WASIFU WA MALKIA ELIZABETH II

WASIFU WA MALKIA ELIZABETH II

Utawala wa muda mrefu wa Malkia Elizabeth II ulijawa na hisia kuu za kuwajibika na kujitolea kwake maisha yake yote kwa cheo chake kama malkia na pia kwa watu wake.

Kwa watu wengi, yeye alikuwa kitu kimoja ambacho hakikubadilika ulimwengu ulipokuwa unabadilika kwa kasi na nguvu za Uingereza duniani kupungua. Jamii ilibadilika pakubwa na majukumu na manufaa ya familia ya kifalme nayo yakaanza kutiliwa shaka.

Kufanikiwa kwake katika kudumisha pamoja familia ya kifalme katika kipindi hicho cha misukosuko kilikuwa ni jambo kubwa sana hasa ikizingatiwa kwamba wakati wa kuzaliwa kwake, hakuna aliyetarajia kwamba angeishia kuwa malkia na kwa muda mrefu.

 

Elizabeth Alexandra Mary Windsor alizaliwa mnamo 21 Aprili 1926, katika jumba lililokuwa karibu na Berkeley Square jijini London.

Alikuwa kifungua mimba wa Albert, Mwanamfalme Mtawala wa York, aliyekuwa mwana wa pili wa kiume wa George V, na mkewe ambaye zamani alifahamika kama Lady Elizabeth Bowes-Lyon.  

Elizabeth na dadake, Margaret Rose, aliyezaliwa mwaka 1930, walipewa elimu nyumbani na kulelewa katika mazingira ya familia yaliyojaa upendo.

Elizabeth alikuwa na uhusiano wa karibu sana na babake na babu yake, George V.

Alipokuwa na miaka sita, Elizabeth alimwambia mwalimu wake wa uendeshaji farasi kwamba alitaka kuwa "mwanamke wa kukaa mashambani na awe na farasi na mbwa wengi."

Alidaiwa kuanza kuonyesha hisia za juu sana za kuwajibika kutoka akiwa na umri mdogo sana.

Winston Churchill, ambaye baadaye alikuwa waziri mkuu, alinukuliwa akisema kwamba "alionyesha hisia za kuwa na mamlaka ambazo zilikuwa nadra sana kupata kwa mtoto kama yeye."

Licha ya kutohudhuria masomo katika shule ya kawaida, Elizabeth alifanya vyema sana katika kuzifahamu lugha mbalimbali na alifanya usomaji wa kina wa historia ya kikatiba.

Kundi maalum la maskauti wa kike, maarufu kama Girl Guides, lililofahamika kama 1st Buckingham Palace liliundwa ili aweze kujumuika na kuzoeana na wasichana wa rika lake.

Baada ya kifo cha George V mwaka 1936, mwanawe mkubwa wa kiume, aliyefahamika kama David, alirithi ufalme na kuwa Mfalme Edward VIII.

Hata hivyo, mwanamke aliyeamua kumuoa, Mmarekani aliyekuwa ametalikiwa mara mbili Wallis Simpson, hakukubalika kwa misingi ya kisiasa na kidini wakati huo. Mwishoni mwa mwaka, alijiuzulu.

 

Mwanamfalme Mtawala wa York, babake Malkia Elizabeth, alichukua ufalme na kuwa Mfalme George VI. Kutawazwa kwake kulimdokezea Elizabeth maisha yaliyomsubiri na baadaye aliandika kwamba aliiona sherehe hiyo kuwa "ya kupendeza sana".

Huku uhasama na wasiwasi ukiongezeka Ulaya, Mfalme huyo mpya, pamoja na mkewe, Malkia Elizabeth I, walichukua jukumu la kurejesha imani ya umma katika familia ya kifalme.

Mfano wao ulimgusa binti wao mkubwa.

Mwaka 1939, binti mfalme huyo aliyekuwa na miaka 13 wakati huo, aliandamana na Mfalme na Malkia kwenye hafla katika chuo cha jeshi la wanamaji la Royal Naval College, Dartmouth.

Kwa pamoja na dadake Margaret, alimsindikiza mmoja wa waliokuwa wanafuzu, binamu wake wa kiwango cha tatu, Mwanamfalme Philip wa Ugiriki.

Vikwazo 

Hiyo haikuwa mara yao ya kwanza kukutana, lakini ilikuwa mara ya kwanza kwake kuanza kuvutiwa naye.

Prince Philip aliwatembelea jamaa zake wa familia ya kifalme alipokuwa likizoni kutoka kwenye jeshi la wanamaji - na kufikia mwaka 1944, alipokuwa na miaka 18, ilikuwa wazi kwamba Elizabeth alikuwa anampenda.

Alikuwa akiweka picha yake katika chumba chake na walikuwa wakiandikiana pia barua.

Binti mfalme huyo alijiunga na kikosi cha wafanyakazi wa ziada wasaidizi wa jeshi kwa jina Auxiliary Territorial Service (ATS) mwishoni mwa vita, ambapo alijifunza kuendesha na kukarabati lori.

Siku ya kumalizika kwa vita, ambayo hufahamika kama VE Day, alijiunga na jamaa wengine wa familia ya kifalme katika Buckingham Palace huku maelfu ya watu wakikusanyika katika barabara kuu ya kuelekea kasri hilo ambayo hufahamika kama The Mall kusherehekea kumalizika kwa vita Ulaya.

"Tuliwaomba ruhusa wazazi wetu tutoke nje kwenda kujionea wenyewe," alikumbuka baadaye.

"Nakumbuka tulikuwa na wasiwasi sana kwamba tungetambuliwa (na watu). Nakumbuka milolongo mirefu ya watu tusiowafahamu wakishikana mikono na kutembea kuelekea Whitehall, sote tulijumuika nao na kutembea kama waliobebwa na wimbi la furaha na kupata nafuu."

Baada ya vita, nia yake ya kutaka kuolewa na Prince Philip ilikabiliwa na changamoto kadhaa.

Mfalme hakutaka kumpoteza binti wake ambaye alimpenda sana na Philip alihitajika kuondoa pingamizi la ubaguzi katika familia ya kifalme ambayo haikuwapendelea watu wenye asili ya nje ya nchi.

Kifo cha babake

Lakini matamanio ya wawili hao yalitimia na mnamo 20 Novemba 1947, walifunga ndoa katika kanisa la Westminster Abbey.

Mtawala wa Edinburgh, cheo kipya cha Philip, alisalia kuwa mhudumu katika jeshi la wanamaji.

 

Kwa muda mfupi, alitumwa kuhudumu jeshini Malta, na huko kwa kiasi fulani walifurahia maisha ya kawaida.

Mtoto wao wa kwanza, Charles, alizaliwa 1948, akifuatwa na dadake, Anne, aliyezaliwa 1950.

Lakini Mfalme, baada ya kupata mfadhaiko sana na shinikizo wakati wa vita, alikuwa amezidiwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu, ambao ulitokana na kuwa mvutaji sigara sugu.

Januari 1952, Elizabeth, aliyekuwa na miaka 25 wakati huo, akiwa na Philip, walifunga safari ng'ambo.

Mfalme alikaidi ushauri wa madaktari na kwenda uwanja wa ndege kuwaaga.

Ilikuwa ni mara ya mwisho kwa Elizabeth kumuona babake akiwa hai.

Elizabeth alipata habari za kifo cha Mfalme akiwa katika mgahawa wa kitalii katika mbuga moja nchini Kenya na mara moja alirejea London akiwa sasa ndiye Malkia.

Baadaye alikumbuka yaliyotokea.

"Kwa njia fulani, sikuwa na wakati wa kujifunza kazi. Babangu alifariki akiwa bado na umri mdogo, kwa hivyo lilikuwa jambo la ghafla sana na ilikulazimu kuitekeleza kazi vyema kadiri ya uwezo wako."

 

Australia na New Zealand

 Sherehe ya kutawazwa kwake Juni 1953 ilipeperushwa moja kwa moja kwenye runinga, licha ya pingamizi kutoka kwa Waziri Mkuu Winston Churchill.

Mamilioni ya watu walikusanyika kutazama kwenye runinga, wengi wao kwa mara ya kwanza, kumtazama Malkia Elizabeth II akila kiapo.

Huku Uingereza ikiwa bado inakabiliwa na kipindi cha kubana matumizi ya ugumu wa kiuchumi baada ya vita, wachanganuzi walitazama sherehe hiyo ya kumtawaza malkia kama mwanzo wa enzi mpya ya mtawala mwingine kwa jina Elizabeth.

Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilikuwa vimeongeza kasi ya kufikisha kikomo himaya kuu ya Uingereza, na kufikia wakati Malkia alipoanza safari ndefu ya kuzuru mataifa ya Jumuiya ya Madola Novemba 1953, maeneo mengi ambayo zamani yalikuwa miliki ya Uingereza, ikiwemo India, yalikuwa yamejipatia uhuru.

Elizabeth aliibuka kuwa mfalme au malkia wa kwanza kuzuru Australia na New Zealand.

Ilikadiriwa kwamba karibu robo tatu ya raia wa Australia walijitokeza kumuona.

Katika miaka ya 1950, mataifa zaidi yaliitupa bendera ya Uingereza na koloni za zamani na tawala zake sasa zilikusanyika kwa pamoja na mkusanyiko wa mataifa yenye uhusiano wa pamoja, kwa hiari.

Wengi wa wanasiasa walihisi kwamba Jumuiya mpya ya Madola ingetoa ushindani kwa muungano uliokuwa unaibuka wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya na, kwa kiwango fulani, sera ya Uingereza iliitenga kutoka kwa Bara la Ulaya.

Kushambuliwa Kibinafsi

 

Ziara yake Marekani mwaka 1957 ilikuwa moja tu ya ziara zake nyingi ng'ambo

Lakini kufifia kwa ubabe wa Uingereza kuliharakishwa na mzozo wa Suez mwaka 1956, ambapo ilibainika wazi kwamba mataifa ya Jumuiya ya Madola hayakuwa na nia ya kuchukua maamuzi kwa pamoja wakati wa mizozo.

Uamuzi wa Uingereza kuwatuma wanajeshi kujaribu kuzuia Misri kutekeleza vitisho vyake vya kutaifisha Mfereji wa Suez ulimalizika kwa aibu ambapo Uingereza ililazimika kuondoa majeshi yake. Hatua hiyo ilisababisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Anthony Eden.

Hilo lilimtumbukiza Malkia kwenye mzozo wa kisiasa. Chama cha Conservative hakikuwa na mfumo wa kumteua kiongozi mpya, na baada ya msururu wa mashauriano, Malkia alimpa idhini Harold Macmillan kuunda serikali mpya.

Malkia alijipata akishambuliwa moja kwa moja na Lord Altrincham. Kwenye makala katika jarida moja, alidai kwamba washauri wa Malkia walikuwa na "Uingereza mwingi" na walikuwa wa "tabaka la juu" na alimtuhumu kwa kutokuwa na uwezo wa kutoa hotuba hata rahisi kiwango gani bila hotuba hiyo kuandikwa.

Tamko lake lilisababisha mtafaruku mkubwa kwenye vyombo vya habari na Lord Altrincham hata alishambuliwa na kupigwa akiwa barabarani na mwanachama wa kundi la kutetea ufalme lililofahamika kama League of Empire Loyalists.

Hata hivyo, kisa hicho kilidhihirisha kwamba jamii ya Uingereza na mtazamo wao kwa familia ya kifalme ni mambo yaliyokuwa yakibadilika sana na kwamba mambo ambayo yalienziwa na kuheshimiwa kwa miaka mingi bila kuhojiwa, sasa yalikuwa yanaulizwa maswali na kutiliwa shaka.

