Kama tunavyojua chipsi ni moja ya vyakula maarufu, vinavyopatikana fastafasta na vinavyopendelewa Zaidi katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania lakini habari mpya na mbaya kutokana na ripoti ya utafiti ya hivi karibuni ni kwamba vyakula hivi vya kukaanga vinaweza kuwa na athari kubwa kwa binadamu upande wa afya ya akili.
Timu ya utafiti kutokea jijini Hangzhou nchini China imegundua kuwa watu wenye tabia ya kula vyakula vya kukaanga mara kwa mara haswa viazi vya kukaanga au chipsi wapo hatarini kukumbwa na hali ya wasiwasi kwa 12% huku asilimia saba wakiwa hatarini kukumbwa na huzuni au mfadhaiko wa akili (depression) kuliko wale wasio na tabia ya kula vyakula vya kukaanga.
Ulaji wa yyakula vya kukaanga mara kwa mara huleta athari mbalimbali za kiafya ikiwa ni pamoja na magonjwa kama shinikizo la damu, unene wa kupindukia na ndio maana watafiti wameshauri watu kupunguza matumizi ya vyakula vya kukaanga kwa nia mahususi ya kuboresha afya ya akili, kulingana na tafiti iliyochapishwa katika jarida la PNAS.
Kwa mujibu wa CNN, wataalam waliosoma lishe walisema matokeo haya ni ya awali tu na si lazima kwa asilimia 100 kuwa vyakula vya kukaanga vilisababisha changamoto za afya ya akili au watu wanaopata dalili za depression au wasiwasi ilisababishwa na ulaji wa vyakula vya kukaanga pekee.
Aidha mtafiti wa Chuo Kikuu cha Zhejiang Yu Zhang akiwa ndie mwandishi wa utafiti huo aliiambia CNN kwamba hakuna haja ya kuwa na hofu juu ya athari mbaya za vyakula vya kukaanga lakini ili kuishi maisha yenye afya bora, kupunguza matumizi ya vyakula vya kukaanga inaweza kusaidia kuimarisha afya yako ya akili.
Leave a Reply