Zuchu ajifunze kwa Yemi Alade

Zuchu ajifunze kwa Yemi Alade

Na Peter Akaro

Tangu mwaka 2022 nyimbo zote za Zuchu zinazotoka ni kete muhimu katika mapambano yake ya kuepuka mtego uliomnasa staa wa Nigeria, Yemi Alade kwenye muziki kwa miaka zaidi ya mitano sasa licha ya jitihada zake za kila mwaka za kujinasua.

Katika hili Zuchu ana kibarua kizito kwa sababu Yemi Alade ana uzoefu mkubwa kwenye muziki kuliko yeye, mathalani alikuwa Jaji wake katika shindano la Tecno Own The Stage 2015 ila mtego huo umemnasa. Vipi kuhusu yeye?.

Utakumbuka Zuchu alitoka rasmi kimuziki mwaka 2020 baada ya kutambulishwa na WCB Wasafi akiwa ni msanii wa pili wa kike na wa saba katika lebo hiyo baada ya Harmonize, Rayvanny, Queen Darleen, Rich Mavoko, Lala Lava na Mbosso.

Miaka yake minne ndani ya Bongo Fleva ametoa nyimbo nyingi ambazo zimefanya vizuri ila wimbo wake, Sukari (2021) ndiyo umetikisa zaidi, mfano video yake ndio iliyotazamwa zaidi YouTube Afrika mwaka 2021.

Video hiyo imebakiza hatua chache kufikisha ‘views’ milioni 100 YouTube ambapo sasa ina milioni 99.8, hivyo inaenda kuandika rekodi kama video ya kwanza ya msanii wa kike kutoka Tanzania na Afrika Mashariki kufikisha ‘views’ milioni 100.

Pia itakuwa video ya kwanza ya msanii solo kufikia mafanikio hayo kwa Tanzania maana video zote nchini zilizofanya hivyo, ni zile ambazo wasanii wameshirikiana ila Zuchu anaenda kuweka rekodi hiyo peke yake.

Hadi sasa video za Bongo Fleva zenye ‘views’ zaidi ya milioni 100 YouTube ni Yope Remix (2019) - Diamond Platnumz ft. Innoss’B, Inama (2019) - Diamond ft. Fally Ipupa, Waah! (2020) - Diamond ft. Koffi Olomide, na Kwangwaru (2018) - Harmonize ft. Diamond.

Lakini Zuchu anapokwenda kuweka rekodi hiyo, pia anaenda kujiingiza katika mtego kwa maana kwamba anatakiwa kupambana zaidi ili kupata wimbo mwingine ambao utafanya vizuri hadi kufikia namba hizo za Sukari.

Huu ndiyo mtego uliomnasa Yemi Alade, tangu video yake, Johnny (2014) kufikisha ‘views’ milioni 100 YouTube hapo Januari 2019 na kuandika rekodi kama msanii wa kwanza wa kike Afrika kufanya hivyo, hadi leo hajaweza kuwa na wimbo uliopata namba hizo.

Video ya Johnny ambayo sasa ina ‘views’ milioni 162, inafuatiwa na ya wimbo, Bum Bum (2018) yenye ‘views’ milioni 50 ikiwa haijafikia hata nusu ya Johnny, hivyo ni wazi Yemi Alade ana kazi kubwa ya kufanya.

Machi 4 mwaka huu, Yemi Alade aliadhimisha miaka 10 ya video yake, Johnny (2014), kupitia Instagram alisema tangu kuachiwa kwa kazi hiyo maisha yake yalibadilika kwenye kila kitu jambo ambalo anashukuru.

Kwa upande wake Zuchu, baada ya Sukari, video yake nyingine iliyotazamwa zaidi YouTube ni ya wimbo, Kwikwi (2022) yenye ‘views’ milioni 48 ikiwa ni nusu ya namba za video ya Sukari, hivyo naye ana kazi kama Yemi Alade. Je, atafanikiwa kujinasua hapo?.

Ukiachana na Yemi Alade, baadhi ya wasanii Afrika wanaopitia changamoto kama hiyo katika muziki wao ni Harmonize, Master KG, Runtown, Magic System, Tyla na Ayra Starr.
Na walioushinda mtego huo kwa kutoa video zaidi ya moja zilizofikisha ‘views’ zaidi milioni 100 ni pamoja na Burna Boy (5), Wizkid (5), Die Antwoord (5), Diamond Platnumz (3), Davido (3), Ckay (3), Omah Lay (3), Tekno (2), Rema (2), Fireboy DML (2).






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post