Kutoka kwa 'utawala wa Kifalme' hadi kwa 'Familia ya Kifalme'

Akitiwa moyo na mumewe, na huku akikosa uvumilivu kwa washauri wake wagumu wa mabadiliko, Malkia alianza kuzoea mtindo mpya.

Utamaduni wa kuwatambulisha wasichana wa makabaila baada yao kukomaa, kwa lengo la kuwatafutia wachimba miongoni mwa makabaila wengine au watu wa tabaka la watawala aliufuta. Kadhalika, alibadilisha matumizi ya 'utawala wa Kifalme' na badala kukawa kunatumiwa 'Familia ya Kifalme'.

Malkia alijipata tena katika mzozo wa kisiasa pale mwaka 1963 Harold Macmillan alipojiuzulu wadhifa wake kama waziri mkuu.

Chama cha Conservative kilikuwa bado hakijaandaa mfumo wa kumchagua kiongozi mpya.

Alifuata ushauri wa Harold wa kumteua Earl of Home kuwa waziri mkuu.

Ulikuwa ni wakati mgumu kwa Malkia, ambaye alikuwa na sifa za kutaka kufuata katiba, na familia ya kifalme ilitenganishwa zaidi na shughuli za kila siku za serikali.

Malkia alichukulia kwa uzito sana haki yake kufahamishwa mambo yaliyokuwa yakitendwa, haki yake ya kushauri na haki yake kutahadharisha - lakini hakuvuka mipaka katika kuzitumia.

Ilikuwa ni mara ya mwisho kwake kuwekwa katika hali kama hiyo. Chama cha Conservative hatimaye kilifutilia mbali utamaduni wake kwamba viongozi wapya wa chama waliibuka tu, na badala yake mfumo mahsusi wa kuamua nani atakuwa kiongozi mpya ukawekwa.

Kutulia

Kufikia mwisho wa miaka ya 1960, Buckingham Palace ilikuwa imeamua kwamba ilihitaji kuchukua hatua kuonyesha kwamba Familia ya Kifalme haikuwa na urasmi sana na ingeweza kufikiwa na raia kwa urahisi.

Matokeo yake yalikuwa ni makala ya aina yake kuhusu familia ya kifalme kwa jina, Royal Family. BBC iliruhusiwa kupiga video za jamaa wa familia ya Windsor wakiwa nyumbani.

Picha za video zilizopigwa zilikuwa zao wakichoma nyama, wakipamba mti wa Krismasi, wakiwapeleka watoto kwa matembezi wakitumia gari - zote ambazo zilikuwa shughuli za kawaida, lakini jambo ambalo hawakuwa wamewahi kuonekana awali wakifanya.

Wakosoaji walidai kwamba filamu hiyo ya Richard Cawston iliharibu dhana ya upekee wa familia ya kifalme kwa kuwaonyesha kama watu wa kawaida, ikiwa ni pamoja na kumuonyesha Mwanamfalme Mtawala wa Edinburgh, mumewe Malkia, akichoma soseji katika bustani katika kasri la Balmoral.

Lakini filamu hiyo iliendana na majira ya wakati huo ya kulegeza mambo na kutulia na ilichangia sana katika kurejesha uungwaji mkono wa familia ya kifalme kutoka kwa umma.

Kufikia mwaka 1977, wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya utawala wale yaani Silver Jubilee kulikuwa na furaha ya kweli miongoni mwa raia waliojitokeza kwenye sherehe barabarani na hafla nyingine zilizoandaliwa kote katika ufalme huo.

Familia ya kifalme ilionekana kuwa salama na kupendwa na wananchi, na hilo zaidi lilitokana na juhudi za Malkia mwenyewe.

Miaka miwili baadaye, Uingereza, kupitia Margaret Thatcher, ilimpata mwanamke wa kwanza waziri mkuu.

Uhusiano kati ya kiongozi wa nchi mwanamke na kiongozi wa serikali mwanamke wakati mwingine ulidaiwa kuwa usio mzuri sana.

Kashfa na majanga

Kitu kimoja kilichokuwa changamoto kwa Malkia kilikuwa ni kujitolea kwake kwa Jumuiya ya Madola, jumuiya ambayo yeye alikuwa ndiye kiongozi.

Malkia Elizabeth aliwafahamu vyema viongozi wa jumuiya hiyo waliotoka Afrika na aliunga mkono juhudi zao.

Anadaiwa kuutazama msimamo wa Thatcher ambao ulikuwa mkali na wa 'vita' kama wa kushangaza, na zaidi alishangazwa na hatua ya waziri mkuu huyo kupinga kuwekewa vikwazo kwa watawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

Mwaka baada ya mwaka, Malkia aliendelea kutekeleza majukumu yake kwa umma.

Baada ya Vita vya Ghuba mwaka 1991, alikwenda ziarani Marekani na kuwa mtawala wa kwanza kwa kifalme wa Uingereza kuhutubia kikao cha pamoja na Bunge la Congress.

Rais George HW Bush alisema kwamba "amekuwa rafiki wa uhuru kwa muda mrefu zaidi, kadiri tunavyoweza kukumbuka."

Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye, msururu wa kashfa na mikasa ilianza kuiandama Familia ya Kifalme.

 Mwana wa pili wa Malkia, Mtawala wa York, na mke wake Sarah walitengana, huku ndoa ya Bintimfalme Anne na Mark Phillips nayo ikivunjika kupitia talaka. Kisha, Mwanamfalme Mtawala wa Wales na mke wake wakafichua kwamba ndoa yao ilikuwa inayumba na kisha wakatengana.

Mwaka huo ulimalizika kwa moto mkubwa katika makao aliyoyapenda sana Malkia, Windsor Castle.

Ilionekana kama ishara ya kusikitisha ya mambo yalivyokuwa katika nyumba ya kifalme. Mambo yalifanywa mabaya zaidi kutokana na mzozo wa hadhara wa iwapo ni mlipa kodi, au Malkia, aliyefaa kugharimia ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa na moto.

Heshima mijadala ikiendelea

Malkia aliueleza mwaka 1992 kama "mwaka wa mikasa na majonzi" na katika hotuba katika Jiji la London, alionekana kukiri kwamba kulihitajika kuwa na familia ya kifalme yenye uwazi zaidi navyo vyombo vya habari visiishambulie sana familia hiyo.

"Hakuna taasisi yoyote, jiji, familia ya kifalme, inaweza kutarajia kutopigwa darubini na wale wanaoweka imani yao kwayo na kuiunga mkono, bila kutaja wale ambao hawafanyi hivyo. Lakini sote ni sehemu ya kitambaa kimoja cha jamii ya taifa na upigaji darubini unaweza kufanikiwa iwapo utafanywa kwa ustaarabu kiasi bila makali, kwa ucheshi ufaao na kwa ufahamu." 

Taasisi ya familia ya kifalme ilikuwa kwa kiwango kikubwa kila wakati inajitetea na kujikinga.

Buckingham Palace ilifunguliwa wazi kwa umma, ambapo watu walilipa kuruhusiwa kuingia, ili kuchangisha pesa za ukarabati Windsor. Na ilitangazwa kwamba Malkia na Mwanamfalme mtawala wa

Nje ya nchi, matumaini ya Jumuiya ya Madola, ambayo alikuwa nayo mapema mwanzoni mwa utawala wake hayakuwa yametimia.

Uingereza ilikuwa imewatenga washirika wake wa zamani, huku ikiangazia mpangilio mpya wa ushirikiano Ulaya

Malkia bado alitazama Jumuiya ya Madola kama kundi lililokuwa na thamani na alifurahia sana Afrika Kusini, ambapo alikuwa amekomalia, ilipotupilia mbali utawala wa ubaguzi wa rangi. Alisherehekea hilo kwa ziara Machi 1995.

Nyumbani, Malkia alitafuta kudumisha heshima kwa familia ya kifalme huku mjadala wa umma ukiendelea kuhusu iwapo taasisi hiyo ilikuwa na manufaa yoyote za siku za baadaye. 

Kifo cha Diana, Princess wa Wales

Uingereza ilipokuwa inahangaika kutafuta mustakabali mpya mambo yalipokuwa yanabadilika duniani, alisalia kuwa mtu wa kutoa matumaini, kwa tabasamu yake.

Jukumu aliloliezi zaidi lilikuwa kuwa kama ishara ya umoja wa taifa.

Hata hivyo, familia ya kifalme ilitikiswa na Malkia akajipata akikosolewa sana, jambo ambalo halikuwa kawaida, baada ya kifo cha Diana, Binti mfalme wa Wales, katika ajali ya barabarani Paris mnamo Agosti 1997.

Umma ulipokusanyika katika makasri London na kuweka mashada ya maua na ujumbe wa pole. Malkia alionekana kusita kutoa mwelekeo kama ilivyokuwa kawaida kwake awali wakati wa matukio makubwa ya kitaifa.

Wengi wa wakosoaji wake walishindwa kufahamu kwamba alikuwa ametokea kwenye kizazi ambapo haikuwa kawaida kujionyesha hadharani ukiomboleza na kuhuzunika, kama ilivyoonekana miongoni mwa umma baada ya kifo cha Diana. 

Pia alihisi wajibu, kama bibi, kwamba alihitaji kuwafariji wana wa Diana faraghani kwenye familia.

Mwishowe, alitoa hotuba ya moja kwa moja kupitia runinga, ambapo alitoa heshima zake na kumsifu Diana, kama mkwe wake na kisha katoa ahadi kwamba familia ya kifalme ingezoea maisha bila yeye.

Hasara na sherehe

Vifo vya Mama Malkia (mamake) na dadake Malkia Elizabeth, Bintimfalme Margaret, mwaka wa kusherehekea miaka 50 ya uongozi wa Malkia, yaani Golden Jubilee, mwaka 2002, kulitandaza kivuli cha huzuni kwenye maadhimisho ya mafanikio hayo kote nchini humo.

Lakini licha ya hayo, na mjadala uliokuwa ikiibuka mara kwa mara kuhusu umuhimu wa familia ya kifalme siku za usoni, watu milioni moja walikusanyika katika barabara maarufu ya The Mall, mbele ya Buckingham Palace, kwa sherehe za jioni za kusherehekea miaka 50 ya uongozi wa Malkia.

Aprili 2006, maelfu ya watu walikusanyika barabara za Windsor Malkia alipokuwa anafanya matembezi yasiyo rasmi kama sehemu ya kusherehekea kutimiza miaka 80.

Na Novemba 2007, yeye na Prince Philip walisherehekea miaka 60 ya ndoa yao katika ibada iliyohudhuriwa na watu takriban 2,000 katika kanisa la Westminster Abbey.

Kulikuwa na hafla nyingine ya furaha Aprili 2011 Malkia alipohudhuria harusi ya mjukuu wake, William, Mwanamfalme mtawala wa Cambridge, na Catherine Middleton.

Na Mei mwaka huo, akawa kiongozi wa kifalme wa kwanza wa Uingereza kuzuru Jamhuri ya Ireland, tukio lililokuwa na umuhimu mkubwa kihistoria.

Katika hotuba, ambayo alianza kuitoa kwa lugha ya Kiairishi, alitoa wito wa kuvumiliana na maridhiano, akirejelea "mambo ambayo tunatumai yangetendwa kwa njia tofauti au hayangetendwa hatakidogo."

Kura ya maamuzi

Mwaka mmoja baadaye, katika ziada Ireland Kaskazini, kama sehemu ya sherehe za Diamond Jubilee, alisalimiana kwa mkono na kamanda wa zamani wa IRA Martin McGuinness

Ulikuwa na wakati wa kihistoria kwa Malkia ambaye binamu yake aliyempenda sana, Lord Louis Mountbatten, aliuawa na bomu lililolipuliwa na IRA mwaka 1979.

Maadhimisho ya Diamond Jubilee yaliwaleta pamoja mamia ya maelfu ya watu ambao walijitokeza barabarani na kwa sherehe za kilele wikendi jijini London.

Kura ya maamuzi kuhusu uhuru wa Scotland iliyofanyika Septemba 2014 ilikuwa mtihani kwa Malkia.

Watu walikuwa hawajaisahau hotuba yake kwa Bunge mwaka 1977 ambapo aliweka wazi kujitolea kwake kuendeleza Uingereza ikiwa moja. 

"Nahesabu wafalme na mamalkia wa England na Scotland, na wanawafalme watawala wa Wales kama miongoni mwa mababu zangu na kwa hivyo nafahamu azma hizi. Lakini siwezi kusahau kwamba nilitawazwa Malkia wa Ufalme wa Uingereza wa Britain Kuu (England, Wales na Scotland) na Ireland Kaskazini."

Katika tamko lake kwa waliofika kasri la Balmoral kumtakia heri mkesha wa kura ya maamuzi kuhusu uhuru wa Scotland, ambalo bila shaka alikusudia lisikike, alisema alitumai kwamba watu wangefikiria kwa makini sana kuhusu siku zao za baadaye.

Matokeo ya kura hiyo yalipofahamika, hotuba yake kwa umma ilisisitiza furaha aliyokuwa nayo kwamba Muungano ulisalia imara, ingawa alitambua kwamba mazingira ya kisiasa yalikuwa yamebadilika.

"Sasa, tunaposonga mbele, tunafaa kukumbuka kwamba licha ya mitazamo mbalimbali ambayo imeoneshwa, tuna upendo wa pamoja usio kifani kwa Scotland, ambao ni moja ya mambo yanayotuunganisha sote."

Katika miaka yake ya baadaye, Malkia alijiondoa katika maisha mengi ya umma ingawa alionekana kwenye roshani kwenye Jumba la Buckingham kusherehekea Jubilee

Mnamo 9 Septemba 2015 aliibuka kuwa mtawala wa kifalme aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Uingereza, na kupita rekodi ya bibi wa bibi yake Malkia Victoria.

Kama kawaida yake, alikataa kujisifu na kujipigia debe na kusema kwamba sifa hizo zilikuwa "kitu ambacho sikuwahi kukitarajiwa wala kukitamania.2

Chini ya mwaka mmoja baadaye, Aprili 2016, alisherehekea kutimiza miaka 90.

Aliendelea na majukumu yake ya umma hadi miaka ya tisini, mara nyingi peke yake baada ya kustaafu kwa Duke wa Edinburgh mnamo 2017.

Kulikuwa na matatizo katika familia - ikiwa ni pamoja na ajali ya gari ya mumewe, urafiki usio mzuri wa Duke wa York na mfanyabiashara wa Marekani aliyehukumiwa, na Prince Harry kukatishwa tamaa na maisha katika familia ya kifalme.

Hizi zilikuwa nyakati za kusumbua, zilizosimamiwa na ufalme ambao ulionyesha kuwa bado ulikuwa na udhibiti thabiti. Kulikuwa pia na kifo cha Prince Philip mnamo Aprili 2021, katikati ya janga la Covid.

Ingawa ufalme haungekuwa na nguvu mwishoni mwa utawala wa Malkia kama ilivyokuwa mwanzoni, alidhamiria kwamba unapaswa kuendelea kuamuru mahali pa upendo na heshima katika mioyo ya watu wa Uingereza.

Katika hafla ya Silver Jubilee(Maadhimisho ya miaka 25), alikumbuka ahadi aliyokuwa ameweka katika ziara ya Afrika Kusini miaka 30 kabla.

"Nilipokuwa na umri wa miaka 21, niliyatoa maisha yangu kwa huduma ya watu wetu na niliomba msaada wa Mungu ili kutimiza kiapo hicho.

Ingawa ahadi hiyo iliwekwa katika siku zangu za ujana, nilipokuwa sina ufahamu kuhusu maamuzi yangu, sijutii; au kuondoa neno moja kwake."


Imeandikwa kwa msaada wa BBC






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags