Yajue matangazo ya biashara yaliyojaa ulaghai

Yajue matangazo ya biashara yaliyojaa ulaghai

Kutokana na utandawazi pamoja na soko huria, siku hizi tumeshuhudia muingiliano wa mkubwa wa kibiashara ambapo yako makampuni mengi ya kigeni yamefungua biashara hapa nchini na hivyo tumejikuta tukiwa tumezungukwa na bidhaa mbalimbali toka nchi za Magharibi, Uchina, Mashariki ya kati na Asia kwa ujumla.

Kutokana na hali hiyo tumejikuta tukishuhudia matangazo ya biashara kila mahali kuanzia kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, kwenye status za Whattsup hadi kwenye vipeperushi, na hivyo hata ile methali yetu ya chema chajiuza na kibaya chajitembeza inaonekana kupitwa na wakati.

Mfumo huu wa matangazo ya biashara upo wa aina nyingi sana hivyo ni vyema tukajifunza baadhi ya matangazo yaliyojaa ulaghai ili tuwe makini wakati wa kufanya manunuzi.

Yapo matangazo yanayotolewa katika mfumo wa aina mbalimbali lakini yapo yale ambayo huonyesha bidhaa zinazouzwa kwenye duka husika yakiwa na bei halisi na punguzo maalum kwa muda maalum.

Matangazo ya aina hii hujulikana kama Informative advertisement  na  ni  mazuri kwa kuwa yanamfanya mnunuzi aweze kuchagua bidhaa akiwa nyumbani na huku akiwa na uhakika na bei, hivyo kupanga bajeti kulingana na kipato chake.

 

Lakini inashauriwa kuwa makini na matangazo ya aina hii, kwani mengi yamejaa ulaghai kwa kiasi fulani. Kwa mfano, unaweza kukuta bidhaa imeandikwa kuwa, sasa inauzwa kwa punguzo la asilimia 25. Hapo mnunuzi lazima ujiulize kuwa ni asilimia 25 ya bei gani?

Kwani yawezekana kweli kuna punguzo la asilimia 25, lakini vile vile kuna uwezekano pia, kuwa bei ya awali iliongezwa asilimia 50 zaidi ya bei halisi, hivyo unaweza kukuta bei ya bidhaa ile ni ghali ukilinganisha na maduka mengine.

Hivyo inashauriwa kufanya utafiti na kulinganisha bei katika maduka mengine, kwani hii itakusaidia kuepuka gharama za ziada zilizojificha.

Aina ya pili ya matangazo ya biashara ni hii inayohusisha bidhaa ambazo zimejijengea umaarufu ulimwenguni pote. {Brand name Advertising}.

Naamini kuwa wengi sio wageni wa bidhaa kama Sony, JVC, Nokia, Samsung, HTC, Apple na LG hizo ni bidhaa  kwa upande wa vifaa vya Elektroniki kama simu nk. Lee na Levi kwa upande wa nguo za Dangriz maarufu kama Jeans, au Nikon, Minolta, Canon, Olympus, Sony nk, kwa upande wa kamera.

Mara nyingi bidhaa za aina hii huwa zinajiuza zenyewe kutokana na umaarufu na uimara wake, ingawa pia bei yake ni ghali kutokana na umaarufu wa bidhaa yenyewe.

Hivyo utakuta mara nyingi mtu anayetaka kununua bidhaa za aina hii huwa anajiandaa kifedha kwa kuwa anajua kabisa bei haitakuwa ndogo.

 

Lakini pia ningependa kutahadharisha kuwa siku hizi kumeibuka makampuni/viwanda vinavyotengeneza bidhaa zinazofanana kabisa na bidhaa nilizotaja hapo juu na kuandika jina linalofanana na majina niliyoyataja awali, lakini majina yenyewe yanaweza kubadilishwa herufi mojawapo ili isifanane na bidhaa halisi au kubadilisha alama pia ili isiwiane na bidhaa halisi.

Hii inafanyika makusudi ili kuepuka kufunguliwa mashitaka na makampuni husika ambayo ndiyo wazalishaji halisi wa bidhaa hizo.

Mara nyingi bidhaa hizi huuzwa kwa bei rahisi sana, ukilinganisha na bei ya bidhaa halisi, hivyo mnunuzi anapoona, kwa haraka hununua bila kuchunguza na kujikuta amenunua bidhaa duni.

Aina ya tatu ya matangazo ni ile ambayo haimtendei haki mteja, kwa kutumia lugha laghai kushawishi wateja, ambapo lugha inayotumika inakuwa ina ukweli lakini inapotosha kwa upande mwingine. Aina hii ya tangazo la biashara hujulikana kitaalamu kama Deceptive Advertising.

Hebu tuangalie mfano huu ufuatao kuhusiana na mchele. Unakuta tangazo kwenye gazeti linalosomeka “Jipatie mchele safi toka kyela kwa bei ya shilingi 1500 kwa kilo moja”.

Kwa haraka msomaji anaamini kuwa mchele unaolimwa Kyela unapatikana kwa bei rahisi kiasi kile, hivyo inamgharimu mteja kusafiri au kuendesha gari lake umbali wa kama kilomita 30 kufuatilia mchele kutoka Kyela, lakini anapofika pale anagundua kuwa ule mchele sio wa Kyela na hauna ubora kama mchele wa Kyela.

 

Anapomuuliza mwenye duka, kuwa kwa nini ametangaza kuwa anauza mchele kutoka Kyela wakati hana huo mchele wenyewe, mwenye duka anamjibu kuwa duka lake ndilo linaloitwa Kyela Trading Company, hivyo alikuwa anamaanisha jina la duka lake.

Kwa hiyo kwa mfano huo utakuta kuwa tangazo la mwenye duka lile halikuwa na makosa, bali lilikuwa linapotosha wateja, kwa sababu wateja wengi wangedhani kuwa duka lile linauza mchele kutoka Kyela, hivyo kwa kuzingatia usumbufu alioupata katika kufuatilia mchele ule atajikuta hana budi kununua mchele huo usio wa Kyela japo hata kilo moja kuliko kurudi mikono mitupu.

Aina ya nne ni ile ambayo mwenye duka anatangaza kuwa aina fulani ya bidhaa inapatikana dukani kwake kwa bei pungufu ya karibu shilingi elfu kumi au elfu hamsini ukilinganisha na bei ya maduka mengine. Ningependa kuelezea aina hii ya tangazo kwa kutumia mfano ufuatao.

Fikiria unasoma tangazo la duka linalouza runinga (TV) flat screen kwa bei labda teseme yenye punguzo la karibu shilingi 100,000, ukilinganisha na bei ya maduka mengine.

Ukizingatia kuwa mkeo na watoto, wamekuwa wakikughasi kuhusu umuhimu wa kununua runinga flat screen kwa muda mrefu na baada ya kuzunguka sana madukani ukakuta aina ya runinga unayoitaka, lakini inauzwa ghali ukilinganisha na bajeti yako, hivyo ukaamua kuahirisha.

Lakini kwa bahati unakutana na tangazo kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram, status za Whattsup, Facebook au gazeti ambalo lina tangazo la duka linalouza runinga uliyokuwa unaitafuta kwa bei ambayo hukuitarajia.

Unafunga safari hadi kwenye duka hilo na unapofika unakuta runinga hizo hazipo, unapomuuliza muhusika, anakuonesha maneno yaliyoandikwa kwenye tangazo hilo, chini kabisa, tena kwa maandishi madogo sana yanayosema kuwa runinga zile zilikuwa zinauzwa kwa idadi maalum, hata hivyo anakwambia kuwa anazo runinga nyingine nzuri sana zaidi ya zile zilizoisha.

Kwa kuwa umekuja tayari na fedha inakuwa ni rahisi kwake kukuchota ununue runinga hizo ambazo hazina ubora ulioukusudia kwa bei kubwa na pengine ambayo hukuitaka.

Aina hii ya matangazo hufanana na hii ambayo hutumiwa sana na wauza magari.

Ni ile ambayo muuzaji hutumia picha katika tangazo kupotosha. Kwa mfano unataka kununua gari. Baada ya kusoma matangazo kwenye mitandao ya kijamii au kwenye magazeti, unakutana na tangazo la kampuni fulani inayouza magari ambapo unakutana na picha ya gari ulilokuwa unatamani kulimiliki likiwa linauzwa kwa bei ambayo unaimudu.

Unapofika pale dukani unakuta picha uliyoiona kwenye tangazo haifanani na gari halisi ulilokuwa unalitaka, kwani mara nyingi picha huwa zina mvuto wa pekee.

Wakati umebaki ukijiuliza, muuzaji anakuonesha aina nyingine ya gari zuri na anakuahidi kukupunguzia bei kama utataka kulinunua.

Baada ya majadiliano mnakubaliana bei ambayo inakubidi ukaongeze fedha kidogo, na kwa kuwa gari lenyewe ni zuri sana na lina ubora kushinda lile ulilolitaka, unajiona u mwenye bahati, hivyo unaondoka huku ukiahidi kurudi siku inayofuata kununua gari hilo.

Unapofika pale siku inayofuata, yule muuzaji anakupeleka ofisini. Wakati anaanda makabrasha ya kusaini kabla ya kupokea fedha, mara inapigwa simu, yule muuzaji anapokea ile simu na kuongea nayo, baada ya majadiliano fulani kwenye simu, anakwambia kwamba, mwenye duka kasitisha uuzwaji wa gari lile kwani amegundua kuwa ataingia hasara, hivyo itabidi uongeze fedha kidogo.

Kwa kuwa ulijiandaa kununua gari unajikuta huna jinsi, unakopa kwa jamaa zako na unaongeza fedha zaidi na kununua gari lile, hasa ukizingatia kuwa wauzaji wa maduka ya magari wana lugha nzuri ya kushawishi, inakuwa ni vigumu kwako kujinasua au kuukwepa mtego huo.

Baadae ukichunguza utakuta umeuziwa bei sawa au zaidi ya bei ya maduka mengine.

Aina ya tangazo hili la biashara hujulikana kama Low-Ball Phenomenon na wauzaji wengi wa magari wamethibitisha kuwa wateja wengi hununua magari kwa mfumo huu, hivyo kuwaingizia faida.

Sina maana kwamba matangazo yote ni ya ulaghai, au matangazo yote ni mabaya, hapana.

Ninachotaka mkifahamu ni kwamba, msipokuwa waangalifu mnaweza kujikuta mmeongozwa vibaya na matangazo na kununua bidhaa au kitu ambacho wala hukuwahi kukifikiria kabla na pengine kwa bei kubwa zaidi.

Lakini mnaweza pia kujikuta mkiwa watumwa wa matangazo kwa maana ya kuyaamini sana kiasi kwamba mtadhani kila kinachotangazwa ndivyo kilivyo.

Pia mnapaswa kujua kwamba kuna wanaotangaza bidhaa halali na kwa njia halali ambao hao mnaweza kuwabaini kwa kuzingatia kile ambacho nimewaambia. Kila mkisoma tangazo likagueni vizuri kabla hamjaamua






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags