Zaidi ya Milioni 422 zatolewa kwa wananchi wa Saranga kuboresha huduma za maji safi na salama

Zaidi ya Milioni 422 zatolewa kwa wananchi wa Saranga kuboresha huduma za maji safi na salama

Zaidi ya Sh. 422 Milioni zimetolewa kwa lengo la kuboresha huduma za maji safi  na salama kwa wananchi 2500 wa kijiji cha Saranga Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la WaterAid, Anna Mzinga, wakati wakikabidhi mradi huo kwa wanakijiji hao uliofadhiwa na WaterAid kwa kushirikiana na kampuni ya Coca-Cola Foundation na People Postcode Lottery (PPL).

Alisema mradi huo ambao ni wa awamu ya pili wa kuwapatia wananchi maji safi na salama, umetekelezwa kwa miezi 11 kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana.

Mzinga alisema wamekuwa mashahidi wa namna mabadiliko ya tabia nchi yalivyoleta athari katika ukanda wa Afrika Mshariki na Tanzana ikiwamo kusababisha ukame, mafuriko na ukosefu wa maji safi na salama kutokana na kukauka kwa vyanzo vya maji.

"Hivyo kutokana na athari hizo, hali ya upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwamo wa huduma ya maji safi imekuwa ni tatizo, msaada huu ulitolewa unakwenda kuwa mkombozi kwa wananchi hao," alisema

Mzinga alisema msaada huo ambao ni usimikaji wa vituo vinne vya kukinga maji unabadilisha maisha kwa kuwezesha upatikanaji wa maji kwa wanakijiji zaidi ya 2,500 wa Sangara kwa kupunguza adha iliyokuwa inawakabili wanawake kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji.

Alisema maono yao kama Shirika la WaterAid Tanzania ni kuona kuwa kila Mtanzania anapata maji safi na salama katika vipindi vyote vya kiangazi au masika.

Naye Mkurugenzi msaidizi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Pamella Temu, alisema maeneo mengi ya Tanzania bado hayana vyanzo vya maji vya uhakika.

“Kwa hapa  Manyara, tunafurahi tumepata maji kwa kuchimba visima, kuteka chemchem  na hata kuvuna mvua, lakini bado tuna matatizo kadhaa katika vyanzo hivi, uharibifu wa vyanzo vya maji unaosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwamo mvua kubwa au ndogo katika vipindi visivyotarajiwa, mafuriko na kiangazi kikali.

“Niwaombe msisahau matatizo kwani ni moja ya sehemu inayozorotesha wizara kuwafikia wananchi wengi kwa wakati. Imani yangu kama wizara ni kwamba tunajenga nyumba moja hivyo ushirikiano ni jambo muhimu,” alisema

Temu aliitaka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), wilaya na mkoa kuyashughulikia kwa ukaribu kwani uendelevu wa mradi huo ni moja ya vipaumbele vya serikali kumtua mama ndoo kichwani.

Kwa upande wake Rais wa Cocacola Foundation, Saadia Madsbjerg, alisema jitihada zao ni kuhakikisha wanafanya mabadiliko barani Afrika katika kuendelea kuunga mkono jitihada mbalimbali za mashirika ya misaada kuhakikisha yanatekeleza miradi yenye manufaa inayoinua maisha ya jamii kwa ujumla hususani kwa wanawake na wasichana.

“Mradi huu unaotekelezwa wilayani Babati ni mfano mwingine unaoonyesha  namna ambavyo misaada ya kimkakati inaweza kuhakikisha watu wanapata maji katika maeneo ya pembezoni katika bara la Afrika.” alisema

Mkazi wa Kijiji hicho, Neema Daudi amesema kabla ya  mradi huo alikuwa anatembea zaidi ya saa nzima kuchota maji katika Kijiji cha Jirani.

 

“Mradi huu umeniwezesha kuanzisha mradi bustani ya mbogamboga nyumbani kwangu na kabla ya mradi huu nililazimika kwenda sokoni kununua,” alisema.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags