VISA NA MIKASA: Nikasema nilikumbwa na jini mahaba

VISA NA MIKASA: Nikasema Nilikumbwa Na Jini Mahaba

Nilikuwa ndio nimemaliza kidato cha nne na kuja jijini Dar na kufikia kwa mjomba wangu aliyekuwa akiishi maeneo ya Tandale kwa Mkunduge ili aweze kunifanyia mpango wa kupata vibarua huko viwandani.

Pamoja na kusomea huko vijijini na kuwa ndio mara yangu ya kwanza kuja mjini lakini nilikuwa ni kijana machachari sana pale mtaani kutokana na ubitozi wangu wa kijijini.

Nilikuwa nimejijengea marafiki wengi pale mtaani na walikuwa wanapenda sana stori zangu za bushi, wakati huo mimi nilikuwa najua nawakoga kwa stori zangu, lakini kumbe walikuwa wananisanifu kwa lafudhi yangu ya kilugaluga.

Miongoni mwa watu waliokuwa wakivutiwa na stori zangu alikuwepo dada mmoja wa Kimakua ambaye alifahamika kwa jina la Cotilda. Tulikuwa tukiishi naye nyumba moja akiwa ndio ana miezi miwili tangu ahamie nyumba hiyo, sisi tukiwa tumepanga nyumba kubwa na yeye akiwa amepanga banda la uani.

Huyu dada alikuwa ni mzuri kwa kiasi chake hasa wa umbo maana alijaaliwa kuwa na kalio kubwa la mviringo mwenyewe nilikuwa napenda kuita kijungu na sura pia haikumuangusha. Alikuwa ni muuguzi na alikuwa anafanya kazi hospitali ya Magomeni wakati huo.

 Hakuwa ameolewa ila aliwahi kunidokeza kwamba anaye mchumba ambaye anasoma nje ya nchi. Alikuwa anapenda sana kupiga stori na mimi na alikuwa ananipenda sana, maana hata vijizawadi alikuwa anapenda kuniletea kila anaporudi kutoka kazini.

Mimi kama kijana ambaye sikuzoea upendo wa aina nyingine isipokuwa ule wa kingono nilianza kuutafsiri vibaya upendo ule. Ingawa alikuwa ananizidi umri labda kama miaka kumi hivi, lakini nilijua dhahiri kwamba dada Cotilda ananitaka, na nilijua anataka vijana shababi kama mimi ambao damu inachemka.

 Niliamini hivyo kwa sababu tangu ahamie katika nyumba tuliyokuwa tukiishi alikuwa anapenda sana kuongea na mimi na ni mimi pekee kati ya vijana tuliokuwa tukiishi katika nyumba ile ambaye nilikuwa naingia chumbani kwake, kupiga naye stori.

Kutokana na ukaribu ule, nilijikuta nikiingiwa na ibilisi na kutamani kumtongoza, maana nilikuwa najua tu kwamba ananitaka lakini nilijua hawezi kuniambia kwa sababu kwa kawaida wanawake huwa hawasemi bali husubiri watongozwe.

Nilianza mikakati yangu ya kumtongoza kwa kumchomekea vijineneno vya mapenzi nikiwa napiga naye stori, lakini akawa anageuza yale mazungmzo yangu kuwa utani, mie kwa ujinga wangu nikajua hiyo ndiyo kawaida ya wanawake ya sitaki nataka.

 Basi siku moja kulikuwa na msiba pale mtaani ikatokea watu wote tumetoka kwenda msibani. na pale nyumbani walikuwa wamebaki watoto pekee. Mida ya saa moja usiku shangazi alinitaka nirudi nyumbani nikakae na watoto kwa sababu kulikuwa hakuna mtu mzima. Nilipofika nyumbani nilipitiliza moja kwa kwa moja hadi uani ambapo nilikuta taa ikiwaka chumbani kwa dada Cotilda.

Nikajua atakuwa amerudi kutoka kazini, nikajiseme moyoni kwamba huo ndio wakati muafaka wa kuomba utukufu, na nilijua kwa sababu tuko peke yetu asingeweza kukataa, nilibisha hodi nikiwa na shauku, na hakuchukua muda akafungua mlango, aliponiona alinikaribisha ndani na moja kwa moja nikaenda kukaa kwenye kitanda.

Alionekana kushtuka kidogo, kisha akaniambia, lakini mbona kochi liko wazi kwa nini ukae kitandani' mimi kwa kutojua amekereka, nikamuuliza, kwani ni nani mwenye mamlaka ya kukalia kitanda hiki zaidi yangu?' hakunijibu bali aliguna tu, alikaa kwenye kochi na kisha akaendelea na kazi yake ya kufuma vitambaa vyake, nilinyanyuka na kuhamia kwenye kochi, na kumwambia, haya nimekuja kukaa karibu yako mpenzi usije ukaninunia bure.

Alinitazama usoni kisha akatabasamu. Mimi kuona lile tabasamu nguvu zikaniishia kabisa nikaona nisicheleweshe mambo, nikajikakamua na kumwambia, unajua Cotilda nakupenda sana na nimeshindwa kuvumilia nimeona leo nikwambie ukweli' Alishtuka kidogo kabla hajaniambia, ahsante kwa kunipenda, mbona hata mie nakupenda sana tu, kwani hata katika amri kumi za Mungu tumeambiwa tuwapende majirani zetu kama tunavyojipenda.

 
Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.

Latest Post