Zijue Faida za kufanya Mapenzi Kiafya

Zijue Faida za kufanya Mapenzi Kiafya

Ee bwana mara nyingi vijana wengi huingia katika mahusiano na baadae hujihusisha na kitendo cha kujamiana bila kujua jambo hilo lina faida gani kiafya.

Leo katika makala ya afya Mratibu wa Lishe Manispaa ya Temeke Dk. Charles Malale anafunguka juu ya faida ambazo watu wanaweza kuzipata wanaposhiriki tendo la ndoa.

Akizungumza na MwananchiScoop, Dk. Malale anasema moja ya faida ya kushiriki jambo hilo ni kkuulinda mwili dhidi ya magonjwa ya moyo.

Anasema wanawake ambao hufika kilele (orgasm) angalau mara mbili kwa wiki kila wanapojamiana, wana uwezekano mdogo sana (30% tu) wa kupata maradhi ya moyo tofauti na wale wasiofikia kilele.

“Hii ni kwa vile homoni ya endorphin inayotolewa wakati wa kujamiiana hupunguza msongo wa mawazo na hivyo kumuepusha mtu na magonjwa wa moyo. Aidha kujamiiana angalau mara tatu kwa wiki, husaidia kupunguza uwezekano wa kupata shambulio la moyo (heart attack) na kiharusi.

“Uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo wakati wa kufanya mapenzi ni mdogo sana, ni asilimia 1 tu ya vifo vyote vinavyotokana na mshtuko wa moyo ndivyo huhusishwa na kujamiiana,” alisema.

Aidha, alisema sababu nyingine inayoongeza uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo ni kuwa na uhusiano nje ya ndoa ambapo huchangia karibu asilimia 75 ya vifo vinavyotokana na kujamiiana, na karibu asilimia 90 ya vifo hivi hutokea kwa wanaume wazee.

“Uwezekano wa kupata shambulio la moyo wakati wa kujamiiana huongezeka ikiwa mtu ana miaka zaidi ya 50, uzito uliopitiliza na matatizo ya afya. Hii ni sawa na kusema unaanza kufanya mazoezi mazito kwa ghafla wakati mwili na umri haviruhusu,” aliongeza.

Hupunguza msongo wa mawazo

Dk. Malale alisema kujamiiana hupunguza msongo wa mawazo na shinikizo la damu na humfanya mtu kupata usingizi mnono.

Alisema kufikia kilele ni sawa na kunywa 2-3mg za dawa ya diazepam (kumbuka diazepam hufanya mwili kupumzika, muscle relaxant), na hii ndiyo sababu kuu ya kwa nini watu hupata usingizi mzito baada ya kujamiiana.

Watu wanaojamiiana huweza kuhimili vizuri msongo wa mawazo tofauti na wale ambao hawafanyi hivyo. Aidha watu wanaojamiiana huwa na kiwango cha kawaida cha shinikizo la damu kuliko wale wasiojamiiana.

“Pia kuwepo kwa viasili vya prostaglandins katika shahawa husaidia kupunguza msongo wa mawazo. Viasili hivi hunyonywa na sehemu za siri za mwanamke. Shahawa pia zina madini ya zinc, calcium, potassium, fructose na protini ambavyo vyote ni muhimu kwa afya njema,” alisema.

Hupunguza maumivu

Hata hivyo Dk. Malale alisema kufikia kilele (orgasm) wakati wa kujamiiana ni tiba ya maumivu.

Anafafanua kuwa homoni ya Oxytocin inayotolewa kwa wingi kabla na wakati wa kujamiiana pamoja na viasili vya endorphins hupunguza maumivu ya kichwa, mgongo, kipandauso, baridi yabisi pamoja na dalili zinazotokea baada ya kukoma hedhi (post menopause syndrome symptom).

Kufanya mapenzi huongeza urembo wa mwanamke

Alisema kuwa wanawake wanaojamiiana angalau mara nne kwa wiki huonekana kuwa na umri mdogo ikilinganishwa na umri wao kwa miaka 7 mpaka 12, hii inatokana na ukweli kuwa kujamiiana huongeza homoni ya oestrogen ambayo hufanya nywele za wanawake kuwa na afya nzuri na ngozi zao kung’aa.

Huongeza uwezo wa kunusa

Dk. Malale alisema baada ya kujamiiana, kiwango cha homoni ya prolactin huongezeka, ambayo hufanya seli za ubongo (brain stem cells) kutengeneza seli mpya katika sehemu inayohusika kunusa na kutambua harufu (brain olfactory bulb).

Hupunguza uzito na kumfanya mtu kuwa na afya njema

Pia alisema kujamiiana ni mazoezi mazuri kwani wakati wa kufanya tendo hilo mapigo ya moyo huongezeka kutoka wastani 70/dakika mpaka 150/dakika ambayo ni sawa na mtu anayefanya mazoezi kwa kiwango cha juu.

“Kujamiiana huchoma karibu 200 calories sawa na kukimbia dakika 15 katika mashine ya tredmill. Mwanamke anayefika kilele huchoma calories 47 zaidi,” anasema.

Huongeza kinga ya mwili

Alisema kuwa kufanya mapenzi mara moja au mara mbili kwa wiki huongeza kiwango cha seli za kinga aina ya immunoglobulin A kwa robo tatu na hivyo kumkinga mtu dhidi ya mafua na magonjwa mbalimbali.

Pia tendo hilo udhibiti mzunguko wa hedhi kuwa wa kawaida, “Wanawake ambao hujamiiana angalau mara moja kwa wiki (isipokuwa siku ambazo wako kwenye hedhi) huwa na mzunguko wa hedhi wa kawaida ikilinganishwa na wale ambao hufanya mapenzi kwa nadra au wale ambao hawafanyi kabisa,” alisema.

Tendo la ndoa huongeza hali ya kujiamini

“Nakwambia kuwa ikiwa litafanyika baina ya wapendao, na tendo lenyewe likawa la furaha na upendo, kujamiana huongeza kujiamini,” alisema.

Dk. Malale alisema tendo hilo pia linaongea ukakamavu katika misuli ya nyonga (pelvic floor muscles) na hivyo kuzuia mwanamke kupata matatizo ya mkojo au ugonjwa wa kibofu cha mkojo.

“Wanawake ambao wamekoma kupata hedhi, kufanya mapenzi mara kwa mara huondoa tatizo la kusinyaa kwa sehemu za siri za mwanamke (vagina atrophy) na hivyo kumwepusha na maambukizi katika njia cha mkojo (Urinary Tract Infection),” anasema.

Pia Dk. Malale alifafanua kuwa kufanya mapenzi huongeza kasi ya mzunguko wa damu mwilini.

“Unapojamiiana na kufikia kilele, mzunguko wa damu huongezeka maradufu, hivyo kuongeza mzunguko wa hewa aina ya oksijeni kwenda kwenye viungo muhimu kama moyo, ubongo na figo hivyo kusaidia kuondoa uchafu na sumu mbalimbali mwilini,” alisema.

Husaidia kuishi kwa muda mrefu

Anasema kufanya mapenzi angalau mara mbili kwa wiki hurefusha maisha. “Kila unapofikia kilele, homoni aina ya DHEA (Dihydroepiandrosterone) hutolewa kwa wingi kutokana na raha ya tendo na kufikia kilele.

“DHEA huongeza kinga ya mwili, hurekebisha tishu zilizoharibika (hutibu vidonda), huongeza kiwango cha ufanyaji kazi cha ubongo, huiweka ngozi kuwa na afya bora na hupunguza msongo wa mawazo. Kwa hiyo, kuongeza kufikia kilele kuna uwezekano wa kurefusha maisha yako,” alisema.

Aidha anasema kufanya mapenzi kuna ongeza uwezo wa kuzaa au kutunga mimba.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags