Weka nguvu kwenye thamani yako

Weka nguvu kwenye thamani yako

Umewahi kujiuliza kwa nini kuna watu wanaonekana wana thamani kubwa dhidi ya wengine, wanaweza wakawa wanafanya kazi pamoja, elimu sawa na wala hawajazidiana kiuchumi, lakini lazima mmoja wao atazungumzwa tofauti.

Thamani ya mtu ni vile anavyotazama vitu na kuvitafsiri mbele ya wengine, na wakati mwingine hatua za kijasiri anazochukua za kutenda ama kufanya maamuzi yasiyo ya kawaida mbele ya jamii.

Kuonekana una thamani halisi si jambo linalokuja kwa bahati mbaya, kuna uwekezaji wa muda, bidii na kujifunza zaidi ili kufanya vitu tofauti na wale wanaokuzunguka.

Kwa haraka haraka, unaweza kujihoji mwenyewe, kwenye majukumu yako, masomo ama chochote unachokifanya, kuna utofauti na unaoshindana nao, kipi kipya cha wewe kutazamwa na wengine kujifunza kwa ajili yako?.

Kama ukiona kile unachokifanya, unafanya kwa ajili ya kutimiza wajibu wako na hauna ubunifu wa kufanya kiwe na mvuto dhidi ya wengine ambao wanafanya kitu kama chako, inakuwa ngumu wewe kupandishwa thamani yako.

 Kuna watu katika kile kile unachokifanya, wanawaza mbali zaidi, wanaongeza ubunifu unaofanya wale wanaomzunguka wamfikirie mara mbilimbili na kutamani kujifunza zaidi kutoka kwao.

 Wengine wanafikiria mbali zaidi, wakidhani pengine kuna watu wameandikiwa kuwa na thamani mbele ya jamii, bila kujikagua mienendo yao na wakaamua kuchukua hatua ya kujitoa na kujifunza.

 Ukiachana na hilo, kuna kila sababu ya kuangalia ni sehemu gani unaweza ukapata thamani yako, ingawa thamani haiwezi kulingana, kutokana na uzoefu, elimu hapo kila mtu anaweza akala urefu wa kamba yake.

 Mfano, tuchukulie wafanyabiashara wadogo kwenye soka fulani, mwingine anaweza akawa anajiongeza kama  kuzungumza vizuri na wateja, mazingira ya kazi yake anavyoyaweka, kuwahi kufika kazini kwake, halafu kuna mwingine hafanyi hayo yote, hapo lazima watakuwa watu wawili tofauti.

 Ukiachana na hilo, unaangalia ukikaa na watu gani, ama sehemu gani wanaona thamani yako, hapo utapaswa kupashikiria na kuongeza ubunifu zaidi ya wanavyoona ni muhimu kwao.

 Neno thamani lina maana yake na linagusa maeneo mengi, wakati mwingine inaweza ikawa mahusiano ya kimapenzi ukajikuta upo na mtu asiyetambua thamani yako, akakuonesha hustahili kuwa naye, bora ukampisha na kujipa uvumilivu wa kumpata aliye sahihi kwako acha uoga na kuwaza mlipotoka .

 Ili thamani yako ianze kuonekana ni wewe mwenyewe kuanza kuchukua hatua ya kubadilisha mtazamo kwa baadhi ya maeneo uliyokuwa unachukulia vitu kawaida na haukuvipa umuhimu unaopaswa.

 Anza kujipa thamani mwenyewe, tambua hakuna ‘kopi’ yako duniani, hivyo hakuna mwingine wa kukufanyia majukumu yako ipasavyo isipokuwa mwenyewe, ukianza kufanya hivyo zipo hatua ambazo utaanza kuziona na jamii kukuona kwa viwango vingine.

 Acha kunyoosha vidole kwa mwingine kuona kuwa ndio wanapaswa ‘levo’ fulani, halafu wewe unaishia hatua ya chini, basi jambo likiharibika unathubutu kulalamika, sasa anza kujisikia vibaya endapo ukiona sehemu fulani hapakufanyika kitu kwa usahihi wake.

 Kadri unavyolichukulia jambo unalopaswa kulifanya, lazima uangalie lina matokeo gani, ukiona mwingine kalifanya lile lile, lakini linasimulika kwa ukubwa, basi jua thamani yako itakuwa ngumu kupanda.

 Mfano mzuri tujifunze kidogo kwa mwanasiasa wa Uganda, Bobi Wine (41), mwenye mvuto mkubwa kwa vijana, kutokana na ujasiri wake wa kujitosa kwenda kugombea Urais, siyo kazi ndogo amekuwa akikutana na mikikimikiki ya hapa na pale.

 Kuthubutu kwake na kuona hakuna linaloshindika, ndiyo kitu kinachomfanya afuatiliwe na vijana wengi wanaopenda ujasiri wake, unaweza ukajiuliza kuna wanasiasa wangapi vijana nchini Uganda, kwa nini yeye anaiteka mitandao ya kijamii, ameweka muda kuipa thamani kazi yake.

 Ukiachana na huyo kuna kiongozi wa upinzani kutoka Afrika Kusini, Julius Malema ni jasiri, asiyeogopa kukabiliana na misukosuko, ana kauli zake za kishujaa, moja wapo anasema haogopi watu wanamuongeleaje, wanamuonaje anachojali ni moyo wake na ndoto alizobeba, hivyo hawezi kuusaliti.

Ushawishi wake mkubwa ni namna anavyopigania maslahi ya watu, kufanya maamuzi magumu asiyojali yanaweza yakamgharimu, anachokisema kama amepewa jukumu la kulifanya basi hawezi kujihurumia binafsi.

Wanasema yale unayojinenea ndivyo yanatokea unatakiwa kufahamu kuwa mchawi wako wa kwanza  ni wewe mwenyewe, ukisema hauwezi basi itakuwa hivyo na ukisema unaweza basi utaweza kweli.
Penda kujifunza kwa hao wanaofanya vizuri pita njia zao ili na wewe uweze kuzungumziwa kama wao, na siyo kuzalisha chuki dhidi yao eti kwa sababu wao wamefanikiwa kukuzidi wewe.

 Hakuna aliyezaliwa anajua wote wamejifunza, nawe kuwa miongoni mwa wanaojifunza ili uweze kutengeneza mabadiliko ndani yako, jifunze kusema neno hujui ili ufundishwe kaata kujifanya kila kitu unaweza kwa sababu tabia hiyo ni sumu kwenye kuongeza maarifa yako mwenyewe.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post