VISA NA MIKASA: Sitakaa nimsahau mwanamke yule

VISA NA MIKASA: Sitakaa nimsahau mwanamke yule

Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1990, nililetwa na mjomba wangu kuja Dar baada ya kusota kijijini kwa ajili ya kuzungumza na mzee mmoja ambaye alikuwa anahitaji kijana wa kumsaidia shughuli yake fulani ambayo mimi niliwahi kuifanya siku za nyuma.

Nilipofika Dar, kesho yake nilipelekwa ofisini kwa huyo mzee maeneo ya Posta na mjomba wangu ambaye ndiye aliyekuwa akifahamiana naye.

Kwa bahati mbaya nilipofikishwa hapo ofisini kwa huyo mzee alikuwa ametoka hivyo mjomba wangu aliomba niwekwe hapo mapokezi ili nimsubiri na yeye akaondoka zake kwenda kwenye shughuli zake ferry.

Nilikabidhiwa kwa secretary wa yule bosi ili nimsubiri. Ile kukabidhiwa tu, alivyoniangalia, nilijua ana kisirani.

Unajua kuna jicho lingine mtu anakupiga hadi unaogopa hata kabla hajakusemesha. Basi, jicho la yule dada aliyekuwa amejichubua na uso wake kufanana kama pupa wa kipepeo liliniambia kwamba, sikuwa nahitajika hapo ofisini. Lakini kwa bahati yake mbaya, nilikuwa ni mgeni wa bosi wake, angefanya nini? Unajua, kuna watu ambao wenyewe, wanapima heshima, hadhi na thamani ya mtu kwa namna mtu huyo alivyovaa au anavyozungumza na sifa nyingine za nje. huyu dada alinipima kwa namna nilivyokuwa nimevaa, bila shaka na hata muonekano wangu kwa ujumla.

Wakati nasubiri hapo kwa mashaka makubwa, nilihisi mzigo wa tumbo, yaani kutaka kwenda kujisaidia. Nilivumilia kwa sababu, nilijua vyoo vya jengo kama lile nisingeweza kuvihimili. Nilijua ningeweza kuvumilia hadi nitakapotoka hapo, ili nikamalize shida kule Mwananyamala nilikofikia kwa mjomba wangu. Lakini tumbo halikuwa pamoja nami. Nilizidi kuhisi kuwa natakiwa kuelekea chooni haraka iwezekanavyo. Unajua ugali wa mtama na maharage yaliyoungwa kwa mawese unapotaka kufanya fujo zake, unafanya hasa. Ilibidi nimuulize yule dada mahali choo kilipo. ‘Mlango ule pale,’ alisema bila kunitazama.

Nilisimama na kwenda huko chooni. Nilipoingia humo ndani nilibabaika sana nikijiuliza choo ni kipi. Hatimaye kwa akili ya kuzaliwa nikajua ni kile kinu kilichokuwa mle ndani. Lakini nakaa vipi kwenye kinu hicho, ikawa shughuli pevu. Niliamua kudandia kwenye kinu hicho na viatu vyangu na kuanza kujisaidia.Nilipomaliza nilishuka na kuchukua karatasi ya choo (toilet paper). Hizi ninazijua, kwa sababu, hata kule kijijini kwetu Kideleko zinauzwa na huwa tunazitumia kupamba kwenye harusi.

Nilikuwa sijawahi kuzitumia hivyo nilichukua furushi kubwa sana la hizo karatasi na kujisafisha halafu nikazitumbukiza hapo kwenye kinu. Nilitoka na kurejea pale mapokezi. Yule sekretari kisirani, aliniangalia wakati nakuja na bila shaka alijua wazi matumizi ya choo kwangu yangekuwa ni mtihani wa Cambridge. Aliinuka na tulipishana, mimi nakaa na yeye anaelekea kule chooni nilikotoka. 

Sikujua kwamba anaenda kufanya ukaguzi, kwa hiyo sikujali. Lakini dakika moja tu baadae nilisikia sauti. ‘Wewe kaka uliyetoka chooni sasa hivi, ndiyo ustaarabu gani ule. Hebu nenda kafanye usafi kule, uondoe uchafu wako. Halafu uliona wapi mtu anapanda juu ya choo badala ya kukaa.’ Aliongea kwa kelele sana na wale wote waliokuwa pale mapokezi walikata shingo kumkagua huyo mshamba mchafu.

Niliduwaa kidogo, na yule dada alinishinikiza.  ‘Nenda kafanye usafi basi au hunielewi…! Wee choo kimekuwa kichafu utadhani tembo walikuwa wanaoga!’ Alizidi kusema yule dada na watu waliokuwa pale mapokezi walinicheka sana. Watu wasio na huruma kwa hisia za wengine. Nilisimama na kwenda kule chooni, ingawa sikuwa najua huo usafi unafanywa vipi. ‘Nenda kaflash, halafu safisha mle ulimokanyaga.’  Aliniambia wakati naenda nikiwa nimeelemewa kwa aibu.

Sikuwa najua maana ya kuflash. Niliingia mle chooni. Wakati najiuliza maana na namna ya kuflash, nilisikia mlango ukifunguliwa. Kijana mmoja alikuwa amesimama nyuma yangu. ‘Wewe si mgeni wa mzee?’ Aliniuliza. Nilisema, ‘ndiyo.’ Yule kijana alinimbia kwamba, atanisaidia kufanya usafi kwa sababu yeye ni mhudumu wa ofisi ile. ‘Huyu dada ana roho mbaya sana. Mtu akija kumwona bosi anachukia sana.’

Nilirudi mapokezi na aibu tele, kwani watu wote walikuwa wakinitazama mimi. Kwa bahati nzuri yule mzee alikuja. Pamoja na kufedheheshwa kule, alisema, niruhusiwe mimi kwanza kuingia.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post