Yule Daktari akaniharibia kwa Wife

Yule Daktari akaniharibia kwa Wife

 

Hatukuwa na vita kali sana na mke wangu, isipokuwa tatizo lake lilikuwa tukikorofishana kidogo zinaweza zikapita wiki mbili hadi tano anazira kuzungumza nami. kwa kweli hii tabia yake ilinichochea kuanza kuwa na uhusiano wa nje ili kupata ‘kampani.’

Hata hivyo hakuwa na uhakika kwamba nina uhusiano wa nje ingawa alikuwa akihisi kwa kiasi cha kutosha. Kiasi cha miaka minane iliyopita tabia yake ya kuzira na yangu ya kutoka nje ya ndoa ilizua la kuzua.

Ilikuwa hivi: siku moja niligombana kidogo na mke wangu na nikamtolea lugha chafu. Kitendo hicho kilichukua wiki tatu bila kuzungumza nami. Kwenye ile wiki ya pili tangu kufungiwa milango ya mazungumzo, nikapata tatizo. Kwenye hangaika yangu, nilikwaa maradhi ya zinaa.

Ilibidi nipige hesabu ya hospitali. Mke wangu alikuwa ni muuguzi kwenye hospitali moja ya serikali ambayo ndiyo niliyokuwa nikitibiwa. (Naomba nisiitaje). Niliogopa ningeweza kukutana naye na hata kama hataniuliza mimi, angewauliza madaktari tatizo langu.

Hivyo niliamua kwenda hospitali nyingine ya binafsi. Nilipofika niliingia kwa daktari ambaye alinichangamkia sana. (Nawashauri kwamba, siku ukienda mahali ambapo unajua hujuani na mtu halafu akatokea mtu akakuchangamkia sana, jiulize mara mbili).

Huyu daktari aliniuliza kama nimeoa, ambapo nilimdanganya kwamba sijaoa. Akaniuliza kama naweza kumkumbuka mtu aliyeniambukiza ili nije naye pale apate huduma. Nilidanganya kuwa amesafiri.

Yule daktari aliniandikia dawa na kabla hajamaliza kuandika alitoka nje akiniomba radhi kwamba, anarejea punde.

Nilikaa kusubiri daktari arejee. Kama dakika kumi baadaye, nikiwa nimeboreka, niliona mlango ukifunguliwa. Halafu nilimuona daktari. Lakini nyuma ya daktari kulikuwa na utata. Nilimwona mke wangu akiwa katika sare zake za uuguzi. ‘samahani. Nimetaka uje uone jinsi watu wanavyofanana. Mimi nilidhani ni shemeji mumeo.’ Alisema daktari akimwambia mke wangu.

Halafu alinigeukia, ‘samahani, yaani mnafanana na mume wa huyu muuguzi wetu, yaani basi tu.’

‘Anaumwa kitu gani?’ Mke wangu alimuuliza daktari.

Yule daktari akamjibu, ‘ni siri yangu na mgonjwa. Nilitaka tu uone maajabu ya kufanana yalivyo. Nilimwona mumeo ile siku ya harusi tu, lakini sura naikumbuka bado. Wanafanana sana kwa kweli….’

Mke wangu alimkata kalma daktari.  ‘Ni yeye kweli. Nashangaa anajifanya hanijui mkewe. Na ndio maana nakuuliza anaumwa kitu gani? Mke si ana haki ya kujua mumewe anaumwa nini?’ Yule daktari akijifanya hakuwa anajua hilo alisema, ‘aisee ni jambo la kusikitisha. Mumeo ana matatizo ya gonorea……

Mke wangu aliruka kwa hamaki na kusema, ‘ati nini, ana kitu gani?’ Yule daktari alimwambia mke wangu atulie. Nilisimama nikiwa na hasira hasa dhidi ya yule daktari.

Inakuwaje akamwite mke wangu na kumpa taarifa ile! Sura ya daktari yule kwa mbali niliikumbuka sasa, ni kweli alikuja kwenye harusi yetu. Alikuwa ni rafiki wa kaka wa mke wangu.

Wakati nataka kutoka, yule daktari alisema, ‘usikasirike, ni vyema tuyazungumze yaishe. Ni jambo la kusikitisha, mkeo kuniambia kwamba tangu ahamie kwenye hospitali yetu kwa takriban siku kumi sasa, wewe hujui, eti kwa sababu hamzungumzi.’

Yule daktari alijitahidi kuwa na diplomasia akijaribu kututaka tujadili jambo lile likiwemo la gonorea ili tuyamalize.  Mke wangu alikuwa mkali kama pilipili na hakutaka kumpa yule daktari nafasi ya kusuluhisha ugomvi wetu.

Hata hivyo baada ya daktari yule kutumia busara ya hali ya juu, hatimaye mke wangu alitulia na tukayazungumza na kuyamaliza na sasa ndoa yangu ni imara kuliko kawaida.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post