Wanawake Wanapokuwa na maswali magumu kwa wenza

Wanawake Wanapokuwa na maswali magumu kwa wenza

Na Shaban Kaluse

Wanawake ni watu wenye utambuzi wa hali ya juu sana kwenye suala zima la mapenzi. Unaweza kusema neno moja tu na kupitia neno hilo wakajua kwa usahihi kabisa kwamba unamaanisha nini au wewe ni mtu wa aina gani. Kuna jambo moja ambalo huwa wanaume hawalijui. Ni kwamba pale unapomdanganya mwanamke wakati unapomtongoza na ukampata, si kwamba umempata kwa sababu ya uongo wako, bali ni kwa sababu mwanamke huyo amekupenda, vinginevyo wala usingempata.

Hapa sizungumzii yale mapenzi ya kimaslahi, yaani mwanamke anampenda mwanaume kwa kuangalia rasilimali anazomiliki. Nazungumzia mapenzi ya dhati, mapenzi yanayounganisha mioyo ya wapendanao. Mapenzi ya watu wanaozungumza lugha moja, wanaokamilishana, wanaopendana bila masharti. Hayo ndio ninayoyazungumzia.

Hivyo basi wanaume wanatakiwa wawe makini sana na kauli zao pale wanapokuwa na wenzi wao. Hapa nazungumzia wapenzi wapya wanaoanza kuwa na mitoko kwa ajili ya kufahamiana.

Hapa chini nitataja baadhi ya maswali ya mitego wanayouliza wanawake kwa nia ya kujua aina ya mwanaume anayetoka naye:

1.Unauonaje uhusiano wetu?

Kama jibu lako la haraka haraka litakuwa ni kutarajia kufunga ndoa na kuzaa watoto nk. Unaweza kumpoteza huyu mwandani wako, kwani kwake yeye atakuona kama unataka kumgeuza mashine ya kutotolea watoto na si vinginevyo. Jibu kama, "nina furaha sana kuwa nawe na sioni kama kuna jambo litakalotutengenisha kati yangu na wewe, huwa najisikia fahari kuwa karibu nawe na nina mararajio makubwa juu yako iwapo mambo yataenda vizuri". Kauli hii inapopenya katika masikio ya mwanamke inamfanya ajisikie fahari sana na ajione kama vile amelamba dume.

2.Ninaonekanaje na nguo hizi nilizovaa?

Mwanamke anapouliza swali la aina hii, anatarajia mwanaume atoe maoni yake si kwa vazi alilovaa kiujumla bali pia anataka kujua maoni ya mwanaume juu kitu fulani kuhusu vazi hilo. Wanawake wangependa kusikia kuhusu rangi ya vazi hilo kama limeendana na ngozi yake ya mwili au aina ya mtindo alioshona kama unamfanya awe na mwonekano gani kulingana na umbo lake.. Je vazi hilo limem-shape vyema nk. Kama ukipatia namna ya kumsifia kulingana na jinsi alivyopendeza lakini bila kutia chumvi utakuwa katika nafasi nzuri ya kudumisha uhusiano. Wanawake ni wajanja sana, iwapo utamsifia kwa kutia chumvi atakusitukia na kukuoana mzushi..

3.Je hutojali iwapo nikikuomba unisaidie?

Jibu kwa swali hilo ni "Sitojali." Na haraka sana unatoa msaada hata kama hujapenda kutoa msaada huo, wanawake wanapoomba msaada kwa wapenzi wao hawataraji jibu la hapana au vijisababu vya kutaka kuhalalisha kutotoa msaada. Kwa kawaida wanaume ni waungwana sana wanapoombwa msaada na si kwa mpenzi wake tu, bali mwanamke yeyote yule. Kwa kawaida mwanaume anakuwa mwepesi kutoa msaada, hata kama sio wa moja kwa moja, lakini hata mawazo yatakayosaidia kupatikana suluhu ya kile mwanamke alichotaka kusaidiwa. Mwanamke atashangaa sana kusikia jibu la hapana kutoka kwa mpenzi wake na jibu hilo litamfanya amuone mpenzi wake kama mtu asiyejali...

 

 

4.Je unawaonaje marafiki zangu?

Kuna msemo mmoja unasema, "unaweza kumjua mtu kutokana na marafiki zake waliomzunguka." Mwanamke anapouliza swali kama hilo hawatarajii jibu moja tu. Kwa mfano jibu kama, "ni wazuri," au "ni wachakaramu sana." Jibu hilo haliwezi kumridhisha mwanamke hata kidogo. Iwapo utawaponda marafiki zake hilo litakuwa ni kosa kubwa, kwani kama utawakosoa kama vile wana tabia zisizofaa, basi atahisi kuwa na yeye umemuweka kwenye kundi la wanawake wenye tabia zisizofaa. Kwa hiyo mwanamke anapokuuliza kama unawaonaje marafiki zake anatarajia ueleze kwa undani jinsi unavyowaona hao marafiki zake, kwa kufanya hivyo atajua kwamba unampenda na kumjali. Sifa za ziada kuhusu huyo mpenzi wako na mmoja wa marafiki zake zinaweza kumfanya mpenzi wako ajisikie vizuri. "Wewe na Sia mnavutia sana mkiwa pamoja, maana kila nikiwakuta mko pamoja mnakuwa ni watu wenye furaha wakati wote, huku mkitaniana na kuongea kwa bashasha. Inaonyesha ni kiasi gani mnapendana sana na mnasaidiana kwa hali na mali." Unaweza kutoa maoni ya aina hiyo.

5.Vipi, mwishoni mwa juma hili utakuwa na shughuli gani?

Iwe una shughuli au huna, wanawake huwa hawapendi kuwekwa roho juu, linapokuja suala la miadi. Iwapo utamwahidi kuwa mtakuwa na mtoko, basi hakikisha kweli mnatoka na kwa muda mliopanga. Utafanya kosa kubwa iwapo utamwahidi mpenzi wako kwamba mtatoka halafu usitokee... Suala la miadi huwa linapewa uzito mkubwa na wanawake. Iwapo mwanaume atakuwa na kauli kama, "nitaangalia," au "labda tutapanga kuwa na mtoko juma lijalo." Kauli za namna hii huwa wanawake hawazipend. Ni vyema mwanaume akawa na uhakika wa kile anachomwahidi mpenzi wake, kama hana uhakika na ratiba yake ni vyema asiahidi. Kama yuko bize yuko bize tu, ya nini kubahatisha. Wanawake wengi huwa hawapendi tabia ya kukurupushwa.

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags