Wanaume wanaooa ‘nyumba ndogo’ huwa hawadumu nazo

Wanaume wanaooa ‘nyumba ndogo’ huwa hawadumu nazo

Bila shaka mmeshawahi kusikia wanawake walioachwa au kutelekezwa na waume zao wakidai kwamba waume hao watawakumbuka. Bila shaka pia mmeshawahi kusikia kuhusu wanawake ambao walisababisha ndoa za wanawake wenzao kuvunjika, ambao nao baada ya kuolewa, ndoa zao zimekuja kuvunjwa na wanawake wengine.

Kusikia kwa matukio kama hayo hakutokani na unasibu (coincidence) wa mambo, bali ukweli wa kimaumbile ambao hakuna mtu anayeweza kupingana nao. Katika maisha kuna kanuni za kimaumbile ambazo ni kazi bure binadamu kujaribu kubishana nazo. Ni upotezaji wa muda, kwa mfano mtu kujaribu kupinga tendo la jiwe kuzama majini linapotupwa ndani ya maji.

Hali ya kimaumbile pia inatawala uhusiano wetu. Hebu fikiria juu ya mtu ambaye anamdharau mkewe na kumtelekeza au kumuacha kwa sababu amepata mwanamke mwingine bora zaidi. Ninavyofahamu mimi ni kwamba kunapokuwa na tatizo katika ndoa wanandoa hukaa na kujadili njia za kulitatua.

Inaposhindikana kabisa ndipo kutengana au kuachana hutokea. Mwanaume ambaye hutafuta ‘nyumba ndogo’ wakati akiwa bado na ndoa yake na baadae kuamua kufunga ndoa ya wazi au ya siri na ‘nyumba ndogo’ hiyo ni mwanaume ambaye hata mtu asiye na elimu ya nafsi atajua kwamba ana matatizo ya kisaikolojia.

Sababu ya kutafuta nyumba ndogo…

Kuna sababu nyingi ni kwa nini wanaume huwa na ‘nyumba ndogo’, lakini sababu zote hakuna hata moja inayoweza kuhalalisha jambo hilo. Kwa muktadha huo tuache kwanza kuhusu sababu hizo, bali tujadili msingi au mahali zinapochipukia tabia hizo. Mtu anayetafuta ‘nyumba ndogo’ ni mtu ambaye haridhishwi na mkewe katika mambo fulani, bila kujali kama ni mambo ya kinyumba au nje ya hayo.

Mtu huyu anaamini, hata kama sio waziwazi bali nyuma ya ubongo, kwamba hiyo ‘nyumba ndogo’ ndiyo yenye ukamilifu, ndiyo inayoweza kuchukuwa nafasi ya mke ambaye ana kasoro. Bila shaka mmeshawahi kusikia wanaume na hata baadhi ya wanawake wakisema kwamba mke mjeuri inabidi atafutiwe mke mwenzie, yaani mke mdogo.

Hawa wana maana kwamba, mwanaume akiona udhaifu kwa mkewe inabidi atafute mwingine ili kuziba pengo hilo na pia kumtia adabu huyu mke wa kwanza. Lakini udhaifu huu unakuwa ni wa kupewa nguvu tu. Kama kuna uchovu wa hisia, yaani mwanaume ameanza kuchujukiwa na penzi la mkewe katika hali mbalimbali dawa au suluhu ya uchovu huu si kutafuta ‘nyumba ndogo’

Kutafuta Suluhu…

Kama mwanaume ambaye suluhu ya kuchoka kwa hisia zake au kuchuja mapenzi kama kunavyoitwa ni kutafuta mwanamke mwingine, ni wazi hawezi kuishi na mwanamke mmoja. Atatafuta mwanamke wa pili ambaye naye hisia zake zitamchoka na hivyo kuhitaji mpya atakayeziamsha hisia hizo, ambaye naye baada ya muda fulani atakuwa hivyo. Inakuwa ni mtindo wa maisha yake kuwabadilisha wanawake kama nguo.

Tafiti za hapa nchini zinaonyesha kwamba kila wanaume saba kati ya kumi ambao huwaacha wake zao na kuoa ‘nyumba ndogo’, baadae ndoa zao na nyumba ndogo hizo huvunjika. Hebu fikiria ni wanaume watatu tu kati ya kila kumi ambao wataweza kuendelea kuishi na ‘nyumba ndogo’ zao, wengine saba wataangukia kwenye kutafuta au kuona ‘nyumba ndogo’ nyingine.

Nawaomba wale wanawake ambao huwa wanafanywa ‘nyumba ndogo’ na baadae kuja kuolewa, wasidhani wamefika mwisho wa safari zao. Nao wataachwa kama wenzao baada ya nyumba ndogo nyingine kupatikana.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post