Wanaume na wanawake hudanganya, hilo halina ubishi, lakini sidhani kama kuna sababu iliyo nzuri katika kuelezea jambo hilo, kwamba kwa nini wanaume na wanawake hudanganya katika mapenzi.
Nitajaribu kuwaeleza sababu (Lakini sababu hizi ni za wapenzi wapya.)
Ninachoweza kusema ni kwamba wanawake na wanaume hudanganya lakini wakiwa na sababu tofauti. Katika mapenzi kila mmoja anajaribu kukwepa kumuumiza mwenzake kihisia na hapo ndipo wanawake na wanaume hujikuta wakidanganya. Wanaume wengi hudhani kwamba kwa kuwa wanawake ni viumbe wenye hisia basi hawawezi kukubali kuambiwa ukweli na hapa chini nitataja mifano ya uongo mzuri (sijui kama ni sahihi kuita hivyo) ambao wanaume huutumia ili kuepusha shari na wenzi wao.
Mh, we ni mpishi mzuri….!
Kama inatokea siku mapishi yanakutupa mkono na unagundua kwamba chakula ulichopika hakina ladha au mchuzi umechachuka, ni vyema ukakiweka kando na kutafuta namna nyingine. Unaweza kwenda kununua chakula kwenye mighahawa ya karibu (Take Away) na kumuandalia mpenzi wako. Usitarajie mpenzi wako akakwambia chakula ni kibaya, atakisifia sana na huenda akakila chote ili kukuridhisha, lakini moyoni mwake anajua hicho chakula hata mbwa asingethubutu kukitoa mdomoni…. Anachofanya ni kuepusha shari ili amani iendelee kuwepo.
Kweli vile sikupata ujumbe wako wa simu…
Inaweza kutokea mwanaume anataka kutoka kidogo na marafiki zake baada ya kutoka kazini, lakini anashindwa kumweleza mpenzi wake kwa kuhofia maswali, hivyo huamua tu kuungana na marafiki zake na kuiweka simu yake silence ili kuepuka simu za mpenzi wake atakapopiga ili kujua amechelewa wapi. Atakaporudi nyumbani na kuulizwa na mkewe mahali alipokuwa, atasingizia kazi nyingi, foleni za magari au atasingizia kwamba simu yake ina tatizo la network nk. Kwa hiyo ukikutana na utetezi wa aina hii kubali yaishe.
Leo nitalazimika kufanya kazi hadi usiku…
Wakati mwingine kama mwanaume ana mishemishe zake na anahisi atachelewa, ili kuepusha maswali atakayoulizwa na mpenzi wake anatoa taarifa mapema kuwa atachelewa kurudi kwa kuwa kuna kazi muhimu au kuna ripoti anaiandaa ambayo ni muhimu sana. Kwa kutoa taarifa ya aina hiyo mapema, anajua kabisa kwamba ataepusha usumbufu wa kupigiwa simu mara kwa mara na kuulizwa yuko wapi. Sio kwamba analazimika kusema uongo wa aina hiyo kwa sababu anayo dhamira ovu, la hasha, inaweza kuwa anataka kujiunga na marafiki zake kwa ajili ya kupata kinywaji au kuangalia mechi muhimu na marafiki zake na asingependa kupata usumbufu wa mara kwa mara wa kupigiwa simu ili kuulizwa mahali alipo na anachokifanya. Sitetei kwamba ni sahihi wanaume kufanya hivyo bali ninachojaribu kueleza hapa ni kuwajulisha wanawake kwamba jambo hilo huwa lipo.
Nitakupigia…..
Inatokea mwanamke anakutana na mwanaume kwa ule mtindo wa chapchap, wazungu wenyewe huita one night stand. Baada ya kumalizana, mwanaume anaagana na mwanamke akimwahidi kwamba atampigia simu baadae. Naomba mfahamu kwamba kwa mwanaume kusema atakupigia, ana maanisha huenda atapigia simu. Ni wanaume wachache sana wanaoweza kutimiza ahadi walioweka ya kupiga simu baadae kwa mpenzi waliyeachana muda mfupi uliopita. Ili kuondokana na jakamoyo ni vyema ukaendelea na shughuli zako na wala usiwe na matumaini makubwa ya kusubiri kupigiwa simu. Iwapo atapiga sawa, lakini akipotezea haitakuumiza.
Wala nilikuwa simwangalii yeye…..
Hiki nacho ni kichekesho cha uongo wa wanaume. Inaweza kutokea mwanaume yuko na mwenzi wake wanatembea, mara wanakutana na mwanamke akiwa na hamsini zake, lakini mwanaume huyu anageuka kumtazama mwanamke huyo na anajisahau kiasi cha kumsindikiza kwa macho. Mara nyingi wanaume hupenda kukodolea macho matiti ya wanawake, makalio au eneo lolote la mwanamke linaloamsha hisia za mapenzi. Inapotokea akaulizwa na mwenzi wake kwamba kwa nini anamkodolea macho mwanamke fulani, mwanaume huyo atakanusha vikali kwamba hakuwa anamuangalia huyo mwanamke wakati ni dhahiri kabisa alikuwa anamkodolea macho. Kwa kawaida wanaume hukodolea wanawake macho bila wao kujijua na ndio maana hufanya hivyo hata wakiwa na wenzi wao, lakini cha ajabu wakiulizwa hukanusha vikali.
Leave a Reply