Wanawake nchini wametakiwa kuendelea kuchukua jukumu la kuongelea na kukataa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyofanywa dhidi yao na watoto.
Pia wametakiwa kuunganisha nguvu zao kwa pamoja katika kulishughulikia zaidi suala hilo katika ngazi zote ikiwemo ngazi ya familia.
Akizungumza hayo leo jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa semina ya mafunzo kwa wanawake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa kuwasaidia Wanawake, Mary Rusimbi amesema suala la ukatili wa kijinsia ni pana na ni refu na sio tu uwe wa kupigwa kwa wanawake.
“Mara nyingi watu wanajua ukatili ni ule wa kupigwa tu kwa wanawake, lakini ukiangalia linamapana marefu, leo naona watu wameungana na kuangalia kwa mapana yake suala la ukatili wa kijinsia katika kipindi hiki cha siku 16 za kupiga ukatili huo,” amesema.
Mary amesema suala la ukatili wa kijinsia limekuwa likishughulikiwa miaka mingi licha ya kuwepo kwa sheria lakini bado wanaona ukiendelea katika jamii.
Amesema vitendo hivyo vinaendelezwa kutokana na uwajibikaji kutokuwa mzuri hivyo amesema ni kuhakikisha jamii inazidi kupaza sauti na kufichua vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na watu.
“Ukatili wa kijinsia unadhoofisha watu kimaendeleo na kunyang’anywa haki na utu katika jamii na kufanya watu kuishi kwa hofu muda wote,”amesema na kuongeza
“Nimefurahi sana kukutana na wakiamama wa Tabata najua watatoka na mikakati ambayo watafanyia kazi kwa ngazi ya jamii,”alisema
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake ya Tapo Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tabata Women Tapo, Stella Mbaga amesema taasisi yao imeamua kuwaunganisha wanawake wa tabata kwa lengo la kuwaelimisha juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia.
Amesema mkutano huo ni muendelezo wa mikutano wanayofanya katika Tapo yao ya kuwakutanisha wanawake na kuwafundisha vitu mbalimbali ikiwemo masuala ya kiuchumi na kijamii.
“Siku kama hizi uwa tunajumuika na wamama na kuadhimisha siku 16 ya ukatili wa kijinsia na maadhimisho hayo yameenda sambamba na siku ya ukimwi duniani ambapo wapo wamama waliofanyiwa ukatili wa kijinsia na kusababishiwa maambukizi hayo ya ukimwi,”anesema.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Msimbazi,Godfrey Kizigo amesema taasisi hiyo,imekuwa msaada mkubwa kwa mtaa wake katika kusaidia wanawake kujitambua na kuwa vinara wa kufundisha watu wengine juu ya masuala ya ukatili
Leave a Reply