Wanaotafsiri filamu wakiri kushuka kwa soko

Wanaotafsiri filamu wakiri kushuka kwa soko

Baada ya kutamba kwa zaidi ya miaka 10 ya ma-DJ wa kutafsiri filamu za kigeni na kulitikisa soko kwa aina yake, sasa baadhi yao wanakili kuwa soko la uuzwaji wa filamu hizo linashuka kutokana na kuwepo kwa waingiza sauti (dubbing) wengi nchini.

Akizungumza na Mwananchi Scoop leo Agosti 7, 2024 Abdallah Omary ‘Dj Dullay’ ameweka wazi kuwa soko la kutafsiri filamu kwa sasa limeshuka ukilinganisha na zamani huku akiongezea kuwa kwa sasa wanafanya ili kuikuza tasnia hiyo waliyoichagua.

“Soko la kutafsiri filamu kwa sasa siyo zuri kama ilivyokuwa mwanzo, watu wengi wamehamia kutazama filamu za kwenye visimbuzi na kwingineko kwa sababu mbalimbali kwani maisha tuliyokua tunapata awali siyo sawa na sasa mwanzo tulianza kutumia VH, CD, Flash kwa hiyo na sisi tunaotafsiri filamu hatuna tofauti na wanaomiliki mabasi ya mikoani dhidi ya SGR,” amesema Dj Dullay

Kuhusu kudanganya, kutafsiri maneno ambayo hayajaongelewa kwenye filamu

“Kwenye filamu zetu sisi huo hatudanganyi lakini kwenye hizi filamu sisi tunakuwa kama washehereshaji kwa hiyo kuna muda unazungumza ukweli lakini kuna muda unatakiwa unaweka maneno yako ya kuichangamsha filamu, kuna wengine wanajua lugha lakini wanafuatilia filamu hizo kutokana na mbwembwe za Dj filamu na ndiyo kitu wanachokipenda baadhi ya watu” amesema Dj Dullay

Hata hivyo amepingana na baadhi ya watu kudai kuwa soko la kutafsiri filamu limekufa kabisa kwani filamu bado zinauza lakini siyo kwa ukubwa ule wa hapo mwanzo

“Sisi filamu zetu mpaka sasa hivi bado zinauza na siyo kwamba haziuzi hapana, tunaendelea kupambana na kuna juhudi mbalimbali ambazo zinaendelea kufanywa na viongozi wanaohusika na ‘grupu’ letu sisi ambao tunatfsiri filamu na kwa sasa tunapambani kutambulika zaidi ni jambo zuri sasa hivi tunatambulika na Serikali na tunavitambulisho rasmi kabisa kwa hiyo tunaendelea kupigania tuwe na uwezo wa kuwadhibiti wanaouza filamu zetu bila vibali,” alimalizia Dj Dullay

Naye Rajab Augustino Mangula ‘Dj Blaki’ amesisitiza kuwa kwa Bongo visimbuzi vimeteka soko hilo, hii ni kutokana na ubunifu wanaouonesha kupitia filamu wanazoziingizia sauti.

“Kwa hapa Bongo ndiyo ipo hivyo kuwa soko limeshuka kwani wanaoonesha filamu za kuingiza sauti (dubbing) wanafanya vizuri ni kutokana na ubunifu walionao, mfano mzuri filamu wanayoionesha sasa Azam ya ‘Karma’ niliitafsiri mimi toka mwaka juzi niseme tuu haikufanya vizuri kutokana na ubunifu wanaouonesha katika filamu zao” amesema Dj Blaki

Hata hivyo Dj huyo amepinga kuhusiana na kauli ya wanaoingiza sauti kudiwa kudanganya katika filamu zao kwa kuweka wazi kuwa kwa upande wake yeye anajua lugha ya ya Kingereza lakini wapo baadhi ya wanaoingiza sauti huku hawajui lugha yoyote huku akiwashutumu kuwa ndiyo waliowaharibia soko.

Kwa upande wake amefunguka kuwa yeye na kundi la wenzake wanaotafsiri filamu wana mpango wa kurudisha soko hilo kwani wanachokifanya wao ni tofauti kabisa na wanaorusha filamu zilizoingizwa sauti (dubbing).

“Mimi na wenzangu tuna njia nyingi za kurudisha utawala wetu kama hapo awali kwa sababu hizo ni Sanaa mbili tofauti kabisa wanachofanya wao na sisi ni tofauti kwani kwa sasa sisi huwa tunapeleka filamu zetu kwenye website moja ambayo ni kama Netflix, ambapo shabiki yetu analipia 3,000 kwa mwezi kufuatilia filamu zetu,” amesema Dj Blaki

Vile vile alikazia kuwa jambo lingine linaloendelea kuwafanya watambe mjini ni kuwa wanaotafsiri filamu wana kampuni yao iitwayo ‘Ajabu Ajabu’ ambayo inawasimamia kwenye kila kitu mfano kwenda kuperfom nje na kuangalia tunapataje fedha kupitia platifomu mbalimbali huku akitoa wito kwa Madj wenzie kuwa na ushirikiano.

Ukiachilia mbali mtazamo wa Ma-Dj hao, mwanadada Twalha Ibrahim ameweka wazi kuwa yeye huwa hakubali filamu zinazotafsiliwa kutokana na baadhi ya Madj kuwa waongo hivyo anaona ni vyema kufuatilia tamthilia zinazoingizwa sauti (dubbing).

“Sijui kwa wengine lakini kwa upande wangu mimi sipendelei kutazama filamu hizo kwani wengi wao ni waongo, wanatafsiri maneno ambayo hayapo kabisa kwenye filamu, sikatai kuwa pindi nilipokuwa mdogo nilikuwa nikizipenda sana lakini baada ya kujua lugha ya kingeleza kwa ufasaha nimeona ni vyema nikatafuta filamu kwenye site mfano Netflix kuliko kuwasikiliza madj hao wapotoshaji” amesema Twalha Ibrahim

Aidha hatukishia hapo pia tulizungumza na mwanamke mmoja ambaye mkazi wa Kigamboni jijini Dar es salaam ambaye aliomba jina lake lisiwekwe wazi, kwa upande wake yeye imekuwa tofauti kwani ndio filamu zinazo mchangamsha akiwa nyumbani.

“Mimi huwa nazikubali sana filamu zinazotafasiliwa na huwa sichagui ni Dj gani ananikosha mimi naangalia filamu ipi nzuri itakayo nivutia”amesema

Aliongezea kwa kudai kuwa mtazamo wake ni tofauti na wengine kuhusiana na filamu hizo kushuka soko kwani anadai kuwa zinamchangamsha wakati anapokuwa peke yake nyumbani na hii ni kutokana na kutokuwa na kazi ya kumfanya atoke nyumbani.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags