktok, mitandao hii ya kijamii ilinifunza vema na kuniongezea ujuzi wa kutosha,” amsema Faraji na kuongeza
“Nawashauri vijana wenzangu wasibweteke hasa wakiwa chuoni, fursa za kujiajiri uanzia chuoni, sasa hivi ni wakati wao mzuri wa kuamka na kujishughulisha na ujasiliamali ili kuepuka janga kubwa la kusubiri ajira ambazo hatuna uhakika nazo,” anasema
Faida alizopata kupitia biashara yake
Faraji anasema moja ya faida aliyoipata kupitia kazi yake hiyo ni kuweza kumudu kulipa kodi ya nyumba anayoishi, kununua mahitaji yake muhimu, kusaidia baadhi ya vitu nyumbani pamoja na masomo.
“Faida zipo nyingi ila kubwa naweza kujikimu mahitaji yangu muhimu ya maisha kama chakula, mavazi na vitu vingine bila msaada wa wazazi wala ndugu, pia nasaidia wadogo zangu kama sasa mdogo wangu ninaye hapa chuoni namgharamikia kila kitu.
“Pia nimepata kujuana na watu wengi wapishi, wateja ambao wananisaidia kwa namna moja au nyengine. Nirudie tena jamani najilipia kodi ya nyumba na kumudu gharama zingine za masomo yangu,” anasema Faraji
Changamoto
Anasema moja ya changamoto kubwa anayokumbana nayo ni kukosa sehemu rasmi ya kufanyia shughuli zake kwani anapikia kwenye chumba chake alichopanga ambacho ni kidogo hakikidhi mahitaji.
“Pia ipo changamoto ya uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi zangu kama vile majiko makubwa na mixer au mashine ya kuchanganyia cake na kukandia unga wa pizza, jiko nililonalo ni dogo ambalo napika cake mbili tu kwa mara moja pia nakanda unga kwa mkono na kusaga keki kwa mashine ndogo ya mkono (handmixer) ambazo zinanipatia shida pale ninapokua na order nyingi za watu hivyo kushindwa kumaliza kwa wakati,” anasema.
Ameongezea kwa kusema changamoto nyingine anayokumbana nayo ni mtaji wake ni mdogo hali inayosababisha anashindwa kufikia watu wengi.
Kitu kingine anachopenda
Anasema anapenda zaidi kusoma vitabu, kuangalia filamu, kusikiliza muziki pamoja na kusafiri kutoa mkoa fulani kwenda mwingine.
Anachokitamani
Faraji anasema anatamani kufika mbali zaidi na kuongeza kuwa anazo ndoto za kufanya kazi UN kama marehemu Dk. Mwele Malecela, Dk. Asha Rose Migiro, John Guteres na wengine wengi.
“Pia natamani kuja kuwa na bakery kubwa itayotoa huduma zote za vyakula na vitafunwa mbalimbali hapa nchini,” anasema
Amesisitiza kuwa anatamani kuwa kama hao aliyowataja kwani wamekua ngao muhimu ya kuiunganisha nchi yao na mataifa mengine katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
“Kupitia wao nimejifunza kufanya kazi kwa bidii na hodari, kutokata tamaa kwani wametoka katika familia za kawaida na kwa jitihada zao wakafika kimataifa, nami hiyo ni ndoto yangu kuona naendeleza mema yao na kuwa zaidi ya wao,” anasema
Leave a Reply